MAHAKAMA YA RUFAA KUMSIKILIZA SHEIKH FARID JUNI 10
Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA
ya Rufani nchini, Juni 10 mwaka huu, inatarajia kuanza kusikiliza ombi lililowasilishwa
na viongozi wa Jumuiya ya Uhamsho na Miadhara iliyokatwa na kiongozi wa
jumuiya hiyo Sheikh Farid Hadi Ahmed na wenzake tisa dhidi
ya Mkurugenzi wa Mashitaka wa Zanzibar.
Ombi hilo
ambalo limepewa Na. 1/2013, Sheikh
Farid na wenzake wanaiomba Mahakama hiyo, itoa amri ya kuifuta rufaa
iliyowasilishwa na DPP, Aprili 15, ya mwaka huu, kwa sababu hadi sasa
hakuna rufaa iliyokuwa imefunguliwa
mahakamani ya kupinga amri ambazo zilitolewa na mahakama.
Kwa mujibu
wa ratiba za vikao vya Mahakama ya Rufani, maombi hayo yanatarajiwa kusikilizwa
na Jopo la Majaji watatu January Msoffe, Salum Massati na William Mandia.
Mbali ya Sheikh Farid, waombaji wengine ni Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Mussa, Azan Khalid, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman, Ghalib Ahmada Juma,Abdallah Said na Fikirini Fikirini.
Sheikh
Farid na wenzake waliwasilisha maombi hayo chini ya hati ya dharura na
wameonyesha tangu Oktoba 25, mwaka 2012 hadi leo wanaishi gerezani na kwamba kama maombi hayo yatacheleshwa kusikilizwa hivyo kama yakicheleweshwa
kusikilizwa yatasababisha waendelee kusota gerezani kwa muda mrefu na hivyo
kuwaletea madhara na usumbufu.
Sheikh Farid anadai taarifa ya kukata rufaa ya DPP haihusiani na uamuzi ulitolewa Machi 11, mwaka 2013 ambao mdaiwa (DPP), anaupinga.
Na kwamba katika maombi ya DPP hayajaambatanishwa na kiapo cha mwapaji ambapo mwapaji ni wakili wa Sheikh Farid , Abdallah Juma Mohammed, ambaye anadai kuwa Oktoba 25, mwaka 2012 waombaji walishitakiwa kwa makosa manne chini ya sheria ya Usalama wa Taifa na Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Wanadai
kuwa , mashitaka dhidi yao walisomewa
mbele ya Msajili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar siku hiyo, lakini hawakupewa
nafasi ya kujibu kwasababu msajili hana mamlaka ya kusikiliza mashitaka hayo.
Wakili Abdallah anadai waombaji waliomba kudhaminiwa mbele ya msajili ambapo Wakili
wa Serikali alipinga maombi hayo kwa
msingi wa kuwa kuna hati ya DPP wa Zanzibar chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa
kwamba usalama wa nchi ungetetereka hivyo mahakama isiwape dhamana.
Wakili huyo anadai Msajili aliwanyima
dhamana wateja wake na kuwaamuru warudi rumande hadi Novemba 8,
mwaka 2012, kesi ilipokuja kwaajili ya utajwa.
Kwa mujibu wa wakili huyo, waombaji hawakuridhika na uamuzi na kuwasilisha
maombi ya marejeo ya uamuzi Mahakama Kuu ya Zanzibar lakini mlalamikiwa
aliwasilisha pingamizi la awali akiomba mahakama itupilie mbali maombi hayo.
Anadai baada ya Jaji Abraham Mwampashi wa Mahakama Kuu kusikiliza maombi ya marejeo na pingamizi la awali la DPP, Machi 11, mwaka huu, alitoa uamuzui wa kutupilia mbali pingamizi na kufuta mwenendo mzima uliokuwa chini ya msajili na uamuzi wa maombi ya dhamana.
Wakili huyo anadai kuwa Machi 12, mwaka huu,DPP aliwasilisha taarifa ya kukata rufani kupinga uamuzi wa Jaji Mwampashi kutupilia mbali pingamizi lake la awali na kuwasilisha sababu za kukata rufani.
Hata hivyo, wakili huyo anadai kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu wa Machi 11, mwaka 2013, hauwezi kupingwa kwa njia ya rufani wala ya marejeo mbele ya Mahakama ya Rufani.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Mei 22 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment