Header Ads

WANAFUNZI MLIMANI WAACHIWA KWA DHAMANA

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), Anthony Machibya, na wenzake wanne wanaokabiliwa na shtaka la kufanya mkusanyiko kinyume na sheria, wameachiwa kwa dhamana.

Washtakiwa hao waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyotolewa na Hakimu Victoria Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Masharti hayo ni kuwa na mdhamini ambaye ni mwajiriwa wa serikali, atasaini dhamana ya sh 500,000. Pia washtakiwa hawataruhusiwa kwenda eneo la Chuo Kikuu hadi wapate ruhusa ya mahakama na kuliripoti kila Ijumaa katika Kituo cha Polisi Oysterbay.

Mbali ya Machibya, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu wa Mtandao wa Wanafunzi Nchini(TSNP), Owawa Stephen; na wengine ni Sabinus Pius, Titus Ndila na Issa Paul.

Washtakiwa hao walitimiza masharti ya dhamana jana mchana na kulakiwa na baadhi ya waadhiri na wanafunzi wenzao nje ya viwanja vya mahakama hiyo.

Jumatano iliyopita, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na shtaka la kufanya mkusanyiko kinyume na sheria.

Washtakiwa hao walidaiwa kutenda kosa hilo Januari 19 mwaka huu, saa nne asubuhi eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa madhumuni ya kutenda kosa, washtakiwa walitengeneza mazingira ya kuhatarisha uvunjifu wa amani wakati zoezi la udahili wa wanafunzi wa mwaka wa tatu na wa nne ukiendelea.

Pia ilidiwa washtakiwa hao walibeba mabango yenye maneno ‘Laiti Nyerere angefufuka leo angelia machozi, kweli Kikwete umesahau umaskini wako;” maneno ambayo yameelezwa yamejielekeza kujenga chuki kwa watu wengine na hatimaye kuweza kuleta uvunjifu wa amani. Kesi itatajwa Februari 7 mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Jumamosi, Januria 24 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.