Header Ads

DK.MKUMBO,MWIKABWE HAWANA KESI YA KUJIBU-MAWAKILI




Na Happiness Katabazi

UPANDE wa utetezi katika kesi  ya kutoa lugha ya matusi dhidi ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama Mapinduzi(CCM), Mwigulu Nchemba inayowakabili makada wawili wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Mwita Mwikabwe Waitara na Dk.Kitila Mkumbo wameiomba Mahakama ya Wilaya ya Singida iwaone washitakiwa hao hawana kesi ya kujibu.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na kosa hilo la kutoa lugha ya matusi dhidi ya Nchemba kuwa Nchemba ni mpumbavu,mzinzi, mwasheretani na ni msanii kuwa walilitenda mnamo Julai 14 mwaka 2012 huko katika Kijiji cha Ndago wilayani Iramba mkoani Singida washitakiwa hao walitamka maneno yasiyofaa dhidi ya Nchemba na kusababisha uvunjifu wa amani hali iliyolifanya  jeshi la polisi kuingilia kati kosa ambalo ni kinyume na kifungu cha kifungu cha 89(1) (a)cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Washitakiwa hao wanaotetewa na wakili wa kujitegemea Onesmo Kyauke na Tundu Lissu waliwasilisha maombi ambayo gazeti hili inayo nakala yake kwa njia ya maandishi ikiwa ni utekelezaji wa amri iliyotolewa na mahakama hiyo Aprili 24 mwaka huu, ambapo mahakama hiyo ilizitaka pande zote katika kesi hiyo kuwasilisha majumuisho hayo.

“Mheshimiwa hakimu neno Mpumbavu siyo tu kama inavyodaiwa na upande wa jamhuri katika kesi hii kwani hata Mwalimu Julias Nyerere katika hotuba zake mbalimbali alikuwa akitumia neno mpumbavu na hakuna hata siku moja alijitikeza mtu kwenda kumfungulia kesi mahakamani kwa kutoa lugha ya matusi , na katika hotuba yake maarufu iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho Demokrasi ndiyo ya mwaka 1992, ambayo ninainukuu hapa chini NYerere alisema hivi:

“Democracy yes, lakini upambavu wa kuchukua nchi hivi hivi tu kwakuwa ‘wakubwa’wakubwa wanazitaka kwamba tusipokubali hatutapata fedha zao…’alisema Nyerere.

Aidha wakili Kyauke alidai kuwa pia alitumia nukuu nyingine ya Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamis Kigwangala alinukuliwa na gazeti la serikali la Habari Leo wakati akichangia bungeni Aprili 14 mwaka huu, ambapo alisema’Chadema ni wapuuzi sana’ na hata Kadinali Polcap Pengo kupitia www.charaz.blogspot.com alinukuwaliwa Pengo akisema ‘baadhi ya wanasiasa wanatabia za kipumbavu na hazina tofauti na wanasiasa waliosababisha vita nchini Rwanda ambao kwa upumbavu wao waliweza kusababisha maafa ya mauji ya alaiki mwaka 1994.

Hivyo wakili Kyauke alieleza kuwa kutokana na maneno hayo ambayo yalitamkwa na viongozi ambao walitumia neno mmpumbavu lakini hawakuchukuliwa hatua lakini washitakiwa wake wamediwa kumuita Nchemba ni mpumbavu, mzinzi wakafungulia kesi, hivyo wao upande wa utetezi wanaona ni jukumu la mahakama kuangalia haki ya mtu kujieleza ambayo ni haki ya kikatiba na pia ni jukumu la mahakama kuangalia kama neno mpumbavu kweli ni kosa na lilistahili kufunguliwa chini ya kifungu cha 89(1),(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu’alidai wakili Kyauke.

“Kupitia ushahidi wa mashahidi wote wa upande wa jamhuri ,sisi upande wa utetezi tumeona upande wa jamhuri wameshindwa kuthibitisha kesi yao na hivyo tunaiomba mahakama hii iwaone washitakiwa wote hawana kesi ya kujibu na iwaachirie huru”alidai wakili Kyauke.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Mei 13 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.