Header Ads

WASHTAKIWA KESI YA 'SAMAKI WA MAGUFULI'WAMALIZA KUJITETEA

Na Happiness Katabazi


HATIMAYE washtakiwa watano raia wa China wanaokabiliwa na kesi ya uvuvi haramu katika ukanda wa Tanzania kwa kutumia meli ya Tawariq 1 maarufu kama ‘Kesi ya Samaki wa Magufuli’ wamemaliza kujitetea katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Washtakiwa hao Hsu Chin Tai, Zhao Hanguing, Hsu Shang Pao, Ca’ Dong Li na Chen Rui Hai wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Ibrahim Bendera na John
Mbele mbele ya Jaji Agustine Mwarija.

Novemba 14, mwaka huu, washtakiwa hao walijitetea kwa lugha ya Kichina na kusaidiwa na mkalimani Mtanzania; walisema: “Mheshimiwa Jaji wateja wetu hao watano wamemaliza kujitetea na tumeona utetezi wao unatosha hivyo hatuhitaji kuleta mashahidi ili waje kuwatetea na kwa hiyo upande wa utetezi katika kesi hii tumefunga ushahidi wetu na tunaiachia mahakama iendelee na taratibu zingine za kisheria,” alisema Wakili Bendera.

Kwa upande wake Jaji Mwarija alikubaliana na ombi hilo na akaahirisha kesi hiyo hadi Novemba 29 ambapo siku hiyo pande zote katika kesi hiyo, ule wa jamhuri unaowakilishwa na wakili mwandamizi wa serikali Biswalo Mganga na wa utetezi unaowakilishwa na mawakili tajwa hapo juu, zinatakiwa kufika mahakamani hapo na kuwasilisha majumuisho yao kwa njia ya mdomo.

Machi 2009 washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kisha kesi hiyo ikahamishiwa Mahakama Kuu wakikabiliwa na makosa ya kuvua samaki bila leseni, kuharibu mazingira katika kina kirefu cha ukanda wa Bahari ya Hindi eneo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Novemba 22 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.