Header Ads

SHAHIDI:MINTANGA HAKUSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA



Na Happiness Katabazi


SHAHIDI wa nne upande wa Jamhuri katika kesi ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya Kilo 4.8 inayomkabili aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Ngumi la Ridhaa Tanzania (BFT), Alhaji Shaban Mintanga, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Charles Ulaya amedai mshtakiwa huyo alistahili kushtakiwa kwa kosa moja tu la kula njama na siyo kosa la kusafirisha dawa hizo.

SSP Ulaya, ambaye ndiye mpelelezi mkuu wa kesi hiyo na aliyeongoza askari wenzake kupekua makazi na ofisi mbili za mshtakiwa (Mintanga), alitoa maelezo hayo jana mbele ya Jaji Dk. Fauz Twaib wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakati akijibu swali la wakili kiongozi wa utetezi Jerome Msemwa anasaidiwa na Majura Magafu na Yassin Membar.

Swali hilo lilimtaka shahidi huyo, aieleze mahakama kama, kutokana na upelelezi wake aliyoufanya na vielelezo alivyovikusanya, alikuwa anaona Mintanga anastahili kushtakiwa kwa makosa mawili ya kula njama na kusafirisha kiasi hicho cha dawa za kulevya.

“Mtukufu Jaji na mimi ndiyo mpelelezi mkuu wa kesi hii na mimi ndiyo niliyemhoji mshtakiwa na nikaongoza askari wengine kufanya upekuzi. Mimi na askari mwenzangu mmoja, tulikwenda hadi nchini Mauritius kufanya upelelezi wa kesi hii na kuwahoji wale Watanzania sita, ambao ulikuwa ni msafara wa mabondia wa hapa Tanzania waliokwenda Mauritius kushiriki mashindano ya ngumi za ridhaa na nilivyowahoji hao Watanzania sita na mwanamke mmoja raia wa Kenya, walinieleza kuwa dawa zile hawakupewa na Mintanga, bali dawa zile walipewa na mtu mmoja ambaye anaitwa Mika, ambaye hadi sasa Jeshi la polisi halijafanikiwa kumkamata.

“Hivyo basi, kwa vielelezo vyote na ushahidi wote niliyoukusanya hapa Tanzania na kule Mauritius, nasema wazi kuwa mshtakiwa hakustahili kabisa kushtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya, badala yake mawakili wa serikali walipaswa kumshtaki mshtakiwa huyo kwa kosa moja la tu la kula njama,” alieleza SSP Ulaya na kusababisha watu kuangua vicheko vya chini chini mahakamani.

Aidha, SSP Ulaya alieleza kuwa, kimsingi kilichofanya mshtakiwa huyo afikishwe mahakamani ni simu yake yenye namba 0754 284887, kuonekana ilikuwa ikitumika kuwasiliana na kampuni ya usafirishaji ya Antelops Tours Agency kwa ajili ya kuwakatia tiketi mashabiki watatu, ambao nao waliongozana na msafara huo uliokamatwa nchini Mauritius. Lakini hata hivyo alivyotakiwa na mawakili wa utetezi kutoa kielelezo hicho kinachoonyesha simu hiyo ilikuwa ikiwasiliana na kampuni hiyo ya ukatishaji tiketi, shahidi huyo alidai kuwa, yeye katika upelelezi wake alikwenda katika kampuni ya simu ya Vodacom, akapewa kielelezo hicho (print out) na kwamba, alishakikabidhi kwa mawakili wa serikali, lakini hadi shahidi huyo anamaliza kutoa ushahidi wake, hakuweza kukitoa ili kiweze kupokelewa na mahakama.

Shahidi huyo akijibu maswali aliyoulizwa kwa mpigo na mawakili wa utetezi, Msemwa na Magafu, kuwa katika maelezo ya nyongeza aliyomchukua Mintanga katika mahojiano yao yaliyofanyika Makao Makuu ya Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, eneo la Kilwa Road jijini Dar es Salaam, Juni 20 mwaka 2008, kuwa, alimhoji mshtakiwa huyo kuhusu matumizi ya simu ya mkononi Na. 0754 284887 inayodaiwa kuwa ni ya mshtakiwa na alikuwa akiitumia kwa mawasiliano na kampuni Antelope Tours Agency, shahidi huyo alidai hakuwahi kumuuliza swali hilo mshtakiwa huyo.

Yafuatayo ni mahojiano baina ya mawakili wa utetezi Msemwa na Magafu na SSP Ulaya:

Wakili:
Tazama haya maelezo ya mshtakiwa aliyoyatoa mbele yako wakati unamhoji, kuna sehemu yoyote inaonyesha wewe ulimuuliza mshtakiwa matumuzi ya hiyo simu ambayo mnadai ni yake, alikuwa anaitumiaje?

SSP Ulaya: Hakuna sehemu inayoonyesha kuwa nilimuuliza swali hilo.

Wakili: Soma haya maelezo yako wewe shahidi, kuna sehemu yanaonyesha ulimhoji mshtakiwa kuhusu matumuzi ya namba hiyo ya simu?

SSP Ulaya: Mhhh! pia sikumuuliza swali hilo.

Wakili: Utakubaliana na mimi hiyo simu namba 0754 284887 unayodai ni ya mshtakiwa siyo mali ya mshtakiwa, bali ni simu ya ofisini kwa mshtakiwa?

SSP Ulaya: Mimi nilivyokuwa nikimchukua maelezo ya nyongeza, mshtakiwa huyo alinieleza simu hiyo ni yake.

Wakili: Soma hii ni Barua ya BFT inakwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa?

SSP Ulaya:Juu ya barua hiyo inaonyesha anwani ya BFT ni Box-15558 namba binafsi ya Mintanga ni 0773-257547, kazi na ofisi ni +255 0754-284887 .

Wakili:Kwa mujibu wa hizo nyaraka, si zinaonyesha simu hiyo ya Vodacom +255 0754-284887 si ni ya ofisini kwa Mintanga?

SSP Ulaya: Ndiyo (watu wakacheka).
Wakili:Ulivyooenda katika kampuni ile ya Antelope kufanya upelelezi wako, ulimhoji nani?

SSP Ulaya:Nilimhoji shahidi wa tatu, Godfrey Mroso na akaniambia namba hiyo ndiyo alikuwa akiwasiliana nayo na ikamtaka awakatie watu hao watatu, licha mwenye namba hiyo hajawahi kumtajia jina lake.

Wakili:Kama hivyo ndivyo, wewe ulisema kigezo pekee kilichokufanya upendekeze mshtakiwa afunguliwe kesi ni simu hiyo?

SSP Ulaya:Ndiyo, kwani nilikwenda hadi Vodacom nikaprint out mawasiliano ya namba hiyo.

Wakili: Hiyo print out umekuja nayo hapa mahakamani ili tuione?
SSP Ulaya:Sijaja nayo ila nakumbuka niliikabidhi kwa mawakili wa serikali.

Wakili:Utakubaliana na mimi hadi sasa hizo dawa za kulevya zilizokamatwa Maurtius hazijaletwa hapa nchini na kesi inayomkabili mshtakiwa ni kula njama na kusafirisha dawa hizo za kulevya Kg.4.8, na hatuoni kuwa hapa tunazungumzia hewa na kucheza mchezo wa kuigiza, kwani kielelezo ni dawa za kulevya na wewe kama mpelelezi mkuu pia hizo dawa za kulevya leo hujazileta hapa mahakamani kama kielelezo?

SSP Ulaya: Mmh! siwezi kusema hii ni kesi hewa na ninavyofahamu mimi hizo dawa bado hazijaletwa nchini.

Wakili:Katika upelelezi wenu, mliweza kubaini katika kipindi hicho cha mgogoro huo kama mshtakiwa aliwahi kwenda nchini Mauritius?

SSP Ulaya:Hatujagundua kama Mintanga aliwahi kwenda Mauritius.
Wakili:Huu uzito wa Kg. 6 wa dawa za kulevya uliupata?

SSP Ulaya: Mauritius ambapo walipowakamata Watanzania wale walilitumia jeshi la Polisi Tanzania kuwa, dawa za kulevya zenye Kg. 6.

Wakili:Unamfahamu mtu mmoja anaitwa Christopher Shekiondo?

SSP Ulaya: Namfahamu, huyo ni Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, ambaye yeye alitoa hati yake inayoonyesha dawa hizo zina uzito wa Kg.4.8 na zina thamani ya sh. milioni 120 na hati inaonyesha ilitolewa na Kamishna huyo Julai 6, 2010.

Wakili:Utakubaliana na mimi kuwa, Kamishna Shekiondo aliyapima madawa hayo na kutoa uzito na thamani ya dawa hizo wakati dawa hizo hazijaletwa bado nchini?

SSP Ulaya: Ndiyo.

Wakili: Huoni kitendo hicho cha Shekiondo kupima dawa hizo wakati dawa hizo bado haziletwa hapa nchini, ndiyo kumemsababisha mshtakiwa afunguliwe kesi hii na hadi sasa anaendelea kusota gerezani?

SSP Ulaya:Kimya.

Wakili:Hivi hizo kilo 6 za dawa hizo ambazo jeshi la polisi la Tanzania lililetewa kwa maandishi na serikali ya Mauritius zinafanana na kilo 4.8 zilizotajwa katika hati ya Shekiondo?

SSP Ulaya:Ni tofauti.

Wakili: Inakuwaje hati ya mashtaka inasomeka mshtakiwa alisafirisha Kg.4.8 kwenda Mauritius na taarifa za kipelelezi za Mauritius walizolitumia jeshi letu la polisi, zinaonyesha waliukamata msafara ule ukiwa na kg. 6 za dawa za kulevya, sasa ieleze mahakama usahihi ni upi?

SSP Ulaya:Kimya.

Wakili: Kwa hiyo utakubaliana na mimi tuhuma kuhusu usafirishaji wa dawa hizo zilikuwa zinamhusu Mika na siyo Mintanga?

SSP Ulaya:Ni kweli, kwani tulipata taarifa hizo toka Mauritius na ndiyo maana tukawa tunamtafuta sana Mika, kwani Petro Mtagwa, Elia Nathaniel, Ally Msengwa na Emilian Patrick ndiyo waliokamatwa na dawa hizo wakiwa wamemeza tumboni na mimi nilipowafuata katika gereza moja nchini humo na kuwahoji, walinieleza kuwa aliyewapatia dawa hizo ni mtu mmoja anaitwa Mika na aliwamezesha dawa hizo katika hoteli moja iliyopo Manzese na aliwapatia dola 100 za kimarekani kwa kila mmoja na Agosti 10 mwaka 2008, walianza safari kuelekea Maurtius wakiwa wamememeza tumboni dawa hizo.

Yafuatayo ni mahojiano baina ya wazee wa baraza na SSP Ulaya:

Swali:Kuna ushahidi gani katika upekuzi unahusiana na makosa yanayomkabili mshtakiwa?
SSP Ulaya: Hakuna.

Swali:Ulisema ulivyofika Mauritius wale Watanzania waliokamatwa walikuambia ni Mika ndiyo aliyekuwa amewapatia zile dawa za kulevya, sasa kwanini Jamhuri inamfungulia kesi hii Mintanga peke yake?
SSP Ulaya:Kimya.

Swali:Una uhakika gani kama mshtakiwa hausiki katika kesi hii?
SSP Ulaya: Naamini ushahidi niliyotoa na upelelezi niliyofanya, mshtakiwa anahusika katika kesi hii kwenye kosa moja tu la kula njama.

Swali:Kwani wale Watanzania waliokamatwa kule Mauritius ulivyowahoji, walikueleza kuwa Mintanga ana husika kusafirisha dawa zile za kulevya walizokutwa nazo?
SSP Ulaya:Walinieleza kuwa Mintanga hausiki kabisa na dawa hizo.

Jaji Dk.Fauz Twaib aliarisha kesi hiyo hadi leo, ambako shahidi wa tano anatarajiwa kupanda kizimbani kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Novemba 18 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.