HEKO JWTZ,POLISI KUDHIBITI VURUGU MTWARA
Na Happiness
Katabazi
BILA woga
wala kumung’unya maneno napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa vyombo vya ulinzi na
usalama yaani Jeshi la Ulinzi la Watanzania (JWTZ), chini ya Jenerali Davis Mwamunyange, Jeshi la Polisi na
chini ya Inspekta Jenerali(IGP), Said Mwema na serikali kwa ujumla wake kwa
kuweza kuwadhibiti wale wahuni ambao ni
baadhi ya wakazi wa Mtwara ambapo kwa makusudi wiki hii waliamua kuanzisha
vurugu kubwa mkoani hapo kwa kisingizio kuwa hawataki bomba la gesi lisije Dar
es Salaam.
Maana bila
vyombo hivyo kuingia kazini ni wazi machafuko makubwa yangeendelea kutokea na
kusababisha madhara makubwa mkoani hapo.Tena
napenda kuvitia moyo vyombo hivyo kuwa viendelee kutimiza wajibu wake bila
kuwaonea haya wahuni ambao wana kila dalili za kutumiwa na watu wenye hulka za
kinyang’au kwa maslahi yao binafsi ili mwisho wa siku waone Taifa letu nalo
likitumbukia katika vita, jambo ambalo wahuni hao ambao wamekamatwa na hao
manyang’au wanaowatuma kufanya hivyo hawatafanikiwa.
Hivyo basi
vyombo hivyo vya dola vilikuwa sahihi kabisa katika kufanya oparesheni yake
kule Mtwara hadi vimefanikiwa kumaliza
ghasia hizo na washiriki wa ghasia hizo wameweza kukamatwa na hivi
kinachosubiriwa ni ofisi ya Mkurugunzi wa Mshitaka(DPP),Dk.Eliezer Feleshi na
waendesha mashitaka wake kuwafungulia kesi wale wote waliokamatwa wakishiriki
uhalifu huo.
Tanzania
itaendelea kuwa ni nchi ya mshikamano na amani yake ni mfano wa kuigwa
ulimwenguni licha ya hivi sasa kumeanza kuibuka baadhi ya matukio yasiyopendeza
yanayoashiria uvunjifu wa amani lakini,kwakuwa vyombo vya unzi na usalama vipo
imara wahusika wanakamatwa na kisha kufikishwa mahakamani na kwa wale wafuasi 53
wa Sheikh Issa Ponda , Machi 21 mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi iliwafunga
jela mwaka mmoja baada ya kuwakuta na hatia ya kufanya mkusanyiko haramu,
kukaidi amri ya jeshi la polisi.
Na Mei 9
mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu pia ilimhukumu kifungo cha mwaka
mmoja nje ,Sheikh Ponda baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kuingia kwa jinai
katika kiwanja cha Chang’ombe Markas.
Sasa na nyie
wahuni wa Mtwara mnaofanya vurugu mjifunze katika hukumu hizo mbili wale
vihelehele waliokuwa wakiandamana wakitaka kwenda kwa ofisini kwa
DPP-Dk.Feleshi ili wamshinikize aondoe hati yake ya kumfungia dhamana Ponda,
walikamatwa na kufikishwa mahakamani na wakafungwa gerezani mwaka mmoja na hivi
sasa wamesambazwa katika magereza kadhaa hapa nchini, na huyo Ponda waliyokuwa
wakimpigania yeye kafungwa kifungo cha nje.
Sasa na nyie
wahalifu mliofanya uhalifu Mtwara nawasii sana mjifunze kutokana na hukumu
hizo, kuwa kama kuna mtu anawatuma kufanya uhalifu huo basi mkae mkijua mtu
huyo anawatoa kafara nyie kwani mtaoshughulikiwa moja kwa moja ni nyie na
mtakaopata madhara makubwa ya kisheria ni nyie.
Na vurugu za
madai ya kidini katika mkoa wa Dar es Salaam, baada wahusika kukamatwa na
kufikishwa mahakamani, zimetulia, Dar es Salaam, hivi sasa ipo shwari na nchi inazidi kusonga mbele.Hivyo kule Mtwara
napo mamlaka husika inatakiwa itumie sheria kuwashikisha adabu wavunjivu wote
wa sheria.
Wiki hii
Tanzania ilijikuta ikiandika historia mbaya katika sura ya dunia kwasababu ya
ghasia kubwa zilizotokea mkoani Mtwara na kusababisha mtu mmoja kupoteza maisha
na wengine,kujeruhiwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo makazi yao na sehemu zao
za kufanyia biashara kuaribiwa.
Chanzo cha
vurugu hizo zinaelezwa kuwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo la Kigoma Mjini
kumaliza kusikiliza hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini iliyowasilishwa na
waziri wa wizara hiyo Profesa Sospitha Muhongo.
Na baadhi ya
wakazi wa Mtwara wamekuwa wakikataa gesi iliyogundulika Mtwara, isiletwe Dar es
Salaam.
Itakumbukwa
kuwa Januari mwaka huu, wananchi wa Mtwara walipozusha ghasia ,niliandika
makala na niliiweka kwenye ukurasa wangu wa facebook ambayo dhima ya makala
yangu ilikuwa ikimshauri Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP),Dk.Eliezer Feleshi
awafikishe mahakamani wale wote walioshiriki kwenye vurugu za Januari mwaka huu
huko Mtwara kwa kisingizo wanazuia bomba la Gesi lisijengwe kutoka Mtwara kuja
Dar es Salaam.
Kuna usemi
usemao ‘Vita haina macho’.Sasa vurugu zile zilizotokea wiki hii Mtwara naweza
kuzifananisha na vita baaida ya wananchi hao ambao kwa makusudi waliamua
kujichukulia sheria mkononi na kuanza kufanya uhalifu na kujibishana jeshi la
polisi kwa kisingizio kuwa bomba la gesi lisijengwe kutoka Mtwara kuja Dar es
Salaam.
Na matokeo
ya kitendo hicho cha kujichukulia sheria mkono kilichofanywa na baadhi ya
wananchi wa Mtwara ndicho mwisho wa siku kilichopelekea Jeshi la Polisi kuingia
kazini kama kifungu cha 20, 21(2) vya Sheria
ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 inavyoanisha wazi majukumu ya
jeshi hilo.
Ambapo
kifungu cha 20 kinampa polisi mamlaka wakati akifanya jukumu lake la ukamataji
wa mwarifu/waharifu kuvunja eneo lolote na kuingia kumkamata mwarifu huyo kwa
lengo la ku.Wakati kifungu cha 21(1) kinamruhusu ofisa wa polisi kutumia nguvu
wakati akikamata waharifu.
Kwa
mtiririko huo ndiyo maana nimelazimika kutumia msemo huo kuwa ‘Vita haina macho’
kwani vurugu za Mtwara zilipoanza kufanywa na baadhi ya wakazi wa Mtwara ambao nao wahuni hao walikuwa na silaha za
jadi mkononi zilisababisha Jeshi la Polisi kuingia kazini na kuanza
kuwashughulikia wale wote waliokuwa wakifanya vurugu hizo na mwisho wa siku hata wale ambao
hakushiriki katika vurugu hizo kwa njia moja ama nyingine wameathiriwa na
vurugu hizo na wengine wakijikuta wamepoteza mahali pa kuishi.
Lakini
Binafsi nimekuwa nijikijiuliza kuwa mbona kila kukicha tunasikia kwenye vyombo
vya habari vikitoa nafasi kubwa ya kusikika habari za wale wahuni wanaofanya
vurugu Mtwara lakini hatuoni vyombo hivyo vya habari vikitoa nafasi kwa wakazi
wengine wa Mtwara ambao hawawaungi mkono wahuni hao?
Je ina maana
ni wakazi wote wa Mtwara wanataka bomba la gesi lisijengwe kuja Dar es Salaam
kwa niia ya vurugu kama zile? Kule Mtwara kuna waandishi wenzetu lakini mbona
hatusikii waandishi wenzetu hao wakienda kuwahoji wakazi wa Mtwara ambao
wanapingana na wenzao kwa kuwasilisha madai yao kwa njia ya vurugu?
Wakati
umefika sasa kwa waandishi wenzetu wa Mtwara kutuletea habari toka kwa wananchi
wengine ambao hawaungi mkono kudai dai hilo kwa njia ya vurugu.Kwani kwa
kushindwa kufanya hivyo,jamii italazimika kuamini wakazi wote wa Mtwara nao
wanaunga mkono wahalifu hao.
Maana
binafsi sikubaliani kuwa ni wakazi wote wa Mtwara wanawaunga mkono wenzao wale
wanaodai kiwanda cha gesi kijengwe Mtwara kwa njia ya vurugu.
Sote
tunafahamu kuwa Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa kufuata utawala wa sheria, na
inamruhusu mtu yoyote yule ambaye anaona haki yake imeporwa au kuvunjwa aende
mahakamani kuidai.
Sasa hawa
waliofanya vurugu Mtwara walikuwa wanapaswa kwenda kudai dai hilo kwa njia ya
amani na kama wangeshindwa wangechangisha fedha wakamweka wakili ,akafungua
kesi ya madai ya kupinga bomba hilo lisijengwe kuja Dar es Salaam, kwaniaba
yao,kuliko uhuni walioufanya.
Licha kuna
watu wamekuwa wakidai kuwa wananchi hao hawajapewa elimu ya kutosha, mi binafsi
sikubaliani na hilo kwani elimu imetolewa ila tu hawa waliofanya vurugu tayari
wana ajenda yao mbaya mioyoni na akili mwao.
Kwani hata
kama hoja ni kwamba hawajapewa elimu ya kutosha, ni kwanini siku Waziri wa
Nishati Profesa Mhongo alipomaliza kusoma bajeti yake,wakaanzisha vurugu?Tena
kama ya bajeti kusomwa siku mbili nyuma walisambaza vipeperushi vya kufanya
vurugu siku hiyo.
Tuwaulize
wahalifu wale hivi siku hiyo Waziri Mhongo aliingia mkataba na wahalifu wale wa
kuwapatia elimu ya gesi akiwa bungeni wahalifu wale ?
Tunachokifahamu
sisi waziri huyo alikuwa akienda kusoma bajeti ya wizara inayohusu nchi nzima
siyo wakazi wa Mtwara.Kwahiyo nasisitiza kuwa wale waliofanya vurugu Mtwara ni
wahuni na ni wahalifu kama walivyowahalifu wengine, na sheria za nchi zipo ,na
ziwashughulikie kikamilifu ili wasiweze kurudia kufanya uhalifu huo ambao
umesababisha watu kupoteza maisha, makazi ya watu kuaribiwa.
Nafahamu
watu watailamu jeshi la polisi ,lakini tunapaswa tujiulize kwanza hivi kama
wale wahalifu wasingezusha vurugu siku ile, jeshi la polisi na JWTZ lingeingia
mtaani kukabiliana na wahalifu wale?Jibu ni jepesi tu ,JWTZ na Polisi
wasingepoteza muda na nguvu zao kuingia mtaani mjini Mtwara na kupambana na
wahalifu wale ambao tayari wameishaipaka matope nchi.
Kwa kitendo
kile walivyokifanya ,hata kama walichokuwa wakikidai ni sahihi, wakae wakijua
wamevunja sheria za nchi, na watafikishwa mahakamani kwa makosa ambayo yatakuwa
yameandaliwa na waendesha mashitaka wetu na hapo ndipo itakapokuwa imeanza
safari yao ya utumwa baina ya wahalifu hao na Mahakama na mahabusu.
Kwa watu
wanaofikiri sawa sawa ,inawawia vigumu kuamini hawa wananchi ni wao wenyewe ndiyo
wanaojituma kufanya uhalifu huo ule kwa kisingizio cha dai hilo.
Kwani hawa
wananchi kwa muda mrefu walikuwa wakilalamika kucheleweshea malipo yao ya mauzo
ya Korosho lakini hata siku moja hatujawahi kuwaona wakifanya uhalifu wa haina
ile.
Na kama
kweli dai lao ni hilo ni la kukataa bomba la gesi lisije Dar es Salaam, dai
ambalo na fahamu haliwezi kutekelezekwa kwasababu ni dai lisilo na tija ,ni
kwanini wahalifu hao wakimbilie kuchoma nyumba za viongozi ,mahakama, ofisi za
CCM,na nyumba ya Mwandishi wa Habari ?
Naviomba
vyombo vya dola ikiwemo Polisi, JWTZ na Idara ya Usalama wa Taifa, ifanye kazi
yake ya uchunguzi ili kujua kama kweli wahalifu hao wanadai hilo kweli? Nani
anawapa jeuri na morali wahalifu hao
kufanya uhalifu ule bila woga tena kwa njia haramu?
Huenda kuna
kikundi cha wadhalimu kipo nyuma ya hawa wahalifu kina watuhumia wahalifu hawa
kufanya uhalifu huo kwa kisingizio cha kukataa bomba hilo lisije Dar es Salaam,wakati
wakifahamu wazi hao wahalifu wanachokikataza hawana mamlaka nacho.
Naamini dola
likiamua kufanyakazi yake kikamilifu huko Mtwara,inauwezo wa kubaini kilichopo
nyuma ya pazia ya chanzo cha vurugu hizo na itawadhibiti na dai hilo litakuwa
ndoto kwa wahalifu hao.
Kwani mifano
ya dola kusambaratisha vikundi vya wahalifu hao hao ni mingi sana na wala si
yakutafuta.Mfano vyombo vya ulinzi na usalama vilivyofanikiwa kuwasambaratisha
wale baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu Mkoani Dar es Salaam, mwaka jana na
Machi mwaka huu ,waliokuwa wakiendesha maandamano haramu kwa kisingizio cha
kutetea uislamu, kutokomeza ujambazi katika mikoa ya Kigoma, Kagera na Arusha, vurugu
za Msikiti wa Mwembe Chai, ujambazi wa
kutisha katikati ya jiji la Dar es Salaam, kati ya miaka ya 2006 muda mfupi tu
tangu Rais Jakaya Kikwete Desemba 21 mwaka 2005, alipoapishwa kushika madaraka
ya urais.
Narudia tena
bado ninaimani kubwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuwa vikiamua kufanya kazi
vinafanyakazi yake kikamilifu na ndiyo maana hata leo hii nimejitokeza
kuvipongeza kwa kuweza kurejesha amani mkoani Mtwara ambayo ilitoweka kwa siku
mbili kwaajili ya vurugu baina ya wahalifu wale na vyombo vya dola.
Niitimishe
makala yangu kwa kuvipongeza vyombo kwa kufanya oparesheni hiyo ambayo imezaa
matunda na kukata ngebe za hao wahalifu ambao ambao kama ya kupata mkong’oto wa
wana usalama walijitapa kuwa wapo tayari kufa kwaajili ya kuipigania gesi.
Lakini cha
kushangaza wahalifu hao waliokuwa wakijitapa kuwa hawaogopi dola, leo hii wamefya
mkia kwa kuhofia oparesheni hiyo.
Nimejiuliza
kuwa hivi mpiganaji gani ambaye ameapa kufa kwaaiili ya kuipigania gesi asalimu
amri baada ya polisi kuwatembezea mkong’oto?
Shujaa au
mpiganaji yoyote huwa aogopi polisi wala bunduki.Sasa iweje hawa waliojitapa
kutoliogopa dola na kuamua kujichukulia sheria mkononi leo hii wameona JWTZ na
Polisi wamekalia kooni wameshusha silaha chini? Ni wazi hawa ni watu waoga
kwani kama siyo waoga wangejitokeza kupambana na askari hao ili tuwajue kuwa
nao ni mahodari na wapo tayari kwa lolote.
Tanzania ni
nchi inayooendelea hivyo binafsi sioni kama ni muda mwafaka kwa sisi wananchi
hususasini wakazi wa Mtwara kuanza kujiingiza kwenye vurugu badala ya kushiriki
kwenye shughuli za kujiletea maendeleo na taifa letu.
Wanahabari
na wananchi wengine wote wapenda amani na tunaoheshimu utawala wa tuukatae
uhuni unaofanywa na wahalifu wale wanaofanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwa
kisingizio cha kuzuia bomba la gesi lisijengwe kuja Dar es Salaam,kwani una
hatarisha amani na wanaoteseka ni watoto na wanawake na miundombinu yetu
inaaribika ambayo imejengwa kwa kodi zetu.
Pia napenda
kutoa raia kwa wale wananchi wote ambao wamechoka kuishi hapa Tanzania katika
nchi yenye amani, basi ni wakati mwafaka kwa watu hao wapenda vurugu kwenye
kuamia katika nchi zenye vita ili wakaishi huko kwenye nchi zenye vita wafurahi
zaidi ,kuliko kuishi hapa nchi na kuanza kutuletea vurugu ambazo zinahatarisha
amani yetu ambazo sisi wengine hatutaki vita jamani.
Mwisho
nimalizie kwa kuvipongeza vyombo ya dola yaani Polisi na JWTZ kwa kuweza
kuwadhibiti wahalifu wale walioleta vurugu kule Mtwara.Na itafute chanzo cha
vurugu hizo kwani hii ni mara ya pili sasa wahuni wale wanazusha vuru hizo kwa
kisingizo hicho na mara ya kwanza vurugu ambazo zilisababisha pia watu kupoteza
maisha ni Januari mwaka huu.
Mungu
ibariki Tanzania,Mungu Ibariki Afrika
Chanzo: www.katabazihappy.blogspot.com
Facebook:happy katabazi , Mei 26 mwaka 2013.
0716 774494
No comments:
Post a Comment