Header Ads

TAFFA YAPINGA ONGEZEKO GHARAMA ZA MAKONTENA

Na Happiness Katabazi

SIKU chache baada ya Mamlaka ya Bandari (TPA), itangaze uamuzi wa kupandisha gharama za utunzaji wa makontena bandarini, Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), kimeupinga uamuzi huo kwa madai kuwa hauna tija kwa taifa.

Akizungumza na waaandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, rais wa chama hicho, Otieno Igogo alisema chama chake chenye makampuni 500 ya ushuru wa forodha, kimepokea kwa masikitiko uamuzi huo kwani umelenga kumuumiza mtanzania na kuikosesha serikali mapato.

Alisema TPA imelenga kumuumiza watumaji wa bandari kwa kisingizo kwamba ndiyo chanzo cha msongamano wa makontena bandari, jambo ambalo alidai si sahihi.

“Waandishi wa habari hamuwezi kuamini TPA hadi sasa ninavyozungumza nanyi, inafanya kazi zake kwa tenknolokia ya zamani, haifanyi kazi zake hizi za ushuru wa forodha kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kompyuta…huwezi hamini bado inatumia carbon paper’ na dole gumba katika shughuli zake na TAFFA tulishaieleza mamlaka hiyo kwamba waachane na mfumo huo na ikakubali ifikapo Julai mwaka jana, wangekuwa wameanza kutumia mfumo wa kompyuta.

“Na ieleweke kwamba TPA ndiyo inachelewa kukagua makontena na yenyewe ikichelewa kuyakagua haipigwi faini, pia TICS haina uwezo wa kutoa huduma ipasavyo, kwa hiyo sisi tunasema ongezeko hilo la gharama ni udharimu mkubwa na pia siku za usoni utaisababishia nchi kukosa mapato kwani zaidi ya nchi saba zinatumia bandari ya Dar es Salaam hivyo zitalazimika kutumia bandari za nchi nyingine, jambo ambalo ni hatari kwa uchumi wa taifa,” alisema Igogo.

Aidha Igogo alimuomba Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati uamuzi huo wa TPA na kuongeza kuwa ipo haja ya serikali kukiondoa kipengele kinachoipa madaraka TICS ya kuendesha shughuli zote za makontena bandarini kwa maelezo kuwa kipengele hicho katika mkataba huo, kinachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la msongamano wa makontena bandarini kwani TICS haina uwezo wa kutoa huduma kikamilifu.

Januari mosi mwaka huu, TPA ilitangaza ongezeko la gharama la utunzaji wa gharama wa makontena bandarini kwa asilimia 100.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Januari 5 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.