Header Ads

WASHTAKIWA EPA WABADILISHIWA MASHTAKA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa serikali katika kesi ya wizi wa sh bilioni 3.8 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jana ulibadilisha hati ya mashtaka katika kesi hiyo na kumuongeza mshitakiwa mmoja.

Mbele ya Hakimu Waliwande Lema, Wakili wa Serikali, Mganga Biswalo, alidai hati hiyo ina mashtaka sita na kumuunganisha Mtanzania mwenye asili ya Kiasia, Aya Somai, kuwa mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ambao walikuwapo tangu awali ni Farijara Hussein, Rajabu Shaaban Maranda, ambaye ni kada wa CCM, Iman Mwakosya, Anna Komu na Sophia Joseph, ambao ni maofisa wa BoT.

Akiwasomea mashitaka hayo, Biswalo alidai kati ya mwaka 2002-2005, walikula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongozo BoT wakionyesha kuwa Kampuni ya Mibale Farm imepewa idhini na kampuni ya India kudai deni la sh 3,868,805,737.13.

Washtakiwa wote walikana tuhuma hizo na Hakimu Lema aliamuru mshtakiwa Somai kupelekwa rumande hadi Januari 26 mwaka huu, ili aweze kupata fursa ya kupitia masharti ya dhamana yaliyotolewa wakati kesi hiyo ilipofunguliwa Novemba 4 mwaka jana. Washitakiwa wengine wapo nje kwa dhamana.

Wakati huo huo, upande wa serikali katika kesi namba 1158 ya mwaka jana ya wizi sh bilioni 1.186 mali ya BoT, inayomkabili Bahati Mahenge na wenzake wanne umebadilisha hati ya mashtaka na kuieleza mahakama kwamba upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Mbali na Mahenge, washtakiwa wengine ni Manase Makale, Davis Kamungu, Godfrey Mosha na Edda Makale.

Katika kesi hiyo, washitakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka tisa likiwemo shitaka la kula njama, kughushi, wizi, kuwasilisha nyaraka za uongo na kwamba katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2003-2005, walighushi hati zilizoonyesha Kampuni ya Marubeni ya India imetoa idhini kwa Kampuni ya Changanyikeni Residential Complex ambayo mkurugenzi wake ni Samson Mapunda ambaye jina lake halipo imepewa idhini ya kurithi deni hilo.

Kesi imeahirishwa hadi Februari 9 mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Januari 23 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.