Header Ads

MHASIBU WA TRA KORTINI KWA UDANGANYIFU

Na Happiness Katabazi


MHASIBU wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Sangu John alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu jana na kusomewa mashitaka 132 akidaiwa kujipatia zaidi ya Sh milioni 944 mali ya mwajiri wake kwa njia za udanganyifu pamoja na kulipa mishahara hewa.


Mashitaka hayo aliyosomewa mbele ya Hakimu Aloyce Katemana na mawakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ben Lincon, Osward Tibabyekomya wakisaidiana na wakili wa serikali Shadrack Kimaro. Mashitaka yalikuwa ni ya kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri wake, kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na kusababisha hasara kwa mamlaka hiyo Sh 944,169,330.

Shitaka la kwanza alidaiwa June 19, 2006 katika ofisi za TRA makao makuu yaliyoko wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kwa nia ya kudanganya alighushi orodha ya malipo ya mshahara kwa mwezi huo, akionyesha wafanyakazi hewa tisa wa shirika hilo walitakiwa walipwe Sh 12,000,000 akijua si kweli.

Katika mashitaka ya kutumia nyaraka kumpotosha mkuu wake wa kazi, alidaiwa moja wapo alidaiwa June 20, 2006 ofisi za TRA akiwa mwajiriwa aliwasilisha orodha hiyo kwa mkuu wake wa kazi akidai kwamba wafanyakazi hao walitakiwa kulipwa fedha hizo huku akijua sio kweli.

Mashitaka mengine alidaiwa kwa nia ya kudanganya alijipatia kutoka benki ya NBC fedha hizo akijidai kuwalipa watu hao kwa mshahara wa mwezi June 2006.
Katika mashitaka mengine alidaiwa kudai malipo hayo hewa miezi mingine kuanzia June 2006 hadi Augost 2009.

Mashitaka mengine John alidaiwa alighushi nyaraka kuonyesha mishahara ya wafanyakazi wa TRA mwezi Novemba ni Sh 2,207,122,430 akijua sio kweli, alidaiwa kuendelea kumdanganya mwajiri wake katika miezi mingine katika kipindi hicho akionyesha mishahara tofauti na iliyokuwa ikistahili wafanyakazi wa TRA kwa mwezi.

Aidha mshitakiwa huyo alishitakiwa pia kwa kufanya mchezo huo aliisababishia hasara mamlaka ya Mapato Tanzania ambayo ndio ilikuwa mwajiri wake Sh 944,169,330.

John alikana mashitaka yote na kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kutoa nusu ya fedha hiyo ambayo ni Sh 472,084,665. Kesi hiyo imepangwa kutajwa Desemba 5 mwaka huu na upelelezi haujakamilika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 24 mwaka 2011.

1 comment:

Jigambe Team said...

Hii ndo tanzania inayotakiwa...! from jigambeads.com

Powered by Blogger.