Header Ads

LWAKATARE AKWAMISHWA TENA


*Korti yuaamuru  Makunga akamatwe

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana iliarisha tena kesi ya kula njama na kutaka kumuua kwa sumu mhariri mtendaji wa Gazeti la Mwananchi Denis Msacky inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.

Hakimu Mkazi Sundi Fimbo alisema anaiarisha kesi hiyo hadi Juni 10 mwaka huu, kwa ajili ya kuja kutajwa na kusema kuwa hawezi kupanga tarehe za mwanzo  kwasababu hata hakimu anayesikiliza kesi hiyo Alocye Katemana ambaye hivi sasa hayupo kazini, akirejea kwanza atatakiwa apate muda wa kuzipitia hoja kuomba dhamana na kupinga dhamana ya washitakiwa hao ambazo ziliwasilishwa mawakili wa pande zote mbele ya Hakimu Fimbo Mei 13 mwaka huu na akaamuru washitakiwa hao warejeshwe gerezani.

Awali jana kabla   ya Hakimu Fimbo kuairisha kesi hiyo wakili Mwandamizi wa Serikali Prudence Rweyongeza alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo  jana ilikuja kwaajili ya kutajwa.

Hata hivyo kwa upande wake wakili wa washitakiwa Peter Kibatara, Profesa Safari  na Nyaronyo Kichere walieleza kuwa wanafahamu kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na kwamba wanaiomba mahakama iwapangie tarehe za karibu.

“Kwa mujibu wa rekodi za mahakama zinaonyesha kesi hii  leo ilikuja kwaajili ya kutajwa na kwamba amesikia ombi la wakili wa utetezi lakini mahakama yake haiwezi kupanga tarehe za karibuni kwasababu hata hakimu Katemana akirejea kazini ,atatakiwa kupata muda wa kuyapitia maombi kuomba dhamana na kupinga dhamana  hivyo anaiarisha hadi Juni 10 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa na ninaamuru mshitakiwa arejeshwe gerezani”alisema Hakimu Fimbo.

Baada ya washitakiwa kutolewa ndani ya chumba cha mahakama na kupitishwa katika korido za mahakama chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza, baadhi ya wafuasi wa Chadema waliokuwa wamevalia sare za chama hicho hicho walikuwa wakisikika wakisema maneno yafuatayo;

“Hii aikubaliki …huu ni mchezo mchafu  unaofanywa na CCM na mahakama kupiga chenga kumpatia dhamana Lwakatare….Kamanda wetu amesota gerezani muda mrefu sana na leo ni mara ya pili tunakuja hapa mahakamani kesi inaarishwa anashindwa kupewa dhamana eti kwa kisingizo cha hakimu anayesikiliza kesi hiyo hayupo…kwani uongozi wa mahakama hauwezi kumpangia hakimu mwingine akampatia dhamana….na hatutaki Televisheni ya TBC imrekodi wakili wa Lwakatare kwasababu TBC inapendelea Serikali;

‘….Mahakama aitendi haki kabisa na tumemsikia Mwigulu Nchemba akimpigia simu Hakimu Katemana akimwelekeza leo hakimu asije mahakamani kumpatia dhamana Kamanda wetu Lwakatare na hata gazeti la Tanzania Daima la leo (jana), limeandika hilo ebu oneni ….”walisikika wafuasi hao wakisema hayo huku wakionyesha watu wengine gazeti hilo la Tanzania Daima la jana.

Hata hivyo Lwakatare aliwapungia mkono wafuasi hao na kuwaeleza neno moja tu ‘Msichoke kupambana’.

 Machi 20 mwaka huu, Lwakatare na wenzake walifunguliwa rasmi kesi Na.6/2013  ya tuhuma za ugaidi ambapo kosa la pili, tatu, na la nne yalikuwa hayana dhamana na hivyo Mei 8 mwaka huu, Jaji Kaduri aliyafuta makosa hayo kwa maelezo kuwa hajaona kama kuna maelezo ya kutosha ya kuwafungulia mashitaka ya aina hiyo washitakiwa hao. Na hivyo kuwabakizia shitaka moja la kula njama ambalo lina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Wakati huo huo  Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Kisutu Waliarwande Lema ametoa hati ya kukamatwa kwa mshitakiwa wa tatu katika kesi ya kuchapisha makala ya uchochezi,aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendai wa Kampuni ya Mwananchi, Theophil Makunga.

Kesi hiyo inayomkabili aliyekuwa Mahariri mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda na mwandishi wa makala hiyo ya uchochezi Samson Mwigamba jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na Kibanda hakuwepo mahakamani kwasababu yupo nchini Afrika Kusini kwaajili ya matibabu na Mwigamba alikuwepo ila Makunga hakuwepo na hakuwa ametoa taarifa za udhuru mahakamani hapo.

Hali iliyosababisha wakili wa serikali Lilian Itemba kuomba mahakama itoe amri ya kukamatwa kwa Makunga, ambapo Hakimu Lema alitoa amri ya kukamatwa kwa Makunga kwasababu ameshindwa kutokea mahakamani jana bila kutoa taarifa na akaiarisha kesi hiyo hadi Juni 20 mwaka huu,itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 28 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.