PONDA AFUNGWA MWAKA MMOJA
Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya
Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemhukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Sheikh Ponda Issa Ponda aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya uchochezi na wizi wa
malighafi zenye thamani ya Sh.milioni 59 baada ya kumkuta na hatia katika kosa moja la
kuingia kwa jinai katika kiwanja cha Chang’ombe Markazi.
Sambamba na
hilo, mahakama hiyo imewaachiria huru washitakiwa wengine 49 baada ya kuwaona
hawana hatia katika makosa matano yote waliyokuwa wakishitakiwa nao kwasababu
upande wa jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi wa kuishawishi mahakama iwaone
wanahatia na kwamba akasema upelelezi
uliofanywa na jeshi la polisi katika kesi hiyo ni dhahifu na kwamba mahakama
haiwezi kumfunga mtu kwa ushahidi wa hisia tu.
Akisoma
hukumu hiyo kuanzia jana saa 3:36-5:56 asubuhi alisema upande wa jamhuri ulikuwa
ukiwakilishwa na Wakili Mwanadamizi wa Serikali Tumaini Kweka katika kuthibitisha kesi yake walileta jumla
ya mashahidi 16 na upande utetezi uliokuwa ukiwakilishwa na mawakili wa
kujitegemea Nassor Juma, Njama ambapo alisema washitakiwa hao walikuwa
wakikabili na kosa la kula njama, kuingia kwa nguvu, kuzuia kwa nguvu, wizi wa malighafi
zenye thamani ya Sh.milioni 59 na uchohezi ambalo kosa hilo la uchochezi
lilikuwa likimkabili Ponda na mshitakiwa wa tano tu (Mukadamu Abdalah).
Hakimu
Nongwa alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote amebaini kuwa jamhuri
limeshindwa kuthibitisha kosa la kwanza ambalo ni la kula njama kwani kosa hilo
kwa mujibu wa hati ya mashitaka limeshindwa kueleza kuwa washitakiwa hao
walikula njama kutenda kosa gani na kwasababu hiyo kosa la kula njama, kosa la
tano la kula njama kutenda kosa la uchochezi nalo limeshindwa kuthibitika
jamhuri imeshindwa kuleta ushahidi unaonyesha Ponda na Mkadamu walimshawishi
nani kutenda kosa hilo na hivyo anakubaliana na hoja za mawakili wa utetezi
kuwa kosa hilo limeshindwa kuthibitishwa.
Akilichambua
kosa la pili ambalo ni la kuingia kwa jinai katika kiwanja cha Markazi ,hakimu
Nongwa alisema kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa jamhuri unaonyesha
washitakiwa waliingia katika kiwanja ila hawakuweza kuwatambua washitakiwa
hao licha Ponda katika utetezi wake alieleza mahakama
kuwa walianza ujenzi wa msikiti wa muda katika eneo hilo Oktoba 12 mwaka jana
ana alikiri yeye na wenzake ambao hawakutambuliwa mahakamani walishiri kujenga
msikiti wa muda.
“Mahakama
hii imeona Ponda amepatiakana na hatia katika kosa hili la kuingia kwa jinai
katika kiwanja cha Markazi kwani kifungu cha 85 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu
ya mwaka 2002 ,ambayo inasema kuingia kwa jinai ni kwa mshitakiwa aingie kwenye
kiwanja kwa kuhusisha idadi kubwa ya watu, kuingia kwa nguvu au kwa nguvu lakini
kwa ushahidi uliotelewa umethibitisha Ponda aliingia katika kiwanja hicho na
kwasababu hiyo mahakama hii inamuona ana hatia katika kosa hilo la pili la
kuingia kwa jinai Ponda peke yake”alisema Hakimu Nongwa.
Kuhusu kosa la kuzuia kwa nguvu , hakimu alisema pia
jamhuri imeshindwa kulithibitisha na kwamba hakuna ushahidi unaonyesha
washitakiwa walionza kujenga msikiti ule wa muda Oktoba 12 ndiyo walewale waliokamatwa Oktoba 14 mwaka
jana nakwamba hakuna ushahidi unaonyesha
ujenzi wa msikiti ule wa muda ulileta hali ya uvunjifu wa amani na kwamba Ponda
na hao wenzake ambao hawajatambuliwa walitumia malighafi za kampuni ya Agritanza
kujengea msikiti ule.
Hakimu
Nongwa kuhusu kosa la wizi ,pia upande wa jamhuri umeshindwa kulithibitisha kwamba
msikiti ule wa muda ulijengwa na malighafi za kampuni ya Agritanza na kwamba
hakuna ushahidi ulioletwa ukaonyesha malighafi za ujenzi wanazotuhumiwa
washitakiwa kujengea msikiti wa muda katika kiwanja cha Markas za kampuni ya
Agritanza zilikuwa na thamani ya Sh.milioni 59 na kwamba hakuna ushahidi
ulioletwa unaonyesha msikiti wa muda ulijengwa kwa malighafi za kampuni ya
Agritanza.
“Mahakama
hii imeona ushahidi ulioletwa na upande wa jamhuri ambao upelelezi ulifanywa na
jeshi la polisi ni dhahifu na ndiyo maana mahakama yake imewachiria huru
washitakiwa 49 katika makosa manne yaliyokuwa yakiwakabiri kwasababu
yameshindwa kuthibitishwa na ninawashauri mawakili wa serikali muwe makini
katika uandaaji wa hati zenu za mashitaka”alisema Hakimu Nongwa.
Wakili Kweka
aliomba mahakama itoe adhabu kali kwa Ponda ili iwe fundisho kwa wengine. Kwa
upande wa wakili wa Ponda, Njama aliomba mahakama impatie mteja wake adhabu
ndogo kwani hiyo ni mara yake ya kwanza kukutwa na hatia na kwamba amekaa
gerezani muda mrefu toka Oktoba 18 mwaka jana hadi jana kwani Mkurugenzi wa
Mashitaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi alimfungia dhamana Ponda na Mukadamu.
Hakimu
Nongwa baada ya kusikiliza hoja za mawakili hao
alisema mshitakiwa anayepatikana na hatia katika kosa hilo la kuingia
kwa jinai kwa mujibu wa kifungu cha 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka
2002 , mtu huyo atatakiwa afungwe jela miaka miwili, au faini au vyote viwili.
“Lakini kwa
mazingira ya kesi hii mahakama hii imeamua kutumia kifungu cha 25(g) cha Sheria
ya Kanuni ya Adhabu na kwamba mahakama
hii imeona Ponda amekaa gerezani muda mrefu na kwamba ni mara yake ya kwanza
kutiwa hatiani hivyo mahakama yake
inamfunga kifungo cha nje cha mwaka mmoja, awe ni mtunza amani na mwenye tabia
nje kwa kipindi chote hicho.
Hata hivyo
hakimu Nongwa alisema inawezekana Ponda alitenda kosa hilo kwa nia njema,ila
Ponda alivunja sheria katika kudai haki yake hivyo na kwamba Ponda akumbuke
hakuna aliyejua ya sheria akaamuru askari wampeleke Ponda kujaza fomu za
masharti hayo ya kuakisha atakuwa ni mtunza amani na mwenye tabia njema, ambapo
Ponda alikwenda kujaza fomu hizo na kisha kuachiliwa huru.
Baada ya
Ponda kuachiliwa huru wafuasi wake waliokuwa wametanda nje ya uzio wa mahakama
hiyo na ndani, walilipuka kwa shangwe.Hata hivyo ulinzi ulikuwa umeimalishwa kwa
farasi ,mbwa lakini hata hivyo hakuwepo na uvunjifu wowote wa amani.
Akizungumza
na waandishi wa Habari Ponda alisema kilichofikiwa na mahakama ni haki yake na
pia alikuwa na haki ya kuwa nje na pia imeonyesha jinsi vyombo vya dola
vinavyoweza kupambikizia watu kesi na kwamba anapata fursa ya kushiriki katika
masuala ya kijamii.
Oktoba 18
mwaka jana, ndiyo walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na
makosa hayo matano.
Chanzo:Gazeti la
Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 10 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment