Header Ads

VIELELEZO VYAKWAMISHA KESI YA MINTANGA

Na Happiness Katabazi


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ililazimika kusitisha kuendelea ushahidi wa shahidi wa tatu na wanne katika kesi ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 4.8 inayomkabili Rais wa zamani wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (TFB) Alhaji Shabani Mintanga baada mahakama hiyo kuvikuta vielelezo vitatu vya upande wa Jamhuri kuwa vina mapungufu.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Dk.Fauz Twaib kufuatia shahidi wa tatu Godfrey Mroso ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Anvelope Travel Agency kutoa sehemu ya ushahidi wake ambapo alidai kuwa yeye ndiye alitengeneza tiketi tatu ambazo aliomba zipokelewe na mahakama kama vielelezo ombi ambalo lilipingwa vikali na mawakili wa utetezi Jerome Msemwa na Yassin Memba kwa madai kuwa tiketi hizo ni nakala badala risiti halisi.

Wakili Msemwa aliomba mahakama isipokee tiketi hizo vivuli kama vielelezo kwasababu tayari upande wa Jamhuri upo kwenye nafasi nzuri ya kuleta tiketi halisi na kompyuta iliyotumiwa na kampuni kutengeneza tiketi hizo ambapo hata hivyo Jaji Dk.Twaibu alikubaliana na pingamizi la wakili Msemwa na akautaka upande wa Jamhuri uende kuondoa neno linalosomeka kuwa tiketi hizo si nakala halisi na akaamuru shahidi huyo aruhisiwe kwenda nyumbani na pindi marekebisho hayo yatakaponywa upande wa Jamhuri umulete tena shahidi huyo ili aweze kuja kumalizia kutoa ushahidi wake na kutaka shahidi wa nne apande kizimbani aanze kutoa ushahidi wake.

Wakati Jaji Dk.Twaibu huyo akitolea uamuzi kuhusu vielelezo hivyo vilivyokuwa vikitaka kutolewa na shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri,Wakili Mwandamizi wa serikali Prudence Rweyongeza alimleta shahidi wa nne, ambaye ni Mrakibu Mwandamizi wa Polisi(SSP), Charles Ulaya ili atoe ushahidi wake lakini hata hivyo wakili huyo alieleza mahakama kuwa kutokana na uamuzi wa mahakama ulitolewa wakati shahidi wa tatu anataka kutoa vile vielelezo vitatu.

Shahidi huyo wan ne (SSP) Ulaya , vielelezo vyake anavyokusudia kuvitoa wakati akitoa ushahidi wake ni kama vya shahidi wa tatu ambavyo vimetengenezwa kwa teknolojia ya kielekroniki na nikala siyo halisi hivyo wakaiomba mahakama shahidi huyo asitoe ushahidi ili upande wa jamhuri uende kuvifanyia marekebisho vielelezo vyote hivyo kwenye kompyuta na leo wataviwasilisha mahakamani na mashahidi hao wataendelea kutoa ushahidi wao.

Aidha Jaji Dk.Twaibu alikubaliana na ombi hilo la wakili wa serikali Rweyongeza la kuarisha kesi hiyo hadi leo na akaamuru vielelezo hivyo ambavyo hata hivyo bado havikuwa vimepokelewa na mahakama hivyo haikuweza kujulikana mara moja ndani ya vielelezo hivyo vimeandikwa nini, hadi leo asubuhi.

Mwaka 2008, Mwintanga alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi hiyo ambayo haina dhamana ambapo kisheria Mahakama ya Hakimu Mkazi haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, kesi hiyo iliamishiwa mahakama Kuu mwaka jana na juzi ikaanza kusikilizwa rasmi ambapo imepangwa kusikilizwa mfululizo hadi Novemba 25mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 16 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.