Header Ads

LWAKATARE AOMBA DHAMANA,DPP APINGA





Na Happiness Katabazi

MAWAKILI wanaomtetea Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare Ludovick Joseph, jana waliwasilisha ombi la kuomba mteja wao apatiwe dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwasababu kosa moja la kula njama linalomkabili hivi sasa linadhamana.

Kosa hilo ambalo ni la kula njama kutenda kosa la jinai kinyume na kifungu cha 284  cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 , na kwamba mnamo Desemba 28 mwaka jana, huko Kimara King’ong’o  Stopover, wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kutaka kutumia  sumu kwa lengo la kumdhuru  Denis Msaki  ambaye ni Mhariri wa habari wa Gazeti la Mwananchi ambalo ni kinyume na kifungu cha 227 cha sheria hiyo.

Wakili Mwandamizi wa Serikali Prudence Rweyongeza alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo ambayo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Alocye Katema jana ilikuja kwaajili ya kutajwa ambapo hata hivyo Hakimu Katemana hakuwepo na badala yake Hakimu Mkazi Sundi Fimbo alimshikia kesi hiyo kwa muda.

Hata hivyo wakili wa Lwakatare, Peter Kibatara alikubali kuwa kweli kesi hiyo ilikuja kwaajili ya kutajwa lakini wao wanawasilisha ombi la kuomba mteja wake apatiwe dhamana kwasababu kosa hilo lina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Wakili wa serikali  Rweyongeza alidai upande wa jamhuri unaomba ombi hilo la mawakili wa utetezi litupwe kwasababu  mahakama haiwezi kutoa dhamana kwa kesi ambayo haipo.

Wakili Rweyongeza alisema kilichopo mahakamani hapo ni jalada la tuhuma zinazowakabili washitakiwa ambazo zipo katika hatua za uchunguzi na kwamba tuhuma hizo mwisho wa siku zitakufunguliwa kesi rasmi Mahakama Kuu kwani Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza hivyo huwezi mahakama haiwezi kutoa dhamana kwa kesi ambayo haipo(Pending Trial).

“Na mahakama ya Rufaa katika uamuzi wake  wa  rufaa iliyokuwa imekatwa na  DPP dhidi ya Ally Nuru Dilie ya mwaka 1988, ilieleza wazi ni wakati washitakiwa wanatakiwa waombe dhamana katika kesi inayowakabili ambayo kesi hiyo inapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu…kesi hiyo inasema wazi mshitakiwa atatakiwa kuomba dhamana pale DPP atakapokuwa amefungua mashitaka rasmi katika mahakama Kuu;

“Na kwa mazingira ya shauri linalomkabili Lwakatare hapa Mahakama ya Kisutu,lipo katika hatua za uchunguzi na  bado DPP hajafungua kesi rasmi Mahakama Kuu, sasa tunashangaa mawakili wa washitakiwa wanawasilisha ombi la dhamana leo hii katika mahakama hii wakati maamuzi hayo ya mahakama ya Rufaa yapo na bado hajatenguliwa?
Rweyongeza aliomba mahakama hiyo itupilie mbali maombi ya mawakili wa utetezi kwasababu hakuna kesi rasmi iliyofunguliwa na DPP mahakama Kuu dhidi ya washitakiwa na kwamba shauri lililopo katika mahakama ya Kisutu lipo katika hatua za uchunguzi.

Baada ya mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha maombi hayo, Hakimu Fimbo alisema amesikia maombi hayo na ayafikisha kwa hakimu anayesikiliza kesi hiyo ambaye ni Katemana ambaye kwa jana hakuwepo ofisini kwasababu alikuwa na udhuru  na kwamba Katemana ndiyo atakayetolea uamuzi kuhusu maombi hayo na akaiarisha kesi hiyo hadi Mei 27 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajawa na akaamuru washitakiwa warejeshwe rumande.
 Baadhi ya watu waliokuwa wamefavalia sare za chama cha Chadema walifika mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo na wengine ambao kabla ya kuanza kwa kesi hiyo walikuwa wakisikika wakisema wamekuja kumlaki Lwakatare kwasababu jana angepata dhamana, matarajio yao hayo yaliyeyuka kwasababu licha ya wakili Kibatara kuwasilisha ombi la dhamana, lakini Hakimu Fimbo alisema hawezi kutoa uamuzi wa maombi hayo kwasababu hakimu anayesikiliza kesi hiyo hayupo.

Mei 8 mwaka huu, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Lawrence Kaduri alitoa uamuzi wake katika ombi lilokuwa limewalishwa kwakwe na Lwakatare liliomba mahakama hiyo ipitie majalada yaliyomfungulia kesi mshitakiwa hayo katika Mahakama ya Kisutu ambapo Jaji Kaduri alitoa uamuzi wa kumfutia jumla ya mashitaka matatu ya tuhuma za ugaidi na kisha kumbakizia shitaka moja la kula njama na akaamuru kesi hiyo ya Na.6/2013 ilirudi Kisutu kwaajili ya hatua zingine.

Machi 20 mwaka huu, Lwakatare na wenzake walifunguliwa rasmi kesi Na.6/2013  ya tuhuma za ugaidi ambapo kosa la pili, tatu, na la nne yalikuwa hayana dhamana na hivyo Mei 8 mwaka huu, Jaji Kaduri aliyafuta makosa hayo kwa maelezo kuwa hajaona kama kuna maelezo ya kutosha ya kuwafungulia mashitaka ya aina hiyo washitakiwa hao. Na hivyo kuwabakizia shitaka moja la kula njama ambalo lina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima, Jumanne Mei 14 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.