MAHAKAMA YAAMURU ROBERT KISENA WA SIMON GROUP AKAMATWE
Na Happiness
Katabazi
MAHAKAMA ya
Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imetoa amri ya kutaka mshitakiwa wa nne
katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la
UDA,Idd Simba, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group Limited,Robert
Simon Kisena akamatwe na kufikishwa
mahakamani kwaajili ya kuja kukabiliana na kesi inayomkabili.
Amri hiyo
ilitolewa jana na Hakimu Mkuu Mfawidhi
wa mahakama hiyo Elvin Mugeta baada ya kuridhia ombi la wakili wa serikali Awamu
Mbagwa na mawakili wa utetezi Alex Mgongolwa na Romani Lamwai ambao walitaka Kisena ambaye ni
mshitakiwa wa nne katika kesi hiyo akamatwe na akifikishwe mahakamani hapo ili
kesi iweze kuendelea.
Wakili wa
Serikali Mbagwa alianza kwa kuikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo jana
ilikuja kwaajili ya upande wa jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa
lakini upande wa jamhuri hautaweza kuwasomea maelezo hayo kwasababu mshitakiwa
wanne(Kisena),bado hajakamatwa na kwamba hawezi kuwasomea maelezo ya awali
washitakiwa watatu wakati mshitakiwa
wanne hayupo kwani kufanya hivyo ni kusumbua muda wa mahakama .
“Sisi upande
wa jamhuri tulikuwa tayari kwaajili ya kuwasomea maelezo ya awali wa
washitakiwa lakini kwasababu mshitakiwa wa wanne hayupo mahakamani na taarifa
tulizonazo bado hajakamatwa tunashindwa leo (jana)kuwasomea maelezo hayo…hivyo
tunaomba mahakama hii itoe amri ya Kisena akamatwe na haweze kufikishwa
mahakamani ili aje kukabiliana na kesi inayomkabili”alidai wakili Mbagwa.
Kwa upande
wao mawakili wa utetezi Mgongolwa na Masumbuko nao walidai wanaunga mkono hoja
hiyo ya wakili wa jamhuri ya kutaka Kisena akamatwe na kwamba kesi hiyo
iarishwe kwa hairisho la muda mfupi kwani wanaamini serikali inamkono mrefu na
ainayafahamu haya makazi ya Kisena na kwamba
hadi kufikia jana ilikuwa ni siku 25 tangu kesi hiyo ilipofunguliwa upya
mahakamani na Kisena akaunganishwa katika kesi hiyo lakini cha kushangaza hadi
leo Kisena hajakamatwa na kufikishwa mahakamani.
“Kesi hii
ina watesa wateja wetu kwani hadi sasa hawafahamu makosa yanayowakabili kwa
kina, hawapati ajira sehemu nyingine kwasababu ya kesi hii…hivyo na sisi
mawakili wa utetezi tunaunga mkono kuwa Kisena akamatwe aletwe mahakamani ili
kesi hii iweze kuendelea na kwamba Kisena ni mtu anayetafutwa sana na serikali
na hata Aprili 30 mwaka huu, kesi hii ilipofunguliwa rasmi Kisena pia hakuwepo
mahakamani na hivyo hakuweza kusomewa mashitaka yake ambapo siku hiyo kesi hiyo
iliarishwa hadi leo lakini pia leo Kisena hajafika mahakamani”alidai wakili
Masumbuko.
Akitoa amri
ya mahakama, hakimu Mugeta alisema amesikiliza maombi ya mawakili wa pande zote
mbili na kwamba mahakama yake inatoa amri ya Kisena akamatwe na afikishwe
mahakamani na akaiarisha kesi hiyo hadi Juni 4 mwaka huu ambapo Simba na
wenzake wataendelea kuwa nje kwa dhamana.
Aprili 30
mwaka huu, upande wa jamhuri uliifuta kesi ya awali ya matumuzi mabaya ya madaraka iliyokuwa
ikimkabili Simba na wenzake wawili na kisha kufungua kesi mpya yenye mashitaka
sita yakiwemo mashitaka ya rushwa na uhujumu uchumi na kisha kumuunganisha Kisena katika kesi hiyo
ambapo katika kesi ya awali iliyofutwa Kisena alikuwa ni shahidi wa upande wa
jamhuri na hivyo kufanya kesi hiyo ya makosa ya rushwa, uhujumu uchumi kuwa na
jumla ya washitakiwa wa nne hivi sasa.
Ilidai siku hiyo ya Aprili 30 kuwa
washitakiwa wanne na wakili Mwandamizi wa Serikali Oswalid Tibabyekomya wanakabiliwa na makosa ya rushwa,uhujumu
uchumi,matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh.
Bilioni 8.4. Na kwamba Tibabyekomya alieleza kuwa baada ya kuyachambua makosa
hayo wamebaini kuwa yanaangukia katika Sheria ya Uhujumu Uchumi
Mbali na Idd Simba ambaye ni
mshtakiwa wa kwanza na Kisena ambaye ni mshtakiwa wa nne, washtakiwa wengine
katika kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 3 ya mwaka 2013, ni Salimu
Mwaking’inda na Victor Alfred Milanzi.Mwaking’inda, ambaye ni mshtakiwa wa pili
katika kesi hiyo alikuwa Mkurugenzi wa UDA na Milanzi ambaye ni mshtakiwa wa
tatu, alikuwa ni Meneja Mkuu wa UDA.
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka hayo mapya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na walisomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali Awamu Mbagwa. Hata hivyo Kisena hakuwapo mahakamani wakati wenzake wakisomewa mashtaka.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka waliyosomewa jana, shtaka la kwanza la kula njama linawahusu Simba na Milanzi na Kisena.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, jijini Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama za kutenda kosa la vitendo vya rushwa, kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya mashtaka, shtaka la pili la vitendo vya rushwa linamhusu Kisena peke yake, hata hivyo shtaka hilo halikusomwa kutokana na mshtakiwa huyo kutokuwapo mahakamani.
Shtaka la tatu ni la vitendo vya rushwa ambalo linawahusu Simba na Milanzi. Wakili Mbagwa alidai kuwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, walikubali kupokea Sh320 milinoni kutoka kwa Kisena ushawishi wa kuiuzia Simon Group hisa za UDA ambazo zilikuwa bado hazijagawiwa.Katika shtaka la nne ambalo ni la matumizi mabaya ya madaraka, linawahusu Simba , Mwaking’inda na Milanzi.
No comments:
Post a Comment