Header Ads

BRELA YAMKAANGA MARANDA

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa kwanza katika kesi ya wizi ya bilioni 1.8 wa Fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) kupitia Benki Kuu (BoT), Afisa Mtendaji Mkuu wa (BRELA) Esteriano Mahingila, ameikana kampuni ya Kiloloma&Brothers inadaiwa kuchota kiasi hicho cha fedha kuwa haijawahi kusajiliwa na ofisi yake.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 1163 ya mwaka jana Farijara Hussein na kada wa CCM, Rajab Shaban Maranda , ambao kwa mujibu wa jarada la kampuni ya Kiloloma&Brothers wao ni wakurugenzi ambao pia wanaruhusiwa kuchukua fedha kwenye akaunti ya kampuni hiyo ambayo inadaiwa kuwa bandia .

Mahingira ambaye alikuwa akiongozwa na Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface aliambia mahakama kwamba ofisi yake inaitambua kampuni iitwayo Kiloloma Bros enterprises ambayo Mkurugenzi wake alikuwa akiitwa Charles Isaack Kissa kabla ya mkurugenzi huyo kubadilisha jina na kuitwa Chares Isaack Kissa.

Alisema kwa mujibu wa jalada kampuni ya Kiloloma Bros Enterprises ambayo BRELA inalo, namba yake ya usajili ni 151025 na ilitolewa na ofisi yake April 4 mwaka 2005.

Alibainisha kuwa ofisi hiyo ilionyesha kuwa ingefanya biashara ya kuuza vifaa vya maofisini (stestionaries) na ofisi hiyo ipo nyumba namba 7 mtaa wa Iramba Magomeni jijini.

Katika jalada linaloonyesha kampuni ya Kililoma&Brothers lilitolewa mahakamani hapo na wakili wa serikali Boniface, linaonyesha kwamba namba ya usajili wa kampuni hiyo inafanana na namba ya usajili ya Kiloloma Bros Enterprises, tarehe na anwani ya kampuni hiyo ya Kilolomo Bros pia zinafanana na Kilolomo&Brothers .

Maelezo hayo ambayo yalikuwa yakisomwa na Boniface yalisababisha wananchi walikuwa wakifuatilia kesi hiyo ambayo jana ilianza kusikilizwa kwa mara ya kwanza kushikwa na butwaa.

Katika kesi hiyo inaongozwa na jopo mahakimu wakazi Naibu Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi,Cypriana William akisaidiana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ,Phocus Bambikya pamoja na Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Saul Kinemela.

Mahingira aliieleza mahakama kuwa licha ya tarehe, namba za usajili, ofisi za kampuni hiyo kufanana katika hati mbili za usajili wa kampuni hiyo Brella haijawahi kuisajili kampuni ya Kiloloma&Brothers ambayo ndiyo inayodaiwa mahakamani hapo kuchota sh 1,864,949,294.45 mali ya BOT.

“Kwa kifupi Kiloloma&Brothers ofisi yangu haijawahi kuisajili na wala haipo kwenye orodha ya makampuni ambayo tumewahi kuyasajili, hatuwezi kutoa namba moja ya usajili wa kampuni mbili” alisema Mahingira

Aliongeza kuwa kutoa namba mbili ni kosa la jinai chini ya Sheria ya Sheria za Biashara Na.25 ya mwaka 1975”

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili Kiongozi wa Serikali Boniface na Shaidi:

Wakili: Ieleze mahakama shughuli yako kubwa pale BRELA ni nini?

Shahidi:Kusimamia shughuli za utawala, pia kushughulika na uchambuzi na kukubali au kukataa maombi ya kuanzisha kampuni na kuweka saini kwenye hati ya kampuni zinazoanzishwa.

Wakili:Usajili wa makampuni unaanzaje?

Shahidi:Mwombaji anaza kujaza fomu ya kusajili jina la kampuni na fomu hiyo inaonyesha anwani ya makazi,jina la biashara anayotaka kuifanya,majina au jina la mmiliki wa kampuni hiyo, uraia wa mwombaji, na katika fomu hiyo kuna kipengele kinachoonyesha kama mwombaji huyo alishawahi kusajili kampuni kwa jina kama hilo na tarehe ya kuaza biashara.

Wakili:Akishajaza hiyo fomu nini kinafuata?

Shahidi:Mwombaji anapaswa kuileta ofisini kwetu na atamkabidhi ofisi ya msajili ambayo atamweleza kiasi cha malipo kisha anaenda kulipa kwa mhasibu.

Wakili:Kisha mhasibu anafanyaje?

Shahidi:Mhasibu anagonga mhuri unaoonyesha terehe ya kulipiwa hiyo fomu kisha anampatia risiti.

Wakili:Mahakama inataka kufahamu Kiloloma Bros kama unaifahamu?

Shahidi:Naifahamu

Wakili:Lini ulianza kuifahamu?

Shahidi:Kwakweli nilianza kuifahamu pale tatizo la EPA liliposhika kasi kwamba kampuni hiyo ilishiriki kuchota fedha za EPA.

Wakili:Huna namna nyingine ya kuitambua kampuni hiyo?

Shahidi:Kwakweli sina namna nyingine ninayoitambua kwani pale ofisini makampuni ni mengi.

Wakili:Unalitambua jalada ya kampuni ya Kiloloma Bros?

Shahidi:Ndiyo nalitambua vyema kwani lina saini yangu ikiwemo namba ya usajili ya kampuni namba 151025 na nyaraka zingine zilizopo ndani ya jalada hili zina saini yangu na itoshe kusema kwamba kampuni hii ilisajiliwa kihalali na kampuni yangu.

Wakili:Soma kwa nguvu kwa sauti, kichwa cha habari kwenye hilo jarada kimeandikwaje?

Shahidi:Registor Of Bussines Name.

Wakili:Ungependa kulitoa jalada hilo lipokelewe na mahakama hii kama kidhibiti?

Shahidi:Ndiyo.

Jopo lilipokelewa kama kidhibiti namba moja.

Wakili:Jina la Biashara linaitwaje?

Shahidi:Kiloloma Bros.

Wakili:Nini kazi ya kampuni hiyo?

Shahidi:Office Equipment and Stationers.

Wakili:Nani hasa alikuwa mwombaji wa kusajiliwa kampuni hiyo?

Shahidi:Chalres Isaack Kissa kabla ya kubadilisha jina na kuitwa Chares Isack Kissa.

Wakili:Alikuwa ni raia wa Tanzania?

Shahidi:Ndiyo.

Wakili:Alilipa shilingi ngapi kama ada ya usajili?

Shahidi:Elfu sita.

Wakili:Katika maombi yake alionyesha biashara yake hiyo ataifanyia wapi?

Shahidi:Nyumba namba 7, Magomeni Mtaa wa Iramba.

Wakili:Hati ya Usajili namba 151025 ilitolewa na nani?

Shahidi:Mimi.

Wakili:Search report ilikuja lini ofisini kwenu?

Shahidi:Januari 11 mwaka 2008, kuna mtu alikuja pale ofisini na kutaka ufanyike upekuzi wa kampuni ya Kiloloma Bros na hati hiyo inaonyesha hakuna jina linalofanana na kampuni hiyo.

Wakili:Katika kambukumbu zako , kuna mabadiliko yaliyoombwa au kutolewa na kampuni hiyo?

Shahidi:Hakuna ombi la kufanyika kwa mabadiliko kupokelewa au kukataliwa na BRELA.

Wakili:Kuna jina la Biashara linaitwa Kiloloma&Brother Enterprises unaifahamu?

Shahidi:Si ifahamu.

Wakili:Hiyo Namba ya hati ya usajili 151025 iliyotolewa April 14 mwaka 2005, hiyo hati imesainiwa na nani?

Shahidi:Saini hii inataka kufanana na yangu lakini siyo yangu.

Wakili:Nani wanaonyesha ni wamiliki wa kampuni hiyo?

Shahidi:Ni Farijara Hussein na Rajab Shaban Maranda ndiyo wamilimiki wa Kiloloma &Brother Entreprises.

Wakili:Inaonyesha biashara wanafanyia wapi?

Shahidi:Nyumba namba 7 Mtaa wa Iramba-Magomeni.

Wakili:Nani wanaonyesha ni wamiliki ya akaunti ya Kiloloma &Brothers Enterprises?

Shahidi:Farija na Maranda.

Wakili:Angalia kwa makini hayo majalada ya makampuni hayo mawili yanaonyesha yamesajiliwa siku na terehe tofauti?

Shahidi:Inaonyesha zimesajiliwa siku na tarehe moja.
Wakili:Katika taratibu za ofisi yenu mnaweza kusajili makampuni mawili kwa namba moja?

Shahidi:Hairuhusiwi hata kidogo.

Wakili:Angalia kidhibiti namba namba moja na kidhibiti namba mbili(majarada) yanaonyesha sehemu gani ofisi hizo zilipo?

Wakili:Inaonyesha pia kampuni ya Kilolomo&Brother inafanya shughuli zake katika nyumba namba 7 mtaa wa Iramba –Magomeni.

Baada ya wakili wa serikali kumaliza kumhoji shahidi, hakimu William alimtaka wakili wa utetezi Majura Magafu aanze kumuuliza maswali shahidi huyo, lakini hata hivyo Magafu alionyesha kushitushwa na hali hiyo na kusema kwamba hawezi kuuliza maswali kwa wakati huo hadi azungumze na wateja wake na kuomba shauri hilo liahirishwe kwa muda ili aweze kuzungumza na wateja wake.

Ombi ambalo lilikubaliwa na jopo hilo ambapo ilipofika saa 6:15 lilirejea mahakamani hapo na Magafu kuanza kumuuliza maswali shahidi huyo ambapo hata hivyo shahidi huyo alikuwa akiyapangua maswali Magafu kwa umakini na kujiamini.

Jopo hilo liliarisha kesi hiyo hadi leo ambapo shahidi wa pili ataanza kutoa ushaidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 28 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.