Header Ads

JAJI WARIOBA:SERIKALI INATAFUTA MCHAWI ANAYEJULIKA

Na Happiness Katabazi

“HIVI nina kosa gani hadi taarifa hizi zinazagaa kwamba nitakamatwa? Ninaamini taarifa hizi hazisambazwi na watu wasio na mamlaka, ni watu wenye mamlaka kwenye taasisi za serikali ndio wamekuwa wakisambaza taarifa hizi, sasa ziwe za kweli au za uongo, nasema hivi, nimechoka na siogopi, hata leo wanaotaka kuja kunikamata waje haraka.”

Hayo ni maneno ya Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo vya habari vitatu, aliouitisha kwa lengo la kueleza jinsi alivyoshiriki kuanzisha Kampuni ya Mwananchi Gold Ltd, Jumanne wiki iliyopita, ofisini kwake Masaki, Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, Jaji Warioba alieleza pia madhumuni ya kuanzishwa kwa kampuni hiyo na jinsi anavyoishangaa serikali jinsi inavyoipiga teke wakati ndiyo iliyoianzisha.

Alisema uamuzi wa kuitisha mkutano huo ulikuwa wa lazima kwake baada ya kusambaa za taarifa kuwa ni mmoja wa viongozi wastaafu watakao fikishwa mahakamani kwa makosa ya ufisadi, akihusishwa na kutafuna fedha za Mwananchi Gold Company Ltd.

Alitumia mkutano huo kunanusha kuhusika na vitendo vya ufisadi na kueleza kuwa taarifa ambazo zimekuwa zikienezwa kwa kasi kuwa ataburuzwa mahakamani wakati wowote kwa tuhuma za kutafuna fedha za Mwananchi Gold Company Ltd zinamkera na zimemchosha.

“Nimewaita, lengo la kuwaita katika mkutano huu ni kuwaeleza kwa mapana, Mwananchi Gold Company Ltd ilianzishwa na nani na kwa madhumuni gani.

Hii ni kwa sababu kampuni hii imekuwa ikitizamwa vibaya na wananchi wakati ilianzishwa kwa ridhaa ya serikali.

“Watanzania wengi wanaitizama kampuni hii kama ya kifisadi wakati ukweli ni kwamba uamuzi wa kuanzishwa kwake ulikuwa wa serikali ambayo ilikuwa ikitekeleza sera yake ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kusafisha dhahabu zao hapa nchini na kuziuza kwa bei halali.
“Ninasikitika kumekuwa na maneno mengi ya kupotosha kuhusu uanzishwaji wa kampuni hii na uamuzi wa serikali kulikalia kimya suala hili pasipo kueleza ukweli wote kuhusu kuanzishwa na madhumuni ya kuanzishwa kwake.

“Kampuni ya uwakili ya Nyalali, Warioba & Mahalu, Law Associates, ambayo mimi ni mmoja wa mawakili wanaoimiliki, iliombwa na serikali kutoa huduma ya kisheria kusaidia kuundwa kwa kampuni hiyo.

“Ilifanya kazi hiyo kama ilivyoombwa na serikali na kuiwezesha kununua kiwanja cha ekari 30, kilichopo kitalu No. 150-164 Vingunguti eneo la Viwanda, Dar es Salaam, ambako kulifungwa mashine za kusafishia madini na ilizinduliwa rasmi na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Desemba 1, 2005.“Kiwanda hicho, mali ya Mwananchi Gold Company Ltd, kimejengwa kwa kodi za Watanzania na kimefungwa mitambo ya kisasa ikiwemo maabara. Kina uwezo wa kusafisha kg 200 katika muda wa saa nane kwa siku,” alieleza Jaji Warioba.

Jaji Warioba ambaye muda wote wa mkutano huo alikuwa akizungumza taratibu huku mara kadhaa akiinama mezani kwake kukagua vielelezo vyake, alisema kiwanda hicho kilianza kufanya kazi kwa kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo wa wilayani Geita, lakini baadaye alishangazwa na uamuzi wa serikali wa kukataa kuuendeleza mradi huo uliokuwa na tija kwa taifa.

”Mradi uliokuwa ukiendeshwa na kampuni hiyo, ungeisaidia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhifadhi dhahabu hapa nchini, na pia ungeisaidia serikali kujua kiasi cha dhahabu kinachopatikana nchini kuliko ilivyo hivi sasa, dhahabu inachimbwa na kusafirishwa nje ya nchi kwenda kusafishwa.

Inasikitisha kwa sababu kupeleka dhahabu nje ya nchi, kunalifanya taifa lisijue kiasi kinachochimbwa na mchimbaji.

“Serikali imeamua kuipa kisogo Mwananchi Gold Company Ltd bila kujali kuwa uamuzi wa kuianzisha ulikuwa wake kwa nia njema.

Ni serikali iliyoamuru BoT, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Kampuni ya MA-CE ya Italia kuunda kampuni hiyo. Baada ya uamuzi huo, serikali ilikuja kwenye ofisi yetu ya uwakili ya Nyalali, Warioba & Mahalu Law Associates ili tuisaidie kuipatia huduma ya kisheria kabla na baada ya kuundwa kwa Mwananchi Gold Co. Ltd.

“Sasa nashangaa tunakwenda kusafisha dhahabu nje ya nchi wakati kiwanda cha kisasa cha kusafishia madini yote kipo pale Vingunguti, tena kilianzishwa kwa uamuzi wa serikali. Lakini maajabu ni kwamba kwa sababu za kisiasa tu kampuni hii inapigwa vita usiku na mchana, wanaharibu mradi huu kwa mambo ya kisiasa tu, kisha wanaanza kutafuta mchawi wakati mchawi ni wao.“Nasisitiza Mwananchi Gold Company Ltd ni mradi wa serikali na serikali ndiyo ilikuja kwenye ofisi yetu kutuomba tuisaidie huduma ya kisheria ya kuanzisha kampuni hiyo, ikairuhusu BoT kuingia kwenye biashara hiyo kwa sababu taasisi hiyo ina fedha.
“Lakini sasa serikali imeishinikiza BoT ijitoe katika mradi huo na wiki tatu zilizopita, BoT iliwasilisha rasmi kwenye bodi ya wakurugenzi wa Kampuni hiyo ya Mwananchi kwamba imejitoa na hivyo sasa imebaki NDC peke yake,” alisema Jaji Warioba kwa masikitiko.Akizungumzia dhamira ya serikali ya awamu ya tatu kuanzisha mradi huo, alisema ilitokana na sera ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo ambayo awali ilipokwama, iliamua kuanzisha kampuni ya Meremeta ambayo ilishindwa kusaidia, ndipo baadaye ikaamua kuanzisha Kampuni Mwananchi Gold Ltd.
Jaji Warioba alieleza kuwa kwa mujibu wa makubaliano ya awali yalitotiwa saini na pande zote tatu, Julai 2002 na aliyekuwa gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali, na aliyekuwa mkurugenzi wa NDC, Kanali Joseph Simbakalia, unaonyesha majukumu yanayopaswa kufanywa na wamiliki wa kampuni hiyo.
Kwamba MA-CE ambayo ni kampuni ya Kiitaliano, iliapaswa kusimamia teknolojia, kuleta mashine, kujenga miundo mbinu ya viwanda, kuzalisha na kutafuta soko la dhahabu pindi inaposafishwa.
Wakati NDC na BoT kwa mujibu wa makubaliano hayo ambayo walipaswa kushughulikia masuala yanayohusiana na manunuzi, kupata baraka zote za serikali za kuingia ubia katika miradi mbalimbali na kutoa msamaha wa EPZ kwa miradi iliyoingiwa.
“Ndani ya Mwananchi Gold Company Ltd kuna kampuni mwamvuli inaitwa Mwananchi Trust Company hivyo ndani ya Mwananchi Trust Company ndiyo kuna vikampuni vidogo vidogo ambavyo vina hisa.
“Kampuni zilizo chini ya mwavuli huo kampuni ya Mwananchi Trust ni Umoja Entertainment yenye asilimia tano ya hisa, VNB asilimia tano, WM Holding inayomilikiwa na Yusuph Mushi ina hisa asilimia na tano, CCM Trust Company inayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) chenye hisa asilimia 15 ambayo ndiyo ilikuwa na hisa nyingi.
“Kwa hiyo, taarifa kwamba mimi nimetafuna fedha za mradi wa Mwananchi Gold Company Ltd si za kweli, sijatumia vibaya fedha za kampuni hiyo, malipo yote tuliyolipwa na BoT yaliyotokana na mkopo kwa mradi huo zipo kwenye maandishi na ushahidi upo wazi.
“Nashangazwa sana na hali kwa sababu wakati serikali ikiipiga vita ya wazi kampuni hiyo, imekuwa ikitoa msamaha wa kodi kwa miaka mitano kwa kampuni za kigeni ambazo zipo nchini kwa ajili ya kuwekeza.“Inaipiga vita sasa wakati ni serikali hiyo hiyo iliimuru BoT iikopesha dola milioni tano kuendesha mradi wake wa kusafishaji dhahabu, fedha ambazo ninatuhumiwa kupitia taarifa zinazoenezwa kwenye mitandao na baadhi ya vyombo vya habari kwamba nilizitumia kiujanja ujanja kwa manufaa yangu binafsi.“Nayasema haya baada ya viongozi wawili wazito kutoka serikalini waliofikia kwa nyakati tofauti kunieleza maneno tofauti.mmoja aliniambia Taasisi ya Kuzua na Kupambana na Rushwa (Takukuru) haina nia ya kunishitaki, mwingine alikuja kunieleza nitashitakiwa bila Takukuru kujulishwa.
“Taarifa hizi zinanisababishia usumbufu mkubwa kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki ambao wamekuwa wakinipigia simu na wakati mwingine wakifurika nyumbani kwangu ili kupata ukweli wa jambo hili.“Ila mimi ni msafi na nipo tayari kwa lolote, kwani hesabu za kampuni hii zipo sawa na ushahidi wa haya yote niliyowaeleza upo kama nilivyowaeleza.” Alimalizia kueleza Jaji Warioba kwa sauti ya masikitiko.

0755 312859

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 21 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.