Header Ads

KESI YA NYAMUMA KUSIKILIZWA UPYA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania imeiamuru Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuanza kusikiliza upya na kutolea uamuzi ombi la kukazia uamuzi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala moja mara.

Hukumu hiyo ilitolewa jana mahakamani hapo na Jopo la Majaji watatu likiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Agustino Ramadhan, ambaye alisaidiana na Jaji Mstaafu Damian Lubuva na Harod Nsekela. Hukumu hiyo ilisomwa kwa niaba yao na Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Profil Lyimo.

Jopo hilo la majaji lilifikia kutoa uamuzi huo baada ya kukubaliana na ombi la madai namba 88 la mwaka 2006 ambalo liliwasilishwa na mrufani ambaye ni Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu(LHRC) la kutaka mahakama hiyo itengue uamuzi wa Mahakama Kuu na kuiomba mahakama hiyo iwasilikilize na iruhusu utekelezaji wa uamuzi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Ubora enzi hizo ilikuwa ikiongozwa na Jaji Robert Kisanga.

“Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili jopo hili linakubaliana na hoja za mrufani na kwa sababu hiyo mahakama hii inaiamuru Mahakama Kuu kusikiliza mara moja maombi ya warufani yanayotaka kukaziwa kwa uamuzi wa Tume ya Kisanga, kwani Mahakama Kuu ina mamlaka ya kisheria ya kulisikiliza ombi hilo.

“Hivyo mahakama hii inatamka bayana kwamba Mahakama Kuu ilikosea kisheria wakati ilipotoa uamuzi wake ilivyosema kwamba mahakama hiyo haina mamlaka kisheria ya kusikiliza ombi hilo kwa sababu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora si mahakama.

“Tume ya Hakimu za Binadamu na Utawala Bora imeundwa kwa mujibu wa sheria za nchi na ina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya haki za binadamu na kutoa maamuzi yake hivyo, Mahakama Kuu ilikosea kusema Tume hiyo si mahakama na pia mahakama hii imeiamuru serikali kulipa gharama zote za uendeshaji wa shauri hili tangu lilipofunguliwa Mahakama Kuu hadi Mahakama ya Rufaa,” alisema Jaji Ramadhani.

Katika rufaa ya kesi hiyo maarufu kwa jina la ‘Kesi ya Nyumuma’mrufani alikuwa akitetewa na wakili wa kujitegea Alex Mgongolwa na Francis Stolla wakati upande wa serikali ulikuwa ukiwakilishwa na Methew Mwaimu.

Akitoa uamuzi wake Jaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi wakati huo, Projest Lugazia alitupilia mbali ombi hilo kwa maelezo kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza hayo ya kukazia uamuzi wa Tume kwa sababu tume si mahakama.

LHCR katika kesi hiyo inamshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Thomas Ole Sabaya, Mkuu wa Kituo cha Polisi wa Serengeti, Alexender Lyimo na uongozi wa kijiji cha Bonchugu na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

Katika madai yake ya msingi aliyowasilisha kwenye Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, LHCR iliomba tume hiyo, itamke kuwa wananchi 135 waliofukuzwa kwenye eneo la Nyamuma Iliyobaki, walifukuzwa kunyume cha sheria na kinyume na Ibara 24 ya Katiba ya nchi inatamka kwamba kila mtu ana haki ya kumiliki mali na hifadhi ya mali zake kwahiyo ni marufuku mtu kuporwa mali na hifadhi zake.

Na kwamba wananchi hao walipwe fidia ya sh milioni 900 kutokana na mali zilizoalibiwa na wadai Oktoba 12 mwaka 2001.Mapema mwaka 2002 LHCR ilipeleka rasmi malalamiko yake kwenye Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora .

Ambapo Desemba 2004 tume hiyo baada ya kutembelea eneo la tukio na kuwahoji mashaidi 30 ilitoa uamuzi wake na kusema kwamba imekubaliana na maombi ya LHCR na kuagiza wananchi hao 135 warudishiwe ardhi ya na kwamba walipwe fidia ya jumla y a sh milioni 900.

Mapema mwaka jana, katika Mahakama Rufaa wakati rufaa hiyo inasikilizwa, Wakili Mgongolwa aliambia Mahakama ya Rufaa kwamba uamuzi wa kuwafukuza wananchi katika eneo lao ulikuwa ni wa uonevu na kwamba ulikiuka Ibara ya 24 ya Katiba ya nchi inayotamka kwamba kila mtu ana haki ya kumiliki mali na hifadhi ya mali zake kwahiyo ni marufuku mtu kuporwa mali na hifadhi zake, lakini serikali ilitumia mabavu na kupora ardhi ya wananchi hao.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Serikali Methew Mwaimu aliomba mahakama hiyo kuitupa rufaa kwasababu ina dosari za kisheria.

Akizungumza na gazeti hili baada ya mahakama hiyo kutoa hukumu,Mgongolwa alisema amefurahishwa na uamuzi huo na kwamba anakwenda kuwaeleza wateja wake na muda wowote kuanzia sasa watapeleka kesi hiyo Katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kwasababu tayari inabaraka za Mahakama ya Rufaa, ili wananchi wa Nyamuma Iliyobaki, waweze kutendewa haki kwa mujibu wa sheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Januari 3 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.