Header Ads

HAKIMU AZUIA WAANDISHI KURIPOTI KESI YA WANAFUNZI WA UDSM

Na Happiness Katabazi



HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Waliarwande Lema kwa mara ya pili jana aliendelea tabia yake kwa kuwazuia waandishi wa habari toka vyombo mbalimbali vya wasiingie kusikiliza kesi ya kufanya mkusanyiko usio halali inayowakabili wanafunzi 50 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Kesi hiyo ambayo jana ilikuja kwaajili wanafunzi 41 kati ya 50 kuja kupatiwa dhamana na hakimu huyo, ambapo waandishi hao wa habari walifika mahakamani hapo tangu saa mbili asubuhi na kuhudhuria kesi mbalimbali lakini ilipofika saa 6.30 mchana wanafunzi hao waliingizwa kwenye ofisi ya hakimu Lema kwaajili ya kuanza kutimiza masharti ya dhamana.

Wakati wanafunzi hao wakiongozwa na askari wa Jeshi la Magereza na Polisi kuingia ndani ya chumba hivyo, pia askari polisi walikuwa wakiwasaidia waandishi wa habari ili waweze kuingia ndani ya chumba hicho ili waweze kusikiliza kesi hiyo lakini ghafla hakimu Lema alipoona sura za waandishi wa habari akatoa sauti ya ukali na ya juu ya kuwafukuza waandishi wa habari wa habari watoke ndani ya chumba hicho bila kutoa sababu zozote.

“Nimesema nyie waandishi wa habari tokeni haraka ndani ya ofisi yangu, na hii ni amri nataka mtoke upesi ili nianze kuendesha kesi hii ya wanafunzi wa Chuo Kikuu”alifoka Hakimu Lema kwa sauti ya juu na kuwafanya waandishi wa habari akiwemo mwandishi wa habari hii kuondoka ndani ya chumba hicho bila kujua kesi hiyo iliendeleaje.

Hata hivyo waandishi hao wa habari za mahakama walionyesha kukerwa na tabia hiyo ya Hakimu Lema ya kuwazuia kuripoti kesi hiyo kwa mara ya pili sasa hali iliyowazimu kwenda kwa kushtaki kwa Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Elvin Mugeta ambaye aliwaomba waandishi wa habari kuwa wapole na akaidi hilo swala kulifuatili ili kujua ni sababu gani iliyosababisha hakimu huyo kufia uamuzi huo wa kuwakataza waandishi wasiingie kusikiliza kesi hiyo.

Mara ya kwanza hakimu huyo kuwatimua waandishi wa habari kuripoti kesi hiyo ni Novemba 14 mwaka huu,wanafunzi hao 50 walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza mbele ya hakimu huyo na kusomewa mashtaka mawili kwamba Novemba 11 mwaka huu,katika eneo la Mlimani la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walifanya mkusanyiko usio wa halali na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo hilo.

Wakili Komanya alidai kosa la pili ni kwamba washtakiwa hao wakiwa kwenye mkusanyiko huo haramu kwa lengo la kufanya mgomo, askari wa Jeshi la Polisi waliwataka wanafunzi hao watawanyike lakini hata hivyo wanafunzi hao walikahidi amri hiyo na kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 17 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.