Header Ads

RUFAA KESI YA JIMBO LA MWIBARA KUSIKILIZWA NA MAJAII WATANO
Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Rufaa nchini, imekubali ombi la mrufani ambaye alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Mwibara kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Chiriko Haruni Davidi iliyoomba rufaa yake isikilizwe na jopo la majaji watano badala ya majaji watatu.

Hoja hiyo ni tafsiri ya kifungu cha 111 cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010, kinachomtaka anayefungua kesi ya uchaguzi kupinga matokeo ya ubunge, kuweka mahakamani dhamana ya kesi aliyoifungua.

Mrufani aliwasilisha ombi hilo kupitia wakili wake Hubert Nyange , siku ya usikilizwaji wa rufaa yake dhidi ya Mbunge wa Mwibara Bunda, Mkoani Mara, Kangi Lugora, wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Uamuzi huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na mahakama hiyo  ambayo ilisema  ilikubaliana na maombi hayo na kusema kuwa sasa hoja hiyo itasikilizwa na jopo la majaji watano, badala ya majaji watatu waliokuwa wamepangwa awali kusikiliza rufaa za msingi.

Mwenyekiti wa jopo la Majaji watano watakaosikiliza hoja hiyo,  January Msoffe, pia aliwataka wajibu rufaa kuwasilisha hoja zao kwa njia ya maandishi ndani ya siku saba , kujibu hoja za mrufani kuhusu hoja hiyo.

Jaji Msoffe  alisema  kuwa  baada ya kupitia hoja za pande zote, watatoa hukumu yao, Mei 31, mwaka huu.
Chiriko  aliyekuwa mgombea wa ubunge katika jimbo hilo mwaka 2010, alikata rufaa katika mahakama hiyo ya juu nchini , kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza iliyompa ushindi Lugora,anatetewa na wakili Melkizedeck Lutema  katika kesi ya uchaguzi aliyoifungua akipinga matokeo yaliyompa ushindi Lugora.

Wakili wa Lugora, Lutema,  na Wakili wa Serikali Mkuu, Obadia Kameya akimwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni mjhibu rufaa katika rufaa ya Chiriko, hawakuwa na pingamizi na hoja hiyo, wakidai kuwa ni vema hopja hiyo iamuriwe na jopo la majaji watano.
Hukumu hiyo iliyokatiwa rufaa na Chiriko pamoja na Lugora, iliyotolewa na Jaji Noel Peter Chocha, Novemba 21, 2011.

Awali rufaa hizo ilipangwa kusikilizwa na jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, lililongozwa na Jaji Edward Rutakangwa, akisaidiana na Jaji Bernard Luanda na Jaji Katherine Oriyo Septemba 26, 2012.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Mei 20 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.