Header Ads

RUFAA YA DPP DHIDI YA ZOMBE YAFUTWA


 Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Rufaa nchini, jana iliifuta rufaa  iliyokuwa imekatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi ya kupinga hukumu ya kesi ya mauji ya  Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyomwachiria huru aliyekuwa    Mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Dar es Salaam(ACP)-Abdallah Zombe na wenzake baada ya kubaini kuwepo kwa dosari katika hati ya kukatia rufaa hiyo.

Uamuzi huo ulitolewa jana na jopo la majaji wa tatu  Edward Rutakangwa,Mbarouk Mbarouk na  Bethek Mila.Uamuzi huo unatokana na jopo hilo Aprili 22 mwaka huu, iliposhindwa kuanza kusikiliza rufaa hiyo Na.254/2009  baada ya jopo hilo kubaini dosari katika hati hiyo   ambapo mawakili wa mwomba rufaa Timon Vitalis na Richard Rweyongeza walikiri dosari hiyo na wakaiomba mahakama iwapatie muda wa kwenda kuifanyia marekebisho hati hiyo ya kukatia rufaa.

Jaji Mbarouk siku hiyo ndiyo aliyeibaini dosari hiyo ambayo dosari yenyewe ni kwamba katika hati ya kukataa rufaa, DPP alisema anapinga hukumu ya kesi ya mauji Na. 26/2006 iliyokuwa ikimkabili Zombe na wenzake kuwa ilitolewa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Salum Massati. Wakati DPP alipaswa kuandika Jaji Salum Massati ambaye wakati akisikiliza kesi hiyo alikuwa  ni  Jaji wa Mahakama Kuu  na wakati akiendelea kusikiliza kesi hiyo aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa , hivyo DPP katika hati yake ya kukata rufaa alipaswa amtambulishe kuwa hukumu ile ilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Massati na siyo jaji wa mahakama ya rufaa.

Akitoa uamuzi huo, jopo hilo lilisema kuwa ibara ya  119 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasomeka kama ifuatavyo:

“Jaji yoyote  wa Mahahakama ya Rufani hatakuwa na mamlaka  ya kusikiliza shauri lolote katika Mahakama Kuu  au katika mahakama ya hakimu  ya ngazi yoyote.:
“Isipokuwa kwamba iwapo jaji yeyote wa mahakama kuu atateuliwa  kuwa Jaji Mahakama ya rufaa, basi hata baaa ya kuteuliwa kwake kuwa jaji wa mahakama ya rufani,jaji huyo  aweza kuendelea kufanyakazi kazi zake katika mahakama kuu mpaka amalize  kutayarisha  na kutoa hukumu  au mpaka akamilishe shughuli nyingine yoyote  inayohusika na mashauri  ambayo yalikwisha anza kuyasikiliza kabla kabla  hajateuliwa  kuwa jaji  wa mahakama rufani, na kwamba ajili hivyo itakuwa  halali kwake  kutoa hukumu  au uamuzi  mwingine wowote unaohusika kwa kutumia  kutumia au  kutaja madaraka  aliyoshika kabla  ya kutueliwa  kuwa jaji wa mahakama ya rufani,  lakini endapo hatimaye hukumu hiyo au uamuzi  mwingine utapingwa kwa njia  ya rufaa itayofikishwa mbele ya  mahakama ya rufani,basi katika hali  hiyo jaji  huyo  wa mahakama ya rufani,hatakuwa  na mamlakaya kusikiliza  rufaa hiyo:inasomeka ibara hiyo.

Jaji Rutakangwa alisema kwa mujibu wa matakwa ya ibara hiyo, na kwakuwa wakili Vitalis alikiri dosari hiyo, mahakama yake imefikia uamuzi wa kuona hati ya rufaa ina dosari na kwa dosari hiyo mahakama yake imeona hakuna rufaa mbele yake na hivyo imefikia uamuzi wa kuifuta ombi hilo la rufaa iliyofunguliwa na DPP dhidi ya Zombe na wenzake.

Aidha alisema pia mahakama yake inatoa fursa kwa DPP kuwasilisha ombi la ukomo wa muda mahakamani hapo kama wataona kuna haja ya kufanya hivyo.

Baada ya uamuzi huo kumalizika kutolewa Zombe na wajibu rufaa wenzake na familia zao walikumbatia kwa furaha na Zombe aliwaambia waandishi wa habari kuwa uamuzi huo ni wa haki na kwamba siku zote wamekuwa hawalali vizuri kwaajili ya kuwaza rufaa hiyo na kwamba huo ndiyo umwe mwisho wa serikali kubambikizia watu kesi kwani ni upande wa jamhuri katika katika kesi hiyo ulikiri mahakamani kuwa  hakuwepo eneo la tukio lakini wanaendelea kumshitaki na kwamba huko nikupoteza fedha za umma na matumizi mabaya ya mahakama.

“Kwa kweli namshukuru mungu, na ninataka jamhuri ielewe kuwa serikali sheria siyo hisia, na sheria hailazimishwi….hatulali vizuri kwaajili ya kuwaza rufaa hii lakini leo hii mungu amewaongoza majaji hawa kutenda haki…namshukuru sana mungu….sheria jamani hailazimishwi na muache kubambikia watu kesi, siyo vizuri jamani”alisema Zombe nje ya viunga vya mahakama.

Aprili 22 mwaka huu, Mahakama ya Rufaa , ilijikuta ikishindwa kuanza kusikiliza rufaa hiyo  baada ya mahakama hiyo kubaini dosari hiyo katika hati ya kukata rufaa.

Kwa upande wao mawakili wa serikali wanaomwakilisha  DPP, Vitalis Timon, Prudence Rweyongeza, Mgaya Mtaki, Alexander Mzikila, Edwin Kakoraki walikiri dosari hiyo na waliomba mahakama hiyo iwapatie ruhusa ya kwenda kufanyia marekebisho dosari hiyo chini ya Kanuni ya 4(2),(2),(b) ya Sheria ya Mahakama ya Rufaa na kwamba hata jana walikuwa wapo tayari kufanyia marekebisho hati hiyo ya kukata rufaa ambayo jicho la mahakama limeona ina dosari na kisha  jana hiyo hiyo kuirejesha upya mahakamani.

Hata hivyo mawakili wa wajibu rufaa Richard Rweyongeza, Majura Magafu, Denis Msafiri  walianza kwa kuishukuru mahakama kuwa jicho mahakama limeweza kubaini dosari hiyo na kwamba kwa dosari hiyo ni kwamba hakuna hati ya rufaa mbele ya mahakama hiyo na kwamba akaiomba mahakama ikatae kuwapa muda wa kufanyia marekebisho kwani tayari muda wa kukata rufaa umeishapita na kwamba kama wanataka kukata rufaa watalazimika kuwasilisha ombi la kuongezewa muda ambao ni siku 30 chini ya kanuni ya 68(1) ya Mahakama ya Rufaa.

Akijibu hoja hiyo wakili Vitalis alidai Kanuni ya 4(2),(a),(b) ya Mahakama ya Rufaa inaipa mamlaka kutoa amri ya kuwaruhusu kwenda kufanyia marekebisho hati hiyo ila wanakiri ni kweli hati yao yao waliyoitumia kukata rufaa ina mapungufu hayo.

Agosti 17  mwaka 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa hukumu ya kihistoria ya kesi ya mauji ya watu wanne iliyokuwa ikimkabili Zombe na wenzake ambapo jaji Salum Massati ambaye hivi sasa ni jaji wa mahakama ya rufani aliwaachilia huru Zombe na wenzake ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi hiyo kwa maelezo kuwa upande wa jamhuri ulishindwa kuleta ushahidi mzuri ambao ungewea kuishawishi mahakama hiyo iwaone washtakiwa hao wana hatia.


Baada ya hukumu hiyo ya mahakama kuu, DPP hakulidhishwa na hukumu hiyo Oktoba 7 mwaka 2009 akakata rufaa Mahakama ya Rufaa ,  kupinga hukumu hiyo ambayo kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya mahakama ya rufaa,rufaa hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa Aprili 22 na 23  lakini ikashindikana.

Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Christopher Bageni, Ahmed Makele, WP 4593 PC Jane Andrew, D 1406 Koplo Emmanuel Mabula, D 8289 DC Michael Shonza, D. 2300 Abeneth Saro, D.4656D/Koplo Rajabu Bakari na D.1317D/XP Festus Gwasabi na jana washtakiwa wote walifika mahakamani hapo.

Washitakiwa hao walidaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa wilayani Ulanga, mkoani Morogoro; Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe pamoja na dereva teski Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Mei 9 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.