Header Ads

SHAHIDI:SIMU YA MINTANGA ILITUMIKA



Na Happiness Katabazi


HATIMAYE Mahakama Kuu Dar es Salaam jana ilizipokea tiketi tatu za ndege kama vielelezo vya upande wa Jamhuri katika kesi hiyo ambazo tiketi hizo zilitumiwa na msafara wa Timu ya Taifa ya Ngumi, ambao ulitiwa mbaroni nchini Mauritius kwa tuhuma za kuingiza dawa za kulevya zenye uzito wa Kg.4.8 nchini humo.


Jaji Dk.Fauz Twaib alisema anazipokea tiketi hizo kama vilelezo kwasababu vimekidhi matakwa ya kisheria na uamuzi alioutoa juzi ambao ulikataa kuzipokea tiketi hizo kama vielelezo hadi upande wa jamhuri utakapokwenda kuzifanyia marekebisho tiketi hizo ambazo zilikuwa ni nakala na kisha jana wazirejeshe mahakamani hapo, amari ambayo ilitekelezwa na mawakili wa upande wa Jamhuri.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani hap na hivyo vielelezo vilivyopokelewa jana na Jaji Dk.Twaibu, kunaonyesha kuwa aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania Alhaji Shabani Mintanga ambaye ndiye mshtakiwa pekee katika kesi hiyo kuwa ndiye aliyehusika kuwatafutaia tiketi watu waliokutwa na dawa hizo huko Mauritius ambao hata hivyo hawajashtakiwa katika Mahakama za Tanzania.

Tiketi hizo tatu zilitolewa jana na shahidi wa tatu, Godrey Mroso ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Anvelope Travel Agency, ambaye alidai yeye ndiye aliyekatisha tiketi hizo mwaka 2008 ambapo tiketi hizo zilikuwa ni za Nathaniel, Msengwa na Mutagwa.

Nathaniel na Msengwa waliambatana na timu hiyo nchini Mauritius kwa madai kuwa ni mashahabiki ambao kwa mujibu wa ushahidi walitambulishwa kwa kocha wa timu hiyo Nassoro Michael Irenge na Mintanga.


Akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Ntuli Mwakahesya, Mroso aliitaja namba ya simu ya kiganjani aliyokuwa akipigiwa na mtu aliyekwenda ofisini kwao kufanya maandalizi na kulipia tiketi hizo nne kwa ajili ya safari hiyo kuwa ni 0754 284887.

Hata hivyo wazee wa baraza Wazee wa Baraza, Zeshta Lyimo na Msakala Tambaza walipomuuliza shahidi huyo swali kuwa mtu ambaye alikwenda kukata tiketi hizo kama alijitambulisha jina, shahidi huyo alijibu kuwa mtu huyo hakujitambulisha jina na hawezi kumtambua kwa sura.

Lakini kwa mujibu wa ushahidi uliokwisha tolewa na shahidi wa kwanza katika kesi hiyo ambaye alikuwa ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Ngumi la Taifa, Christopher Mtabarukwa,mapema Jumatatu wiki alieleza mahakama hiyo kuwa mwenye namba hiyo ya hi namba hiyo 0754 284887 ni mshtakiwa Mintanga.

Mutaburukwa alidai kuwa alikuwa akiwasiliana na rais wake (Mintanga) kwa kutumia simu hiyo kuhusu maendeleo ya kambi ya timu hiyo wakati ikiwa kambini.
Irenge na bondia Patrick Emilian pia walikuwa wameshikiliwa nchini Mauritius kwa tuhuma hizo lakini wao wameshaachiwa baada ya kuonekana kuwa hawahusiki na uingizaji wa dawa hizo nchino humo, lakini Bondia Mutagwa, Nathaniel na Msengwa bado wanashikiliwa nchini humo.

Akitoa ushahidi wake juzi shahidi wa pili upande wa mashtaka kocha wa zamani wa timu hiyo ya ngumi Nassoro Michael Irenge alidai kuwa dawa hizo za kulevya anazoshtakiwa nazo Mintanga zilikutwa kwenye begi la Bondia Petro Mutagwa.

Irenge aliieleza mahakama kuwa katika msafara wa timu hiyo ulikuwa na mabondia wawili Patrick na Mutagwa na yeye kocha na kwamba ndio wlaioagwa.

Hata hivyo alidai kuwa baada ya kuagwa aliambiwa na Mintanga kuwa kuna watu wengine ambao ndio waliomdhamni bondia Mutagwa tiketi ya kusafiri, pia watakuwa nao katika msafara huo.

Alidai kuwa walipofika uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere, alikutana na watu wengine aliowataja kwa majina ya Nathaniel na Msengwa ambao walijitambulisha kuwa ni mashahabiki.

Alidai kuwa wakiwa katika hoteli waliyofikia Mauritius, siku ya pili akiwa chumbani kwake na mabondia wake waliingia askari wa Mauritius wakiwa na wale mashahabiki pamoja na begi lilioandikwa Tanzania likiwa na jina la Petro Mutagwa.
Alidai askari wale waliwaweka chini ya ulinzi kwa tuhuma za kukutwa na dawa zaa kulevya ambazo walizitoa kwenye begi lile na kuzimwaga chini.

Irenge aliendelea kudai kuwa Mutagwa alikubali kuwa begi lile ni lake na kwamba liliazimwa na mmoja wa wale mashahabiki kuwa kuna vitu alikuwa anakwenda kuvinunua.Kesi hiyo inaendelea tena leo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 17 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.