Header Ads

SERIKALI YACHARUKA VIGOGO BOT KORTINI

MINARA PACHA

.Ni Liyumba na mwenzake Deogratius Kweka
.Wadaiwa kusababisha hasara ya bilioni 221/-
.Wakosa dhamana, wapelekwa rumande Keko
.Ulinzi mkali, makachero watanda Kisutu Dar

Na Happiness Katabazi

KWA mara nyingine, Serikali imeonyesha makucha yake kwa watumishi wa umma wanaotuhumiwa kutumia vibaya madaraka yao hivyo kuisababishia hasara ya mabilioni ya fedha.

Katika hatua hiyo, Serikali jana iliwafikisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba na Meneja Mradi wa benki hiyo, Deogratius Kweka.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kutumia vibaya fedha za umma kwa kuidhinisha ujenzi wa minara Pacha ya BoT maarufu kama ‘Twin Tower’.

Liyumba ambaye amestaafu kazi ya utumishi wa umma pamoja na mwenzake wamefunguliwa kesi hiyo ya jinai Na. 27 ya mwaka huu.

Wakili Kiongozi wa Serikali, John Wabuhanga aliyesaidiana na wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda na Tabu Mzee kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Hadija Msongo, kwamba watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu.

Wakili Wabuhanga alidai kwamba shitaka la kwanza linamkabili mshitakiwa wa kwanza ambalo ni matumizi mabaya ya ofisi ya umma kwamba kati ya mwaka 2001-2006 akiwa mwajiri wa serikali aliidhinisha ujenzi wa minara pacha bila baraka za uongozi wa juu wa benki hiyo.

Shitaka la pili, ambako alisema pia linamkabili mshitakiwa wa kwanza peke yake ambalo ni kuidhinisha malipo ya ujenzi huo bila kibali cha Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Wabuhanga alidai kuwa shitaka la tatu ni kuisababishia serikali hasara ambalo shitaka hilo linawakabili washtakiwa wote, akidai kwamba kati ya mwaka 2001-2006, wakiwa ni watumishi wa umma, kwa makusudi au kwa kushindwa kuwa makini na kazi yao waliisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Hata hivyo washtakiwa wote ambao muda wote walikuwa wakijifuta jasho wakati wapo kizimbani walikana mashtaka hayo.

Akitoa masharti ya dhamana hakimu Msongo alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima kila mmoja awe na wadhamini wa wawili wa kuaminika ambao watasaini bondi au kuwasilisha hati yenye thamani ya nusu ya kiasi wanachotuhumiwa kuisababishia serikali hasara.

Sharti jingine ni washtakiwa kuacha hati za kusafiria mahakamani na kila Ijumaa watahitajika kuripoti ofisi za Takukuru na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ya kibari cha korti.

Nusu ya kiwango wanachodaiwa kuisababishia serikali ni sh bilioni 110 hivyo kila mmoja wao atapaswa kusaini bondi au kuwasilisha hati yenye thamani ya sh bilioni 50.

Sekunde chache baada ya hakimu Msongo kutoa masharti hayo ndugu na jamaa wa washtakiwa hao waliokuwa wameketi viti vya nyuma kufuatilia shauri hilo, walitoka kwenye viti hivyo kimya kimya na kwenda kwenye benchi walilokuwa wameketi mawakili wa utetezi na kuwakabidhi hati za mali kama njugu ili zitumike kuwadhamini washitakiwa.

Mawakili wa utetezi Alexander Kyaruzi na Osca Msechu waliomba mahakama hiyo wateja wao kudhaminiwa kwa hati za nyumba zenye zaidi ya thamani ya sh milioni 600 na kuongeza hati hizo wamekuja nazo mahakamani hapo.

Kutokana na hali hiyo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda, alisimama haraka na kuiomba mahakama kutokubali ombi hilo kwa sababu upande serikali unahitaji kupata muda wa kukagua kwa umakini vielelezo hivyo kama ni za kweli au la.

“Mheshimiwa hakimu tunaomba hati hizo zisitumike leo kuwadhamini washtakiwa kwani sisi upande wa serikali tunaitaji kupata muda wa kuzipitia kwa kina hati hizo zinataka kutumika kuwadhamini washtakiwa ili tujue ni za kweli au la,” alisema Manyanda.

Hakimu Msongo, alikubalina na ombi la Manyanda na kutoa amri kwamba washtakiwa kwenda rumande huku wakisubiri upande wa serikali ukamilishe kazi ya kuzikagua hati hizo.

Hakimu huyo aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 10, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa kwa mara ya pili.

Awali, watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo saa nne asubuhi na maofisa wa Takukuru, kabla ya kupanda kizimbani saa nane mchana katika ukumbi namba mbili wa korti hiyo huku wote wawili wakiwa wamebeba maji ya kunywa aina ya Kilimanjaro.

Kwa wakati wote wakiwa wameketi kwenye gari hilo nje ya mahakama kabla ya kupanda kizimbani, makachero wa Takukuru walikuwa wameimarisha ulinzi mkali katika eneo ambalo gari hilo limeegeshwa.

Tanzania Daima Jumatano, lililokuwepo mahakamani hapo hadi saa tisa na nusu alasiri, liliwashuhudia watuhumiwa hao wakipelekwa katika Mahabusu ya Keko, chini ya ulinzi mkali wa makachero wa polisi na Takukuru.

Kufikishwa kwa watuhumiwa hawa jana mahakamani kuna kumetokana kwa kelele nyingi zilizopigwa na makundi mbalimbali ya wananchi vikiwemo vyama vya upinzani vilivyoongozwa na Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk.Willbroad Slaa na vyombo vya habari kwamba ujenzi wa minara hiyo una wingi la ufisadi kwani gharama zilizotumika kujenga ni kubwa ikingalishwa na gharama halisi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi wa Benki Kuu ya mwaka 2005, zilionyesha kwamba ujenzi wa Benki hiyo utagharimu sh bilioni 500.

Hii ni mara nyingine kwa vigogo wanaotuhumiwa kutumia vibaya madaraka kufikishwa kortini kwani mwishoni mwa mwaka jana, Serikali iliwafikisha mahakamani waliokuwa Mawaziri waandamizi wa awamu ya tatu ya uongozi wa nchi hii, Basil Mramba (Fedha) na Daniel Yona (Nishati na Madini) pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja kwa kuisababishia Serikali hasara sh bilioni 11.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 28 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.