Header Ads

MNYIKA AKANUSHA MADAI YA NG'UMBI



Na Happiness Katabazi

MBUNGE wa Jimbo la Ubunge kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), John Mnyika ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, itupilie mbali hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya (CCM), Hawa Ng’umbi kwa madai kuwa tuhuma zilizoelekezwa kwake na Ng’umbi ni za uzushi na hazina ushahidi.


Katika kesi hiyo ya madai ya Na.107/2010 ,iliyopo mbele ya Jaji Upendo Msuya , Ng’umbi anayetetewa na wakili wa kujitegemea Issa Maige,anamshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Ubungo na Mnyika, ambapo anadai Sheria ya Uchaguzi ilikiukwa katika uchaguzi huo na kwamba mwanasheria mkuu wa serikali na msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo walishindwa kutimiza majukumu yao ya kuakikisha sheria za uchaguzi katika uchaguzi huo zisivunjwe na Myika na mawakala wake.

Majibu hayo ya Mnyika dhidi ya hati hiyo ya hati hiyo ya madai iliyofanyiwa marekebisho yanatoka na amri iliyotolewa na Jaji Msuya Septemba 27 mwaka huu, ambapo Jaji huyo alimwamuru Ng’umbi kuiondoa hati hiyo ya madai na kwenda kuifanyia marekebisho na kisha airejeshe mahakamani hapo , amri ambayo ilitekelezwa na mlalamikaji huyo ambaye Oktoba 11 mwaka huu, aliwasilisha mahakamani hapo hati hiyo mpya ambayo aliifanyia marekebisho.

Mnyika anayetetewa na wakili Edson Mbogoro anadi kuwa madai kuwa yeye na mawakala wake waliitumia kompyuta zao kuhesabia kura bila idhini ya wagombea wenzake na Tume ya Uchaguzi , hayana msingi kwani hajaona sheria yoyote hapa nchini inayokataza mgombea kuingiza kompyuta ndani ya chumba cha kuhesabia kura.

Mnyika anadai tuhuma kuwa Septemba 11 mwaka 2010 wakati akihutubia kwenye mkutano wake wa kampeni eneo la Riverside kuwa alitoa maneno ya kashfa dhidi ya Ng’umbi alipokuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wilaya ya Kinondoni(UWT),alijihusisha na ufisadi wa kuuza nyumba za jumuiya kinyume cha sheria, kuwa tuhuma hiyo haina ukweli wowote na kuongeza kuwa hata kama aliitoa tuhuma hiyo kwenye mikutano yake ya kampeni, mlalamikaji ameshindwa kuonyesha ni jinsi gani matamshi hayo yameweza kuathiri matokeo yake ya uchaguzi wa ubunge.

Kuhusu tuhuma kuwa kuna baadhi ya vituo fomu za matokeo hazikuwasilishwa kwa NEC, Mnyika pia anapinga tuhuma hiyo na kuongeza kuwa mlalamikaji ameishoa kutoa tuhuma hiyo bila kuonyesha vielelezo.

“Naiomba mahakama hii itupulie mbali tena kwa gharama hati hiyo ya madai iliyofanyiwa marekebisho kwasababu madai anayotuhumiwa nayo ni ya uzushi na yasiyo na ushahidi”alidai Mnyika anayetetewa na wakili Edson Mbogoro.

Oktoba 11 mwaka huu, Ng’umbi aliwasilisha hati iliyofanyiwa marekebisho na kuiomba mahakama hii itamke kufanyike uchaguzi huru na wa haki kwasababu uchaguzi mkuu wa jimbo hilo uliofanyika mwaka jana aukuwa huru na wa haki kwani sheria za uchaguzi zilivunjwa na Mnyika katika mikutano yake kampeni alimtolea maneno ya kumkashfu kwa kumuita fisadi aliyeza nyumba za CWT tuhuma anayodai ilisababisha wanawake wengi wa jimbo hilo kutompigia kura kwaajili ya kuchafuliwa kwa kashfa hiyo na mdaiwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 2 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.