Header Ads

ZOMBE,LWAKATARE KUCHEKA AU KULIA LEO
Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Rufaa nchini leo inatarajia kutoa uamuzi rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Abdallah Zombe wa kuifuta au kuto ifuta rufaa iliyokatwa na DPP baada ya jicho la mahakama kuona hati ya kukatia rufaa ina dosari.

Sambamba na hilo, pia Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo inatarajia kutoa uamuzi wa kuifuta au kutoifuta kesi ya tuhuma za ugaidi za kutaka kumteka Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Denis Msaki ainayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo(Chadema),Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.

Uamuzi wa ombi hilo la kuomba mahakama kuu ifanyie mapitio  majalada ya kesi ya msingi iliyopo mahakama ya kisutu inayomkabili Lwakatare ilifunguliwa mahakamani hapo mbele ya Jaji Lawrance Kaduri na washitakiwa hao, ambapo lilisikilizwa Aprili 15 mwaka huu, ambapo mawakili wa Lwakatare, Peter Kibatara, Tundu Lissu na Mabere Marando walidai kitendo alichofanya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hakikuwa cha lazima. Kwamba licha ya mkurugenzi huyo kuwa na mamlaka ya kufuta kesi, lakini anapofanya hivyo lazima aoneshe amefuta kwa masilahi ya umma, kutafuta haki au pengine kuzuia mahakama isidhalilike na hukumu ambayo ingetolewa.

Mawakili hao walidai  kuwa kesi iliyofutwa na kurejeshwa tena Kisutu ilikuwa ni matumizi mabaya ya mamlaka ya DPP, hivyo kuiomba Mahakama Kuu kupitia upya mwenendo wa kesi namba 37/2013 iliyofunguliwa Kisutu kwani ilifunguliwa kwa nia ya kumdhalilisha mtuhumiwa.

Walihoji iliwezekanaje kufuta kesi na kuifungua ndani ya muda mfupi, kwamba walipata wapi ushahidi mwingine mpya.

Mawakili hao wa utetezi wanaiomba Mahakama Kuu ifanye yafuatayo:
Kwanza, ipitie mwenendo wa kesi zote mbili, namba 37/2013 na 6/2013 ili kujua kama zina hoja ya msingi, halali au la.

Pili, wanaomba mahakama iamrishe kuwa mwenendo wa kesi namba 6 urudi katika kesi namba 37, ili Mahakama ya Kisutu iweze kutoa hukumu kutokana na mambo yaliyokuwa yanabishaniwa kisheria.

Tatu, wanaiomba Mahakama Kuu kuingilia mchakato wa ‘nole’ (hawana hatia) iliyotolewa na DPP kwa muda mfupi kisha kumtia mtuhumiwa hatiani, ambavyo ni kinyume kabisa cha madaraka ya DPP.
Nakuongeza kuwa anaiomba mahakama kuu iifute kesi ya msingi inayowakabili washitakiwa hao kwa sababu kosa la pili, tatu na nne hayaoneshi nia ya washitakiwa hao kutenda makosa ya ugaidi, alidai kuwa hoja hizo zimeletwa wakati usio sahihi kwani kesi ya msingi ipo katika hatua za uchunguzi, upelelezi bado haujakamilika.

Kwa upande wao mawakili wanaomwakilisha DPP,Prudence Rweyongeza, Ponsian Lukosi wakijibu hoja za mawakili wa washitakiwa pangua  ambazo zilidai DPP alitumia madaraka yake vibaya kuifuta kesi Na. 37/2013 na akazitaja sababu zilizosababisha aifute kesi hiyo na kufungua kesi mpya Na. 6/2013 Machi 20 mwaka huu, kwa kuwa mashitaka ni yale yale.

RWeyongeza alitaja  sababu ya kwanza iliyofanya DPP aifute kesi Na. 37 /2013 iliyofunguliwa Machi 18 mwaka huu, kuwa ni uongozi wa Mahakama ya Kisutu kukosea na kuifungua kesi hiyo katika jalada la kesi zinazoendeshwa katika mahakama za chini (Subordinate Court) badala ya kuisajili kesi hiyo katika rejista ya kesi zinazopaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu.

Pili, ni kwamba hakimu aliyeisikiliza kesi hiyo, Emilius Mchauru, alikosea kuwaruhusu washtakiwa hao kujibu mashitaka wakati Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi hiyo ya ugaidi.

“Hivyo basi upande wa Jamhuri tunasisitiza kuwa uamuzi wa DPP wa kuifuta kesi ile ulikuwa wa haki ambao ulikidhi matakwa ya kifungu cha nane cha  Sheria ya Uendeshaji wa Mashitaka ya mwaka 2008,” alidai Rweyongeza.

Aprili 22 mwaka huu, jopo la majaji wa mahakama ya rufaa linaloongozwa na Jaji Edward Rutangakwa na Mbarouk Mbarouk na Milla lilibaini dosari katika hati ya kukata rufaa na kwamba dosari hiyo ni kwamba hati hiyo ilisomeka kuwa Jaji Salum Massati ambaye ndiye alitoa hukumu ya mahakama kuu na kuwamwachiria huru Zombe na wenzake walimtambulisha kuwa ni jaji wa mahakama ya rufaa, badala ya kuandika kuwa wakati huo jaji Massati alikuwa ni jaji wa mahakama kuu na sasa ni jaji wa mahakama ya rufaa na kwa dosari hiyo jopo hilo lilisema mahakama ya rufaa haiwezi kusikiliza rufaa ambayo hukumu yake imetolewa na jaji mwenzao wa mahakama ya rufaa na hivyo rufaa hiyo ikashindwa kusikilizwa hiyo aprili 22 mwaka huu, na likaaidi kwenda kuandaa uamuzi wake kuhusu kubainika kwa dosari hiyo ambapo uamuzi wake wanautoa leo.

 Agosti 17  mwaka 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa hukumu ya kihistoria ya kesi ya mauji ya watu wanne iliyokuwa ikimkabili Zombe na wenzake ambapo jaji Salum Massati ambaye hivi sasa ni jaji wa mahakama ya rufani aliwaachilia huru Zombe na wenzake ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi hiyo kwa maelezo kuwa upande wa jamhuri ulishindwa kuleta ushahidi mzuri ambao ungewea kuishawishi mahakama hiyo iwaone washtakiwa hao wana hatia.

Baada ya hukumu hiyo ya mahakama kuu, DPP hakulidhishwa na hukumu hiyo Oktoba 7 mwaka 2009 akakata rufaa Mahakama ya Rufaa ,  kupinga hukumu hiyo ambayo kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya mahakama ya rufaa,rufaa hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa jana lakini ikashindikana.

Chanzo;Gazeti la Tanzania la Daima la Jumatano, Mei 8 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.