Header Ads

WANACHUO UDSM 50 KORTINI KWA MAANDAMANO HARAMU

Na Happiness Katabazi

JUMLA ya Wanafunzi 50 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, wakikabiliwa na makosa mawili ya kufanya mkusanyiko usihalali na kukaidi amri ya Jeshi la Polisi liliwataka watawanyike.


Mawakili wa Serikali Ledslaus Komanya na Shadrack Kimaro walidai mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema waliwataja washtakiwa hao kuwa ni Mwambapa Elias,Evalist Elias, Baraka Monesi, Hellen Mushi, Alphonce Lusako, Matrona Babu, Rolana Wilfred, Godfrey Deogratius , Munisi Denis,Evanos Gumbi na wenzao 40.

Wakili wa Serikali Komanya alidai kuwa mnamo Novemba 11 mwaka huu,katika eneo la Mlimani la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walifanya mkusanyiko usio wa halali na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo hilo.

Wakili Komanya alidai kosa la pili ni kwamba washtakiwa hao wakiwa kwenye mkusanyiko huo haramu kwa lengo la kufanya mgomo, askari wa Jeshi la Polisi waliwataka wanafunzi hao watawanyike lakini hata hivyo wanafunzi hao walikahidi amri hiyo na kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Hata hivyo washtakiwa hao ambao walifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi, walikana mashtaka hayo na Hakimu Lema alisema ili mshtakiwa apate dhamana ni lazima kila mshtakiwa awe na mdhamini mmoja wa kuaminika ambaye atasaini bondi ya Sh milioni moja.

Hata hivyo ni washtakiwa tisa tu kati ya 50 ndiyo waliotimiza masharti na kupata dhamana na wengine waliosalia walijikuta wakipelekwa gerezani kwa kushindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana.

Washtakiwa hao waliopata dhamana ni Rehema Mnuo, Grory Masawe, Happy Amulike, Elisia Mpangala, Frida Timoth , Stela Msofe, Betwel Martin, Mmasi Stephano na Lugemalila Venance.

Hakimu Lema aliarisha kesi hiyo Novemba 28 mwaka huu, ambapo siku hiyo itakuja kwaajili ya upande wa jamhuri kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.

Novemba 11 mwaka huu, Jeshi la polisi liliwatanya baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho ambao walianzisha mgomo kwa kile walichodai ni kuishinikiza bodo ya Mikopo iwapatie mikopo wanafunzi wenzao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Novemba 15 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.