Header Ads

LEMA USITUNYIME UHURU WANAHABARI




Na Happiness Katabazi

INASHANGAZA kuona uandishi wa habari za mahakamani licha ya kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu kesi za wananchi na viongozi, mchango wake bado haujatambuliwa.

Nadiriki kusema hivyo kutokana na kitendo kilichofanywa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Waliarwande Lema, Novemba 14 na 16 mwaka huu.

Nasema jamii na serikali haina budi kuthamini mchango wetu waandishi wa habari za mahakamani kwani tukiamua kuziripoti kesi hizo mara moja tu wakati zinafunguliwa mahakamani na kisha tukaacha kuripoti mwendelezo wake, matokeo yake si serikali, wakuu wa vyombo vya habari wala jamii watakao kuwa wakifahamu kesi hizo zimefikia hatua gani.

Lakini kwa uzalendo wetu na kwa kupenda kuripoti habari za mahakamani tumekuwa tukiziripoti kesi hizo mwanzo - mwisho na tunauhakikishia umma wa Watanzania kuwa tutaendelea kuziripoti kesi hizo bila kuchoka.

Novemba 14 mwaka huu, wanafunzi 50 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), walifikishwa mahakamani hapo wakidaiwa kutenda makosa mawili ya kufanya mkusanyiko haramu Novemba 11, na kosa la pili ni kukaidi amri ya Jeshi la Polisi lililowataka wanafunzi hao kutawanyika.

Siku zote hizo mbili kesi hiyo ilipokuja kwa mara ya kwanza kwa ajili ya washitakiwa kusomewa mashitaka, waandishi wa habari tuliingia ndani ya chumba cha mahakama kwa ajili ya kuanza kusikiliza kesi hiyo lakini ghafla Hakimu Lema aliwatimua waandishi ambao tulitii amri yake tukatoka nje na kesi ilipokwisha tulitumia mbinu zetu za kujua kilichoeendelea ndani ya chumba hicho.

Kesho yake tukaenda kuiripoti kesi hiyo kwenye vyombo vya habari bila kukosea.

Aidha, Novemba 16 katika hali isiyotarajiwa Hakimu Lema aliendeleza kasumba yake ya kutufukuza waandishi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya wanachuo hao 41 kuja kupata masharti ya dhamana.

Kweli tuliitii amri yake na kutoka nje na kwakuwa tuliona hakimu huyo hakututendea haki kwakuwa kesi hiyo ilikuwa ikiwahusu watu waliozidi miaka 18, si kesi ya kulawiti wala kubakwa, tuliamua kwenda kumripoti kwa mkuu wake wa kazi, Hakimu Elvin Mugeta, ambaye alitupokea na kututaka tuwe na subira na kwamba atakwenda kuzungumza na Hakimu Lema kujua ni kwanini alifikia uamuzi huo wa kutufukuza.

Na wakati Lema akitufukuza tusiingie kwenye chumba alichokuwa akiendeshea kesi, wanausalama mbalimbali wanaoshinda mahakamani hapo walikuwa wakijitahidi kadiri ya uwezo wao kuwasaidia waandishi wa habari kuingia ndani ya chumba hicho ili waweze kusikiliza kesi hiyo bila mafanikio.

Si siri, kitendo alichotufanyia Hakimu Lema si tu kinanyima haki ya waandishi wa habari kupata habari, pia kilitudhalilisha waandishi wa habari tuliokuwa tumefika hapo kwa ajili ya kuripoti habari hiyo na nyingine.

Pia kitendo hicho kimeibua maswali mengi yasiyo na majibu kuwa hakimu huyo ana nini anachotaka kukificha katika kesi hiyo?

Au Hakimu Lema alidhani sisi ni wafuasi wa kikundi cha wanamgambo wa Kisomali cha Al - Shabaab tuliobeba mabomu kwenye pochi zetu kwenda kumlipua?

Tumuulize Hakimu Lema ana masilahi gani binafsi katika kesi hiyo hadi atuzuie kuripoti kesi hiyo?

Kwa upande wa pili wa shilingi, binafsi namuona Hakimu Lema ni miongoni mwa mahakimu wanawake wachache wenye uzoefu wa kazi hiyo na wanaojiamini katika kutoa maamuzi yao ukilinganisha na baadhi ya mahakimu wengine wanawake ambao si jasiri.

Na katika hili nampongeza Hakimu Lema, kwani kupitia kesi mbalimbali anazoziendesha ambazo mimi nimekuwa nikihudhuria, nimeweza kulibaini hilo.

Hivyo basi, ni rai yangu kwa Hakimu Lema atambue kuwa tunaheshimu uhuru wa mahakama na utawala wa sheria na tunakuza utawala wa sheria kupitia uandishi wetu wa habari hizo za mahakamani na tunafahamu vema miiko na mipaka ya taaluma yetu.

Tunamwakikishia Hakimu Lema kuwa tutaendelea kuiripoti kesi hiyo ya wanafunzi wa UDSM na nyingine kwa njia tunazozijua sisi, hata kama atatuzia kuripoti kesi hiyo.

Mungu ibariki Tanzania,
Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Novemba 22 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.