Header Ads

JELA MIAKA MITATU KWA KOSA LA KUUA BILA KUKUSUDIANa Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemhukumu kwenda jela miaka mitatu Anderson  Raphael, baada ya  mshitakiwa huyo kukiri kosa la kumuua bila kukusudia marehemu  Francisco Severine Makupa.

Hukumu hiyo ilitolewa jana asubuhi na Jaji John Utawama muda mfupi baada ya mshitakiwa huyo kikiri kosa la kuua bila kukusudia muda mfupi baada ya kusomewa maelezo ya kesi na wakili wa serikali Nassor Katuga ambapo jana kesi yake ilikuja kwaajili ya kumsomea shitaka linalomkabili na mshitakiwa huyo akaamua kukiri kosa.

Wakili Katuga alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 19 mwaka 2010 huko Bagamoyo, ambapo siku ya tukio mshitakiwa na marehemu walikuwa wamekaa pamoja tangu asubuhi hadi saa tisa wakinywa pombe za kienyeji na ilipofika muda huo wa saa tisa, marehemu alimkataza mshitakiwa asile ugali na ndipo ugomvi wa kugombea ugali ulipoanza na hivyo kusabababisha marehemu kupoteza maisha yake.

Jaji Utamwa alisema kabla mahakama yake haijatoa adhabu, mahakama yake imezingatia yafuatayo kuwa ni kweli mshitakiwa hakutaka kuisumbua mahakama wala kupoteza muda wa mahakama kuendesha kesi hiyo, ni kweli mshitakiwa na marehemu walikuwa ni marafiki,na kosa hilo lilitenda katika mazingira ulevi na sababu ya ovyo ovyo ya kugombea ugali.

“Ni kweli mshitakiwa ameishakaa gerezani muda mrefu kwa takribani miaka mitatu ,ni kijana ambaye taifa linamtegemea na hoja hizo zimeifanya mahakama iwe na mkono wa huruma lakini pia mahakama imeona katika kosa hili kuna mtanzania amepoteza maisha yake kwa sababu ya mshitakiwa kujichukulia sheria mkononi kwa kumpiga  na kwamba maisha ya mtu hayapaswi kukatishwa na binadamu mwenzie kwa njia ya kujichukulia sheria mkononi na hivyo mahakama hii inamhukumu kwenda jela miaka mitatu ili iwe funzo kwa wananchi wengine wanaopenda kushiriki vitendo vya kupigana pigana”alisema Jaji Utamwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 17 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.