MENEJA BENKI YA CRDB JELA MIAKA MITANO KWA WIZI
Na Happiness Katabazi,Mwanza
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mwanza, imemhukumu kifungo cha
miaka mitano jela Meneja wa Benki ya CRDB,wa matawi ya Nyanza na Bugando mkoani
Mwanza, Daniel Peter Waijaha, pamoja na mteja wa benki hiyo, Dismas Mohamed
Ndaliko baada ya kuwakuta na hatia
wa kosa la wizi wa jumla ya Sh
Milioni 140 mali ya benki hiyo.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Mwanza, Anjelo Rumisha ambaye
alikuwa akisikiliza kesi hiyo ya jinai Na.76 ya mwaka 2011.Ambapo mbali na
adhabu hiyo pia hakimu huyo amemtaka meneja huyo azirejeshe fedha hizo
alizoziiba katika Tawi la Nyanza.
Hakimu Rumisha alisema baada ya kumtia hatiani meneja huyo
pia Meneja wa Business Banking, Stephano Harry Mboma, ambaye alikuwa mshatakiwa
wa pili katika kesi hiyo amemuachia huru
baada ya kuona hana hatia katika mashitaka dhidi yake.
Kwa upande wake Ndaliko (mteja) ambaye alikuwa mshtakiwa wa
tatu katika kesi hiyo alihukumiwa adhabu hiyo kwa kosa la kujaribu kumsaidia
meneja huyo kuepukana na adhabu kwa kufuta ushahidi wa kosa hilo.
Wakati meneja huyo na mteja wakihukumiwa adhabu hiyo, Meneja
wa Business Banking, Stephano Harry Mboma, ambaye alikuwa mshatakiwa wa pili
katika kesi hiyo ameachiwa huru baada ya kuonekana kuwa hana hatia katika
mashtaka yote yaliyokuwa yakimkabili.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Mwanza, Jumatatu ya Juma hili, Anjelo Rumisha, aliyekuwa akisikiliza kesi
hiyo.
Hata hivyo licha ya kuwatia hatiani washtakiwa hao kwa
mashtaka hayo, na kuwahukumu adhabu hiyo, Hakimu Rumisha aliwaachia huru katika
mashtaka mengine yote yaliyokuwa yakiwakabili.
Upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na Wakili wa
Serikali Mwandamizi, David Kakwaya haukuridhika na uamuzi huo wa washtakiwa hao
kuachiwa huru katika mashtaka mengine, na tayari umewasilisha taarifa ya
kusudio la kukata rufaa.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wote kwa
pamoja walikuwa wakikabiliwa na jumla ya mashtaka matano, lakini ni
mashtaka mawili tu ndio yalikuwa yakiwahusu washtakiwa wote watatu, ambayo ni
kula njama kutenda kosa na kughushi.
Katika shtaka la kwanza washtakiwa wote walikuwa wakidaiwa
kuwa katika tarehe tofautitofauti katika miezi isiyofahamika, mwaka 2010,
walikula njama kutenda kosa la kughushi nyaraka.
Shtaka la pili lilikuwa ni la wizi likiwahusu mshtakiwa wa
kwanza Meneja Waijaha na mshtakiwa wa pili, Mboma. Walidaiwa kuwa katika
tarehe na miezi isiyofahamika mwaka 2010, kwa pamoja waliiba Sh 107.8 milioni
katika benki hiyo tawi la Nyanza.
Shtaka la tatu ambalo pia ni wizi lilikuwa likiwahusu
mshtakiwa wa kwanza, Waijaha na wa tatu, Ndaliko (mteja). Walidaiwa kuwa
Desemba 4, 2010, katika benki hiyo tawi la Bugando, waliiba Sh32.15 milioni
mali ya benki hiyo.
Katika shtaka la nne la kughushi, washtakiwa wote walikuwa
wakidaiwa kuwa kati ya Desemba 4, 2010, katika tawi la Bugando, kwa pamoja walitengeneza
nyaraka za uwongo za kuchukulia pesa benki kwa lengo la kufanya udanganyifu.
Ilidaiwa kuwa lengo la nyaraka hizo za uwongo lilikuwa ni
mteja mmoja aitwaye New Ana Filling Station, mmiliki wa akaunti namba
01J1016800800, alichukua pesa kiasi cha Sh 140 miloni katika tawi hilo, jambo
ambalo halikiuwa kweli.
Mshtakiwa wa tatu (Ndaliko) pia alikuwa pia akikabiliwa na
shtaka mbadala la kusaidia kutendeka kwa kosa la wizi.
Alidaiwa kuwa kati ya Desemba 4, 2010, na kwa
siku nyingine baadaye , akijua kuwa mshtakiwa wa kwanza aliiba pesa jumla ya
Sh140 milioni mali ya CRDB, alimsaidia kufuta ushahidi ili kumwezesha kuepuka
adhabu.
Shtaka la tano ni la kuwasilisha nyaraka za uwongo,
lililokuwa likimkabili mshtakiwa wa kwanza peke yake (Meneja Waijaha).
Ilidaiwa kuwa Desemba 4, 2010 katika tawi la CRDB Bugando
Mwanza, akijua na kwa udanganyifu, alitoa risiti ya benki ya kuchukulia pesa
kwa lengo la kuonesha kuwa ilisainiwa na mteja, New Ama Filling Station na
akaunti namba 01J1016800800, jambao ambalo si kweli.
Kwa mujibu wa maelezo ya awali ya kesi waliyosomewa
washtakiwa hao, wizi huo ulibainika baada ya Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani
kumwagiza mkaguzi wa ndani kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika tawi la Nyanza.
Uamuzi huo wa Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani kuamuru
kufanyika kwa ukaguzi wa kushtukiza katika tawi hilo ulitokana na taarifa
zilizopatikana kuwa kulikuwa na tofauti kubwa ya ulali wa pesa katika tawi
hilo.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Mei 30 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment