Header Ads

MKURUGENZI WA SIMON GROUP AUNGANISHWA KESI YA IDD SIMBA

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mkurugenzi  Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group Limited, iliyonunua hisa za Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam, Robert Simon Kisena ameunganishwa katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, Idd Simba na wenzake.

Sambamba na hatua hiyo, pia Idd Simba na wenzake ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya awali ya matumizi mabaya ya madaraka, wamefutiwa kesi hiyo na kufunguliwa kesi upya  ambapo wameongezewa kosa jingine la uhujumu uchumi.

Kutokana na mabadiliko hayo,washtakiwa walisomewa mashtaka sita yakiwamo ya rushwa,uhujumu uchumi,matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh8.4 bilioni.Wakili wa Serikali, Oswald Tibabyekomya alidai mahakamani kuwa baada ya kuchambua ushahidi wamebaini kuwa makosa hayo yanaangukia katika Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Mbali na Idd Simba ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na Kisena ambaye ni mshtakiwa wa nne, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 3 ya mwaka 2013, ni Salimu Mwaking’inda na Victor Alfred Milanzi.Mwaking’inda, ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo alikuwa Mkurugenzi wa UDA na Milanzi ambaye ni mshtakiwa wa tatu, alikuwa ni Meneja Mkuu wa UDA.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka hayo mapya jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na walisomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali Awamu Mbagwa. Hata hivyo Kisena hakuwapo jana mahakamani wakati wenzake wakisomewa mashtaka.
Washtakiwa waliokuwapo mahakamani jana nipamoja na Simba, Mwaking’inda na Milanzi waliokana mashtaka yote.

Wakili Tibabyekomya alidai kuwa Kisena hakuwapo mahakamani hapo jana kwa kuwa taratibu za kumfikisha mahakamani zilikuwa bado hazijakamilika.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka waliyosomewa jana, shtaka la kwanza la kula njama linawahusu Simba na Milanzi na Kisena.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, jijini Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama za kutenda kosa la vitendo vya rushwa, kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya mashtaka, shtaka la pili la vitendo vya rushwa linamhusu Kisena peke yake, hata hivyo shtaka hilo halikusomwa kutokana na mshtakiwa huyo kutokuwapo mahakamani.

Shtaka la tatu ni la vitendo vya rushwa ambalo linawahusu Simba na Milanzi. Wakili Mbagwa alidai kuwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, walikubali kupokea Sh320 milinoni kutoka kwa Kisena ushawishi wa kuiuzia Simon Group hisa za UDA ambazo zilikuwa bado hazijagawiwa.

Katika shtaka la nne ambalo ni la matumizi mabaya ya madaraka, linawahusu Simba , Mwaking’inda na Milanzi.

Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com; Mei Mosi mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.