Header Ads

MRAMBA,YONA,MGONJA,KESI MOJA

*Sasa wapunguziwa dhamana zao
*Wacheka na kutabasamu kizimbani

Na Happiness Katabazi

KATIBU Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja, wameunganishwa katika kesi moja ya jinai namba 1200 ya mwaka 2008 inayowakabili waliokuwa mawaziri waandamizi wa serikali ya awamu ya tatu, Basil Mramba na Daniel Yona.

Kuunganishwa kwa Mgonja katika kesi hiyo kulitokana na ombi la Mwanasheria wa Serikali, Biswalo Mganga, ambaye aliwasilisha ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DDP), Eliezer Feleshi.

Mwanasheria huyo alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, DPP hana nia ya kuendelea na kesi namba 1211 ya mwaka jana iliyokuwa ikimkabili Mgonja.

Maganga alisema kwa sababu hiyo, DPP ameiomba mahakama imuunganishe Mgonja katika kesi hiyo namba 1200 ya mwaka jana, ambapo kwa sasa itakuwa na jumla ya washtakiwa watatu ambao ni Mramba ,Yona na Mgonja, ombi ambalo lilikubaliwa na Hakimu Hezron Mwankenja wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Baada ya kesi hiyo kufutwa mahakamani hapo, washitakiwa hao walipandishwa tena kizimbani na kusomewa mashtaka mapya, na mwanasheria huyo kuieleza mahakama kwamba, kwa kuwa Mgonja ameongezeka katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa umeandaa hati mpya ya mashtaka ambayo ina jumla ya mashtaka 12.

Katika kesi hiyo Mramba anatetewa na mawakili wa kujitegemea Harbert Nyange na Peter Swai,Yona akitetewa na wakili Sam Mapande na Joseph Tadayo wakati Mgonja akitetewa na Profesa Leonard Shaidi.

Hati ya mashtaka inaonyesha kuwa Mramba anakabiliwa na mashitaka yote 12, Yona mashitaka sita na Mgonja anakabiliwa na mashtaka saba.

Awali Mgonja alikuwa akikabiliwa na mashtaka nane, Yona mashtaka matano na Mramba mashtaka nane, hivyo kufanya hati hiyo ya mashtaka yaliyofunguliwa mwanzoni kuwa na mashtaka 13.

Akiwasomea maelezo ya kosa hilo, Mganga alidai kwamba katika shtaka la kwanza, pili, tatu , nne, saba, na la 12 yanamkabili Yona, na shtaka la tano, sita, tisa, kumi, 11,12 yakimkabili Mgonja, wakati Mramba akiwa anakabiliwa na mashtaka yote 12.

Mganga alidai kwamba, washtakiwa kwa makusudi au kwa kushindwa kuchukua tahadhari kwa mujibu wa taratibu za kazi, akiwa Katibu Mkuu Hazina na wakiwa mawaziri katika serikali ya awamu ya tatu, waliruhusu kutolewa kibali cha serikali kilichoisaidia Kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation kutolipa kodi, tofauti na mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA), uamuzi ambao uliisababishia serikali hasara ya sh 11,752,350,148.00.

Mganga alidai kwamba Mramba na Yona kati ya mwaka 2002 na 2005, Mramba akiwa Waziri wa Fedha na Yona akiwa Waziri wa Nishati na Madini, walitumia madaraka yao vibaya kwa kuingia mkataba wa miaka miwili na Kampuni ya M/S Alex Sterwart (Assayers) Government Bussiness Corporation kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Mwaka 2002.

Alidai kuwa, mkataba huo ulianza Juni 14 mwaka 2005 hadi Juni 23 mwaka 2007 na kati ya Machi na Mei 28 mwaka 2005, watuhumiwa hao walitumia vibaya ofisi za umma kwa kumualika Dk. Enrique Segure wa M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation kuja nchini na kumtaarifu kuwa wizara walizokuwa wakizisimamia zimeidhinisha kuipatia mkataba wa miaka miwili kampuni hiyo ya uhakiki wa madini kabla ya timu ya serikali kuruhusu kuingiwa kwa mkataba na kampuni hiyo.

Aliendelea kudai kwamba, Oktoba 10 mwaka 2003 Mramba, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Fedha, alitumia madaraka yake vibaya na kudharau maelekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA) ya kutaka kampuni hiyo isipewe msamaha wa kodi.

Alidai mahakamani hapo kwamba, kati ya mwaka 2003 na 2005 Mramba na Mgonja waliipendelea kampuni hiyo kwa kutoa notisi ya serikali ya kuisamehe kodi, kwa hati namba 423/2003, 424/2003, 497/2004 498/2004, 377/2005 na 378/2005 na kuisababishia serikali hasara ya sh 11,752,350,148.00.

Washtakiwa wote walikana mashtaka na Hakimu Mwankenja alisema wataendelea kuwa nje kwa dhamana hadi Februari 2 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.

Hata hivyo mawakili wa utetezi waliiomba mahakama hiyo kupunguza kiwango cha dhamana kwa washtakiwa hao kwa sababu Mgonja ameongezeka kwenye shauri hilo.

Awali Mramba na Yona walitakiwa watoe fedha au hati zenye thamani ya sh bilioni 2.9 ili wapate dhamana, wakati Mgonja aliamriwa kujidhamini kwa hati zenye thamani ya sh bilioni 5.9

Ombi hilo lilikubaliwa na hakimu Mwankenja ambapo alisema kwa kuwa mshtakiwa mwingine ameshaongezeka kwenye kesi hiyo, kila mshitakiwa atatakiwa kudhaminiwa kwa hati ya sh bilioni 2.

Hakimu huyo aliamuru kwamba hati za awali zilizotumika kuwadhamini watuhumiwa hao ambazo
zina thamani zaidi ya kiasi hicho warudishiwe wadhamini wao na zibaki hati zenye jumla ya thamani ya kiwango kipya cha bilioni 2 kwa kila mshtakiwa.

Mramba na Yona kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani Novemba 15 mwaka jana wakati Mgonja alifikishwa mahakamani hapo Desemba 15 mwaka jana. Washtakiwa wote walikana mashtaka yao na wote wapo nje kwa dhamana.

Hata hivyo katika hali isiyotarajiwa watuhumiwa hao walikuwa wakicheka na kutabasamu wakati wote tangu walipofika jana asubuhi ambapo waliketi kwenye chumba cha mawakili mahakamani hapo hadi majira ya saa 5:15 walipoingia kwenye chumba namba mbili kwa ajili ya kusikiliza mwenendo wa shauri lao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Januari 3 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.