Header Ads

KESI YA WANAFUNZI UDSM YAPIGWA KALENDA

Na Happiness Katabazi


UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya maandamano na kufanya mkusanyiko haramu inayowakabili wanafunzi 50 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jana ulishindwa kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao kwasababu ya mshtakiwa mmoja kuongezwa katika kesi hiyo na mshtakiwa mmoja kushindwa kufika mahakamani hapo.



Wakili wa Serikali Ladiuslaus Komanya mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema,alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwaajili ya kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa lakini haitawezekana kwasababu wanamuongeza mshtakiwa mmoja Fred Hatari na hivyo kufanya idadi ya washtakiwa kufikia 51 hivi sasa.

Wakili Komanya alidai sababu ya pili ni mshtakiwa mmoja Said John ameshindwa kufika mahakamani hapo na kulazimika kuomba mahakama itoe hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa huyo na mdhamini wake aitwe mahakamani, maombi ambayo yalikubaliwa na hakimu Lema
Hata hivyo mshtakiwa aliyeongezwa, Hatari alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na amepelekwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Hakimu Lema aliarisha kesi hiyo hadi Desemba 20 mwaka huu itakapokuja kwaajili ya kutajwa na kwamba upande wa Jamhuri uje kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali Januari 10 mwakani.

Novemba 14 mwaka huu, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na wakili wa serikali Komanya alidai kuwa katika eneo la Mlimani la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walifanya mkusanyiko usio wa halali na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo hilo.

Na kwamba shtaka la pili ni kwamba washtakiwa hao wakiwa kwenye mkusanyiko huo haramu kwa lengo la kufanya mgomo, askari wa Jeshi la Polisi waliwataka wanafunzi hao watawanyike lakini hata hivyo wanafunzi hao walikahidi amri hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Novemba 29 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.