Header Ads

MARANDA AFUNGULIWA KESI MPYA YA EPA



Na Happiness Katabazi


KADA wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Rajabu Maranda jana alifikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na kesi mpya ya kugushi na kujipatia ingizo la jumla ya Sh bilioni 5.9 toka Benki Kuu ya Tanzania, mali ya benki hiyo kinyume cha sheria.


Maranda na mpwa wake Farijala Hussein ambao kwa sasa wanatumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kutiwa hatiani na mahakama hiyo Mei mwaka huu, kwa makosa ya kughushi na kujipatia ingizo la shilingi bilioni 1.8 toka katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), na hadi sasa anakabiliwa na kesi tano za aina hiyo katika mahakama hiyo ambazo bado hazijatolewa hukumu.

Wakili Mwandamizi wa serikali Fredrick Manyanda mbele ya Hakimu Mkazi Alocye Katemana, alidai kesi hiyo kwa sasa itakuwa na jumla ya washtakiwa watano ambapo washtakiwa wapya ni Maranda,aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Idara ya Madeni ya Nje(EPA), Ester Komu na Kaimu Katibu BoT, Bosco Kimela na wafanyabiashara Ajay Somani na Jai Somani.

Wakili Maranda alidai Maranda anakabiliwa na makosa matano ya kula njama, kugushi, kuwasilisha hati ya kuamisha deni iliyogushiwa, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kujipatia ingizo la kiasi hicho cha fedha toka Benki Kuu.

Alidai kuwa Desemba 15 mwaka 2004 alighushi hati ya kuamisha mali kati ya Philip Sceman of Societe Alsociene de Construction De Machines Textile 146-148,Ruedaboukir 75002 ya Paris Ufaransa na Maulid Kaasa wa kampuni ya Liquidity Services Ltd kuonyesha kwamba mauled wa kampuni ya Liquidity Services Ltd amepewa idhini ya kudai deni la shilinigi bilioni 5.9 mali ya kampuni ya M/S Societie Alsacienne De Cpnstruction De Machines Textile ya Ufaransa.

Kwa upande wa Komu na Kimela alidai wanashtakiwa kwa kosa moja la kuisababishia BoT hasara ya kiasi hicho cha fedha kwani wao walikuwa watumishi wa benki hiyo na wakashindwa kutimiza majukumu yao hivyo kuisababishia benki hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo washtakiwa wote walikana mashtaka hayo na Maranda akadai juzi jioni alipigiwa simu akiwa katika gereza la Ukonga anakoishi kwa sasa akitakiwa jana afike mahakamani hapo bila kujua afike kwaajili ya jini na kwamba hata wakili wake hana taarifa kama amefunguliwa kesi hiyo mpya ila anaiomba mahakama hiyo impatie dhamana kwa mashtari yatakayowekwa na mahakama hiyo.

Hakimu Katemana alisema Komu na Kimela wanakabiliwa na kosa la kusababisha hasara hivyo ili wapate dhamana ni lazima kila mmoja wao awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya bilioni 1.5.

Wakati Maranda anayekabiliwa na makosa ya kula njama, kugushi na kujipatia ingizo atapaswa awe na wadhamini wawili ambao watatoa fedha taslimu au kuwasilisha hati yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.6.Hata hivyo Maranda ameshindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana na kesi hiyo imearishwa Desemba mosi mwaka huu na watasomewa maelezo ya awali watasomewa Januari 16-20 mwaka 2012.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 17 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.