Header Ads

RAMA 'MLA KICHWA' HURU




Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemwachiria huru mtoto  Ramadhamani Selemani Mussa, maarufu kama ‘Rama mla kichwa’,na mama yake mzazi Hadija Ally waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauji.

Rama na mama yake walikuwa wakikabiliwa na kosa la kuua kwa kukusudia mtoto Salome Yohana (3), kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ya mwaka 2002.

Amri ya kuachiliwa huru kwa Mussa na mama yake ilitolewa jana na jaji Rose Temba ,ambaye alisema mahakama yake imefikia uamuzi huo baada ya kuridhishwa na  ripoti ya jopo la madaktari waliomfanyia uchunguzi wa Akili zake Mussa, iliyoeleza kuwa wakati wa tukio hilo hakuwa na akili timamu.

“Kwa sababu hiyo mahakama hii inamuachiria huru Mussa kwasababu ripoti ya madaktari imethibitisha kuwa wakati Mussa anatenda kosa hilo la kukutwa na kichwa cha binadamu hakuwa na akili timamu.Na pia mahakama hiyo inamuachiria huru mama yake Rama kwasababu Mkurugenzi wa Mashitaka amewasilisha taarifa yake ya kuwa hana nia tena ya kuendelea kumshitakiwa mama huyo chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai”alisema Jaji Temba.



Baada ya jaji huyo kutoa uamuzi huo wa kuwaachilia huru washitakiwa hao, ghafla uamuzi huo ulisababisha mama wa mtoto aliyeuwawa na kichwa cha marehemu kukutwa anacho Mussa, Upendo Dustani na shangazi wa mtoto huyo, Furaha Mussa, aliyekuwa akiishi na mtoto huyo nyumbani kwake Tabata kuangua kilio.

Septemba 29, 2011, Mahakama Kuu iliamuru Rama apelekwe katika hospitali ya magonjwa ya akili ili apimwe akili kama alikuwa na akili timamu au la, wakati wa tukio hilo.

Amri hiyo ya Mahakama iliyotolewa na Jaji Samuel Karua, ilitokana na maombi yaliyotolewa na Wakili Yusuph Shehe aliyekuwa akiwatetea

Wakili Shehe alidai amefikia uamuzi wa kuwasilisha mahakani hapo ombi hilo kwasababu anataka mahakama ijiridhishe kuwa Mussa alikuwa ana akili timamu kabla ya kuanza usikilizwaji wa kesi hiyo ya mauji Na.26/2010 kulingana na kumbukumbu za maelezo ya ushahidi ulioko mahakamani.

Jana, kabla ya washtakiwa hao kuachiwa, Wakili wa Serikali, Secy Mkonongo aliyekuwa akisaidiana na Clara Charles, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali, kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao.
Hata hivyo Wakili Shehe alidai kuwa mara ya mwisho Mahakama hiyo iliamuru mshtakiwa wa kwanza, Rama, apelekwe katika hopsitali ya magonjwa ya akili kwa ajili ya uchunguzi wa akili zake.
Wakili Shehe alidai kuwa  ripoti hiyo tayari imeshawasilishwa mahakamani hapo kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Akili ya  Isanga tangu Juni 20, 2012, ikiwa imesainiwa na Dk Mndeme Eramus na kwamba inaeleza kwa mshtakiwa wakati akitenda kosa hilo hakuwa na akili timamu.
Kutokana na ripoti hiyo, Wakili Shehe aliiomba mahakama hiyo  ijielekeze katika vifungu cha 220 (4) na 219 (2) vya CPA na kumfutia mashtaka mshtakiwa huyo

Kwa upande wake wakili wa  Serikali Mkonongo alidai kuwa upande wa jamhuri hauna pingamizi na hoja hiyo ya wakili wa washitakiwa.


Jaji Temba alisema kuwa kwa mujibu wa ushahidi ulitolewa mahakamani hapo,mahakama yake inaamini mshitakiwa wa kwanza alitenda kosa la mauji  licha mahakama yake inamuachiria huru mshitakiwa huyo kwasababu ripoti ya daktari imethibitisha kuwa Mussa wakati akitenda kosa hilo alikuwa hana akili timamu.

Jaji Temba alisema kutokana na ripoti ya daktari ambayo imesema wazi Mussa wakati akitenda kosa hilo hakuwa na akili timamu , chini ya kifungu cha 219 (2) CPA, Sura ya 20 kama kilivyorekebishwa mwaka 2002,  mahakama haiwezi kumtia hatiani kwa kosa hilo na badala yake ina muachiria huru.

“Licha mahakama hii inamuachiria huru Mussa kwa kigezo hicho cha ripoti ya daktari ,mahakama hii inatoa amri ya Mussa aendelee kubakia  chini ya uchunguzi wa Watalamu wa magonjwa ya akili na hospitali itakuwa ikitoa taarifa kwa Waziri wa Sheria na Katiba.”, alisema Jaji Temba.

Ramadhan alikamatwa na mlinzi wa Hospiltali ya Muhimbili Furgence Michael akiwa na kichwa cha mtoto huyo kikiwa kimesukwa nywele, April 26, 2008, akidai kuwa alikuwa anampelekea zawadi muuguzi mmoja wa hospitali hiyo.

Kichwa hicho kilikuwa ndani ya mfuko wa nailoni aina ya Rambo huku akikitafuna hadharani huku akidai kuwa alikuwa amezoea kula nyama za watu yeye na bibi yake.
Hata hivyo walimweka chini ya ulinzi mkali, na kutoa taarifa polisi ambapo baada ya polisi kufika walimuhoji akadai kuwa alikuja na bibi yake anayeishi makaburi ya Jeti Lumo na kwa bahati mbaya wamemuacha na wao wamepaa na ungo.
Kabla ya mwili na kichwa chake kupatikana mahali tofautotofauti mtoto Salome alipotea muda wa saa 2 usiku April 25 akiwa nyumbani kwa shangazi yake Furaha Majani (28), anayeishi Segerea kwa Bibi.
Mtoto huyo alifika kwa shangazi yake hapo akiwa na wazazi wake, baba yake Yohana Majani na mama yake Upendo Datsun, wakazi wa Kimara, kwa ajili ya kumtembelea shangazi yake huyo.
Baada ya kubaini kuwa mtoto huyo alikuwa amepotea katika mazingira ya kutatanisha walitoa taarifa kituo cha polisi baada ya kumtafuta kwa ndugu na jamaa bila mafanikio.
Baadaye kiwiliwili cha mtoto huyo kiliokotwa ndani ya shimo la choo cha washtakiwa kikiwa kimekatwa kichwa na wazazi walitambua kuwa ni kiwiliwili cha mtoto wao.
Alidai kuwa baadaye walipata taarifa za Ramadhani kukamatwa Muhimbili akiwa na kichwa cha mtoto, wazazi hao walifika hospitalini hapo  na walikitambua kichwa hicho kuwa ni cha mtoto wao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Mei 25 mwaka 2013.


No comments:

Powered by Blogger.