Header Ads

LWAKATARE AFUTIWA MAKOSA YA UGAIDI





Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemfutia  jumla ya makosa matatu ya tuhuma ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Wilfred Lwakatare  ambaye alikuwa akikabiliwa na jumla ya makosa manne ya tuhuma za ugaidi.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Lawrance Kaduri  jana asubuhi ambapo alisema uamuzi huo unafuatia ombi la mawakili wa Lwakatare peke yake ambao ni Tundu Lissu, Peter Kibatara na Mabare Marando  kuwasilisha  ombi Na.14 /2013  waliliomba mahakama hiyo ipitie mwenendo mzima wa majalada ya kesi Na.37  na 6 za mwaka huu ambazo zipo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),Dk.Eliezer Feleshi alitumia madaraka yake vibaya kinyume cha sheria ya kuifuta kesi na.37 ya mwaka huu.
Pia katika usikilizwaji wa ombi hilo ambalo ulifanyika Aprili 15 mwaka huu, mawakili wa Lwakatare pia walidai DPP alitumia madaraka yake vibaya kwa kuifuta na kufungua kesi upya na kwamba wanaomba mahakama hiyo  itoe amri ya kuifuta kesi ya msingi iliyopo mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayowakabili Lwakatare peke yake  kwa sababu mashitaka anayoshtakiwa nayo hayaonyeshi kama mshitakiwa alikuwa  na nia ya kutenda kosa la ugaidi.

Akitoa uamuzi wake Jaji Kaduri alisema  amekubaliana na hoja ya mawakili wa Lwakatare ya kwamba shitaka la pili,tatu na la nne  hayaonyeshi kama Lwakatare  alikuwa na nia ya kutenda koswa la ugaidi na kwasababu hiyo hati ya mashitaka Lwakatare atabakia akikabiliwa na kosa moja   ambalo ni Kosa la kwanza ambalo linawakabili washitakiwa wote kuwa ni la kula njama kutenda kosa la jinai kinyume na kifungu cha 284  cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 , na kwamba mnamo Desemba 28 mwaka jana, huko Kimara King’ong’o  Stopover, wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kutaka kutumia  sumu kwa lengo la kumdhuru  Denis Msaki  ambaye ni Mhariri wa habari wa Gazeti la Mwananchi ambalo ni kinyume na kifungu cha 227 cha sheria hiyo.

“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama hii inatoa amri ya kumfutia Lwakatare mashitaka matatu yaani kosa la pili, tatu na la nne kwa sababu jamhuri imeshindwa kuonyesha maelezo yanayotesheleza kumshitaki Lwakatare kwa kesi ya ugaidi na hivyo naamuru jalada la kesi ya msingi lilirudishwe mahakama ya Kisutu kwaajili ya mshitakiwa kuendelea kushitakiwa kwa kosa moja la kula njama ambalo linaangukia katika sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002”alisema Jaji Kaduri.

Hata hivyo Jaji Kaduri alitupilia mbali hoja za mawakili wa Lwakatare iliyodai DPP alitumia madaraka yake vibaya ya kufuta kesi na kuifungua upya ambapo alisema anakubaliana na hoja ya mawakili wa serikali  Prudence Rweyongeza na Ponsian Lukosi kuwa uamuzi wa DPP wa kufuta kesi ya Na.37 na kisha kuifungua kesi hiyo kwa mashitaka yale yake ambayo ilipewa Na. zote za mwaka huu,ulikuwa sahihi kisheria na akaamuru washitakiwa warejeshwe rumande.

Itakumbukwa kuwa Aprili 30 mwaka huu, kesi ya msingi inayomkabili Lwakatare katika mahakama ya Kisutu ilikuja kwaajili ya kujatwa na wakili wa Serikali Peter Mahugo alieleza mahakama hiyo kuwa kwa mujibu wa taarifa za jeshi la polisi upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na Hakimu Alocye Katemana aliarisha kesi hiyo hadi Mei 13 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Aprili 15 mwaka huu, wakili Wakili Prudence  Rweyongeza akijibu hoja za mawakili wa Lwakatare mbele ya Jaji Kaduri alikanusha hoja za mawakili wa Lwakatare zilizodai kuwa  DPP alitumia madaraka yake vibaya kuifuta kesi ya Na.37/2013 na akazitaja sababu zilizosababisha DPP aifute kesi hiyo na kufungua kesi mpya iliyopewa Na.6/2013 Machi 20 mwaka huu na mashitaka ni yale yale.

Wakili Rweyongeza aliitaja sababu ya kwanza iliyofanya DPP aifute kesi Na.37 /2013 iliyofunguliwa Machi 18 mwaka huu, ni kwamba uongozi wa mahakama ya Kisutu ulikosea na kuifungua kesi hiyo katika jalada la kesi zinazoendeshwa katika mahakama za chini (Subodnate Court) badala ya kuisajili kesi hiyo katika rejista ya kesi zinazopaswa kusikilizwa na mahakama kuu.

Sababu ya pili ni kwamba hakimu aliyeisikiliza kesi hiyo Emilius Mchauru alikosea kuwaruhusu washitakiwa hao kujibu mashitaka wakati mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi hiyo ya Ugaidi.

‘Kwasababu hizo mbili ndiyo maana DPP-Feleshi Machi 20 , kesi hiyo ilipokuwa inakuja kwaajili ya hakimu Machauru kutoa uamuzi wa ama kuwapatia dhamana au la, DPP akawasilisha hati ya kuifuta kesi na baada ya muda mfupi washitakiwa walikamatwa na kupandishwa kizimbani na kufunguliwa kesi mpya iliyopewa Na. 6/2013 ambayo ilifunguliwa na uongozi wa mahakama ya Kisutu kwa kufuata taratibu zote ,licha mashitaka yalikuwa niyale yale yaliyoyokuwa kwenye kesi iliyofutwa:

“Hivyo basi upande wa jamhuri tunasisitiza kuwa uamuzi wa DPP wakuifuta kesi ile ulikuwa ni uamuzi wa haki ambao ulikidhi matakwa ya kifungu cha  9 cha  Sheria ya Uendeshaji wa Mashitaka ya mwaka 2008”alidai wakili Rweyongeza.

Akipangua hoja ya mawakili wa Lwakatare iliyokuwa ikiiomba Mahakama Kuu iifute kesi ya msingi inayowakabili washitakiwa hao kwasababu kosa la pili,tatu na nne hayaonyeshi nia ya washitakiwa hao kutenda makosa ya ugaidi,alidai kuwa hoja hizo zimeletwa wakati usiyo sahihi kwani kesi ya msingi ipo katika hatua za uchunguzi, upelelezi bado haujakamilika  na kwamba uenda siku za usoni DPP akaamua kubadilisha hati ya mashitaka kwahiyo ombi hilo halina msingi na kwamba hata hivyo Sheria ya Kuzuia Ugaidi  inasema kitendo cha kumteka nyara mtu ni kosa la ugaidi  kwahiyo kinachotakiwa kuzingatiwa katika hilo ni suala la ushahidi tu.

 Awali mawakili wa Lwakatare licha mshitakiwa wa pili  Ludovick Joseph ambaye naye ni Kada wa Chadema, hakuwa na wakili, waliiomba mahakam hiyo itupilie mbali kesi ya msingi inayomkabili Lwakatare kwasababu makosa ya ugaidi yanayomkabili ambayo yameainishwa kwenye hati ya mashitaka,hayaonyeshi nia ya mshitakiwa kutenda kosa la ugaidi.

Pia wakili Lissu alidai kuwa DDP alikuwa na nia ovu na kwamba alitumia madaraka yake vibaya kwa kitendo chake cha kuifuta kesi hiyo na kisha kuifungua upya ambapo inakwenda kinyume na kifungu cha 8 cha Sheria ya Uendeshaji Mashitaka ya mwaka 2008 ambayo kifungu hiki kinamtaka DPP aifute kesi katika mazingira ya kulinda haki, haja ya kuzuia matumizi mabaya ya mfumo wa mahakama, haja ya maslahi ya umma na kudhibiti mshitaka.

Makosa yaliyofutwa ni haya haya hapa, kosa la pili lilikuwa ni la  kula njama  ambalo pia ni kwaajili ya washitakiwa wote  ambalo ni kinyume na kifungu cha 24(2) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi Na.21 ya mwaka 2002, ambapo washitakiwa hao walitenda kosa la ugaidi la  kutaka kumteka Msaki  kinyume na kifungu  cha 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

Shitaka la tatu ni la washitakiwa wote ambapo wanashitakiwa kwa kosa la  kupanga kufanya makosa ya ugaidi  kinyume na kifungu cha 59(a) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi kwamba Desemba 28 mwaka jana,walishiriki katika mkutano wa kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyaraka Msaki  kinyume na kifungu 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi.

Shitaka la nne, Rweyongeza alidai linamkabili Lwakatare peke yake  ni aliwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume na kifungu cha 23(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi , kwamba Desemba 28 mwaka jana, Lwakatale akiwa ni mmiliki nyumba hiyo ilipo Kimaraka King’ong’o  kwa makusudi  aliliruhusu  kufanyika kwa kikao hicho baina yake na Ludovick  cha kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka nyara Msaki.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Mei 9 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.