Header Ads

HUKUMU KESI YA JERRY MURRO NOVEMBA 30

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imesema Novemba 30 mwaka huu, itatoa hukumu dhidi ya aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa(TBC1), Jerry Murro na wenzake ambao wanakabiliwa na kesi ya kula njama na kuomba rushwa ya Sh milioni 10.


Hayo yalisemwa jana na Hakimu MKazi Frank Mosha jana wakati kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya hukumu.

‘Oktoba 4 nilitoa amri ya kuzitaka pande mbili katika kesi hii zilete majumuisho yao ya kuwaona washtakiwa ama wana hatia au hawana hatia ambapo upande wa utetezi uliwasilisha majumuisho yao Oktoba 21 mwaka huu na upande wa Jamhuri uliwasilisha majumuisho yao ambayo yaliomba mahakama hii iwaone washtakiwa wanahatia Oktoba 28 mwaka huu:

‘Kwa kuwa amri hiyo imetekelezwa kikamilifu na mawakili wa pande zote mbili kwa mujibu wa sheria, hatua inayofuata ni ya mahakama hii kupanga tarehe ya kutoa hukumu katika kesi hii na hivyo basi leo hii mahakama hii inatamka kuwa itatoa hukumu dhidi ya Murro na wenzake Novemba 30 mwaka huu’ alisema Hakimu Mosha.

Februali 5 mwaka 2010, Murro na washtakiwa wenzake Edmund Kapama na Deogratius Mugasa walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo wakikabiliwa na makosa kula njama, kuomba rushwa na kujifanya wao ni watumishi wa serikali.Murro anayetetewa na wakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza anakabiliwa na makosa mawili ya kula njama na kuomba rushwa, wakati Mugasa na Kapama wanakabiliwa na mashtaka yote matatu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Novemba Mosi mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.