Header Ads

SHAHIDI AZIDI KUIBUA MAPYA

Na Happiness Katabazi

MKUU wa kitengo cha uendeshaji wa huduma kwa wateja katika Commercial Bank of Africa, Ronald Manongi, ambaye ni shahidi wa pili katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 za EPA inayomkakili Farijala Hussein na Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda, jana alimaliza kutoa ushahidi wake kwa kuieleza mahakama kuwa hajawahi kupokea malalamiko toka Kampuni ya BC Cars Export Ltd ya Mumbai, India kwamba imedhulumiwa fedha na Kampuni ya Kiloloma & Brothers ya Tanzania.

Shahidi huyo, alieleza hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, alipokuwa akijibu maswali ya wakili wa utetezi, Majura Magafu.

Alidai BC Cars Export Ltd yenye akaunti UK iliingiziwa fedha hizo kwa njia ya Telegraph Transfer (TT) na kampuni ya Kiloloma & Brothers ambayo ilikuwa na akaunti Commercial Bank of Africa.

Hata hivyo, alidai BoT haijawahi kuitaarifu benki yake kwamba sh bilioni 1.8 walizoiingizia Kiloloma & Brothers si malipo halali.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili Magafu na Shahidi Manongi:
Wakili: Jana (Juzi) wakati unaongozwa na msomi mwenzangu, Stanslaus Boniface, kutoa ushahidi, uliiambia mahakama kwamba baada ya kuona kiasi hicho cha fedha kimeingia kwenye akaunti ya washtakiwa ulipatwa na wasiwasi, eh ulimpigia simu Ofisa wa BoT? Tutajie jina lake tafadhali?
Shahidi: Iman Mwakosya ambaye pia anakabiliwa na kesi za EPA katika mahakama hii.
Wakili: Eeeh.. Mwakosya alikujibu nini kwenye mazungumzo yenu katika simu?
Shahidi: Aliniambia fedha hizo ni halali na BoT imezituma kwa Kiloloma & Brothers.
Wakili: Ulimuuliza Mwakosya ni kwa nini BoT inawalipa hizo fedha?
Shahidi: Alinijibu ni deni la EPA.
Wakili: BoT waliingizia fedha akaunti kwa Tsh au fedha za kigeni ambayo zina thamani gani?
Shahidi: Paundi 921,178.83.
Wakili: Kuna siku yoyote BoT waliwahi kuwaandikia kwamba malipo hayo si halali?
Shahidi: Hawajawahi kuiandikia benki yetu kwamba malipo hayo si halalali.
Wakili: Kuna siku wateja wangu walikiuka masharti ya benki mliyowapa kabla ya kufungua akaunti yao?
Shahidi: Sikumbuki kama waliwahi kukiuka masharti.
Wakili: Ni wakati gani benki inaweza kumwambia mteja hapo umekiuka taratibu?
Shahidi: Pale mteja anapokiuka taratibu za kibenki.
Wakili: Nyie benki mnaruhusiwa kuingilia matumizi ya fedha za mteja wenu?
Shahidi: Hatuingilii.
Wakili: Mteja anapokuja na leseni na deed of partnership ya kampuni yao zinazoonyesha wanafanya biashara mbili tofauti, yaani leseni inasema wanafanya biashara ya kukusanya manyoya halafu deed of partnership inasema wanakusanya madeni mnafanyaje?
Shahidi: Sisi tulimwangalia mdhamini wa Kiloloma & Brothers ambaye ni Rashhaz(T)Ltd, ambaye ndiye alimtambulisha kwetu tukawafungulia akaunti. Na kwa mujibu wa saini ya akaunti ya Rashhaz(T)Ltd inaonyesha Maranda ndiye mmiliki kwa kampuni hiyo.
Wakili: Utakubaliana na mimi benki yenu, suala la leseni na deed of pertneship mnalifumbia macho?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Kimsingi mtakubaliana na mimi benki yenu, Kiloloma & Brothers hamna tatizo nayo?
Shahidi: Hatuna tatizo nayo.
Wakili: Benki yenu mliwahi kuona makubaliano ya Kiloloma & Brothers kuitumia fedha BC Cars Export Ltd?
Shahidi: Hatujawahi kuyaona.
Wakili: Benki yenu ilishawahi kupata malalamiko toka BC Cars Export Ltd kwamba wamedhulumiwa fedha zao na Kiloloma & Brothers?
Shahidi: Hatujawahi kupata malalamiko.
Wakili: Mnawaamini wateja wenu (washtakiwa)?
Shahidi: Tunawaamini ndiyo maana tuliendelea kufanya nao biashara.
Aidha shahidi wa tatu katika kesi hiyo, Meneja wa Kenya Commercial Bank Tawi la Mlimani, Twilumba Talawa (34), alidai yeye ndiye aliyewafungulia akaunti ya Kiloloma & Brother washtakiwa wakati huo akiwa Meneja Msaidizi Kitengo cha Huduma kwa wateja wa benki ya United Bank of Africa.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili wa Serikali na shahidi:
Wakili: Agosti mwaka 2003 ulikuwa ukifanya kazi katika benki gani?
Shahidi: United Bank of Afrika (UBA).
Wakili: Kuna umoja wa biashara unafahamika kwa jina la Kiloloma & Brothers, uliufahamu lini na vipi?
Shahidi: Niliufahamu baada ya wateja wangu kufika ofisini kwa ajili ya kufungua akaunti.
Wakili: Angalia hii fomu, waliomba kufungua akaunti ya kampuni hiyo ni akina nani?
Shahidi: Farijara na Maranda.
Wakili: Watu hao wapo hapa mahakama ebu watambue?
Shahidi: Wale wawili walioketi pale kizimbani (anawanyooshea kidole).
Wakili: Fomu hiyo ya kufungulia akaunti ya kampuni hiyo ililetwa na nani ofini kwenu?
Shahidi: Farijara Hussein na fomu hiyo alinikabidhi mimi.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili wa utetezi Majura Magafu na shahidi:
Wakili: Je huyu Farijara na Maranda walileta leseni wakati wanafungua akaunti?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Hiyo leseni benki inawasaidia nini?
Shahidi: Haitusaidii kitu. Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa,Januari 30 mwaka 2009


No comments:

Powered by Blogger.