WATANZANIA TUACHE UNAFIKI
Na Happiness Katabazi
WIKI iliyopita Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon alihutubia mkutano wa marais wa nchi za Jumuiya ya Madola uliofanyika nchini Austalia. Tanzania tuliwakilishwa na rais wetu Jakaya Kikwete na msafara wake.
Imeripotiwa kuwa katika mkutano huo Waziri Mkuu wa Uingereza, Cameroon aliwahutubia viongozi hao mambo mengi likiwemo agizo la kuzitaka nchi za Afrika kwenda kutunga sheria itakayoruhusu ndoa za jinsi moja la sivyo nchi yake itazinyima misaada nchi za Afrika.
Tangu kuripotiwa na vyombo vya habari agizo hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe amejitokeza hadharani kutoa tamko kwa niaba ya serikali kuhusu agizo hilo ambapo alisema msimamo wa serikali yetu, ni kwamba haitakaa itekeleze agizo hilo kwasababu siyo utamaduni wetu na kwamba heri watanzania wafe masikini kuliko kutunga sheria hiyo.
Wananchi kupitia njia mbalimbali za mawasiliano wanaendelea kutoa maoni yao kuhusu agizo hilo ambapo wananchi wengine wanataka sheria hiyo itungwe huku wengine wakitaka isitungwe.
Ieleweke wazi kuwa hadi sasa sheria na Katiba ya Tanzania haitambui ndoa za jinsia moja.
Licha ya vitendo vya ushoga, usagaji na vya baadhi ya wanawake kupenda kufanyiwa matendo ya ngono kinyume na maumbile kwa hiari yao au wengine siyo kwa hiari yao vinazidi kushika kasi kila kukicha na baadhi viongozi wa serikali, wananchi wakiwemo wazazi na viongozi wa dini wanafahamu fika hilo ila kwa unafiki wetu tulifumbia macho ubazazi huu kwa kukataa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola wale wote wanaofanya ufilauni huo.
Lakini leo hii Camerron ametoa agizo hilo mbele ya marais wetu, ndiyo serikali yetu,wananchi,viongozi wa dini nao wanaibuka nakutoa matamko ya kupinga utekelezwaji wa agizo hilo.
Nakubaliana na matakwa ya Ibara 18(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inampa uhuru kila mwananchi kutoa maoni na kutoa fikra zake;
Lakini huu ni unafki wa kujitokeza kupinga agizo hilo wakati tayari kuna baadhi ya Watanzania wenzetu wameishakubuhu na wamegeuza vitendo hivyo ndiyo ajira yao inayowapatoa riziki.Na inaelezwa hata baadhi ya wanaume waliofunga ndoa uamua kuwasaliti wake zao na kuamua kuwatafuta mashoga kwa siri ili wawapatie huduma hiyo ya ngono kinyume cha maumbile.
Leo hii hapa Dar es Salaam, zile sherehe maalum za kumfunda bibi harusi mtarajiwa(Kitchen Party), kwenye kumbi hasa zinazopiga muziki wa Taarabu hata dansi ni kawaida kabisa kuwakuta mashoga wakiwa wametamalaki na ‘kutamba,kujishebedua’ bila wasiwasi.
Kitchen Party nyingi siku hizi mashoga hukodishwa kwaajili ya kuja kusasambua sanduku analotuzwa bibi harusi mtarajiwa, kucheza muziki wa mwambao na mashoga hao ama kwa hakika uchangamsha sherehe hizo. Na wakati mashoga hao wakifanya vitendo hivyo wazazi wa bibi harusi mtarajiwa na ndugu wa mwanaume ambao mtoto wao wa kiume siku chache zijazo anatarajia kumuoa bibi harusi huyo, wanakuwepo ukumbini na kushuhudia hali hiyo na wala hawakemei au kususia sherehe hizo na ndiyo huwa wa kwanza kuwatunza fedha mashoga hao.
Baadhi Maustaadhi wa dini ya Kiislamu nao wamekuwa wakilalamikiwa kichini chini na wengine kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kuwalawiti watoto wa kiume ambao ufika ‘Chuoni’ kufundishwa mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Nao baadhi ya viongozi wa dini ya Kikristo hasa wale Roman Katoliki nao wamekuwa wakituhumiwa kuwanajisi watoto wa kiume ambao hufika makanisani kujifunza dini na wengine pia wakafikishwa mahakamani kwa makosa ya kulawiti.
Malalamiko hayo ya mapadri kuwanajisi watoto wa kiume ambayo yamezaaga karibu dunia nzima, hivi karibuni yalimlazimu Kiongozi wa Kanisa hilo la Katoriki Papa Benedict akiwa kwenye ziara yake nchi moja , kuomba radhi kwa vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya mapadri kwaniaba ya kanisa hilo.
Kwa muktadha huo hapo juu, sioni sababu ya kupinga utekelezwaji wa agizo la Uingereza licha tayari serikali yangu imetoa tamko la kulipinga.
Kwani hakuna ubishi kwamba Tanzania licha inautajiri mkubwa tu, taifa letu limeamua kuwa tegemezi kwa nchi zilizoendelea.Na siyo tu serikali yetu imeamua kuwa tegemezi pia hata vyama vya siasa si CCM,Chadema, CUF na vingine navyo vimegeuka kuwa omba omba ‘Matonya’ kwa ama wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya nchi au vyama vya siasa vya nchi zilizoendelea kikiwemo cha huyo David Cameroon na vimekuwa vikipatiwa misaada ya kifedha, mafunzo na vifaa mbalimbali.
Ukizigeukia hizo taasisi binafsi zinazojiita taasisi za wanaharakati uchwara ambazo kila kukicha zimekuwa zikiishutumu bajeti ya serikali kutegemea wafadhili, wakati kumbe taasisi hizo nazo zinaendeshwa kwa kutegemea fedha hizo hizo za wafadhili.
Tumuulize huyo Bernad Membe ni kwanini asingepinga agizo hilo pale pale wakati Swahiba wetu Cameroon anaongea kule Australia?
Membe kasubiri amefika hapa nchini kwa sisi malofa wenzie ndiyo anajifanya mwamba kwa kutoa tamko la kupinga agizo hilo?Ananichekesha sana.
Binafsi nazifahamu fika hulka za wanasiasa wa Tanzania, wengi wao ni wanafiki na wazandiki wakubwa, kwani wanachokisema adharani siyo wanachokifiria wala kukitenda.
Ieleweke wazi ule mshikamano na umoja wa kweli wa nchi za Jumuiya ya Afrika haupo tena.Kila nchi inaangalia maslahi yake kwanza tofauti na awali.Hivyo katika utekelezwaji wa agizo hilo mwisho wa siku msije mkashangaa nchi zingine za Afrika ikiwemo Tanzania zikaridhia kutekeleza agizo hilo kwa kigezo kwamba wanaogopa kunyimwa misaada.
Wanasiasa kama mnakataa sheria hiyo isitungwe hapa nchini basi hata wakati wa Uchaguzi mkatae kupigiwa kura za ndiyo na hao mashoga, wasagaji.
Katika mawazo yangu nitabaki nikiamini kuwa David Cameroon hakutoa agizo lile kwa bahati mbaya ndani ya mkutano ule maana hatukuona hata rais yoyote ndani ya mkutano ule aliyejitutumua kunyosha kidole kupinga agizo hilo la Bwana Mkubwa “Cameroon’ ambaye nchi yake imekuwa ikitupatia misaada kila wakati, kulipinga.
Nimalizie kwa kuwataka watanzania watambue misemo hii yenye maana kubwa ndani yake kuwa “Maskini hana kiapo, Hakuna bingwa wa shida,na ukijua kupokea ujue na kutoa.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
0716 774494:www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Novemba 8 mwaka 2011.
1 comment:
ifahamike kwamba kila kitu hakikosi sababu kwani kuendelea kuzilazimisha nchi za afrika kukubaliana na sheria hiyo ni kuzipa uwezo nchi za ulaya katika kutekeleza mipango yao ikiwemo huo wa kuanzisha ndoa za jinsia moja kwa lengo la kupunguza kuzaliana kwani njia mbalimbali zinafanya kuhakikisha kizazi cha afrika kinateketea ivi tunaenda wapi ivi kweli waafrika hasa tanzania tumeshindwa kujitegemea hakika tanzania tunahitaji rais dictator huu ujinga tumeuchoka na kama hilo litapita basi aanze kuolewa atakae pitisha hilo agizo ili aone utamu wa ndoa hiyo
Post a Comment