Header Ads

KINARA WA RICHMOND KORTIN

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE, serikali jana imemfikisha mahakamani mtu anayetajwa kuwa kinara wa kashfa ya Richmond.

Mtuhumiwa huyo, Naeema Adam Gile, alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa tuhuma za kughushi na kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa serikali.

Gile, alifikishwa mahakamani hapo kimya kimya saa 8:05 mchana, na kusababisha waandishi wa habari wanaoripoti habari za mahakamani kushindwa kujua kinachoendelea huku wengine wakiwa wakimekwisha kuondoka.

Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, aliyekuwa akisaidiana na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Frederick Manyanda, alidai mbele ya Hakimu Waliarwande Lema kwamba, mshitakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka matano ambayo aliyatenda kwa nyakati tofauti.

Wakili Boniface alidai kuwa, Machi 13, 2006, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa na dhamira ya kutenda kosa, alighushi hati ya nguvu ya kisheria (power of attorney) inayoonyesha imetolewa na Hamed Gile, ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, kwamba amemruhusu kufanya shughuli za kampuni hiyo hapa nchini.

Wakiri Boniface alidai kwamba, shitaka la pili ni kutoa taarifa za uongo, kuwa Machi 20 mwaka 2006, katika eneo la Ubungo, Umeme Park, Barabara ya Morogoro, mshitakiwa alitoa hati hiyo ya nguvu ya kisheria inayomuidhinisha yeye kwamba ameruhusiwa kufanya kazi ya kampuni hiyo ya Marekani hapa nchini.

Aliendelea kudai kuwa, shitaka la tatu linalomkabiri mtuhumiwa huyo ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma na kwamba Julai 20, 2004 eneo la Ubungo Umeme Park, alitoa taarifa ya uongo kwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Shirika la Umeme (TANESCO). Kwamba Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 100 kwa Tanzania ili wajumbe wa bodi hiyo waweze kumpendekeza kupewa tenda ya kutoa huduma hiyo.

Katika shitaka la nne, alidai Juni, 2006 jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya serikali, kuwa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango hicho ili apewe tenda hiyo.

Wakili Boniface ambaye amejizolea sifa tangu kuanza kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa wa kesi za wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) alidai shitaka la tano la mshitakiwa huyo ni la Julai, 2006, ambapo mshitakiwa akifahamu na kwa ulaghai, alitoa hati ya nguvu ya kisheria iliyotolewa Machi 3, mwaka huo iliyokuwa ikimuonyesha kuwa ameruhusiwa na Mwenyekiti wa Kampuni, Hemed Gile, kufanya kazi za kampuni hiyo hapa nchini.

Hata hivyo, mshitakiwa alikana mashtaka yote na upande wa serikali ulisema upelelezi bado haujakamilika na kwamba hauna pingamizi na dhamana.

Wakili wa kujitegemea, Kato Zake, anayemtetea mshtakiwa, aliiomba mahakama impatie dhamana mteja wake kwa sababu afya yake si nzuri na anatarajiwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo habari zilizopatikana mahakamani hapo zilieleza kuwa hati ya kusafiria ya mshitakiwa inashikiliwa na polisi. Hakimu Lema alisema uamuzi wa kumpatia dhamana mshtakiwa atautoa leo na aliamuru mshitakiwa apelekwe rumande.

Wakati huo huo, waandishi wa habari wanaoripoti habari za mahakamani jana walionekana kukerwa na hatua ya Hakimu Lema kuendesha kesi hiyo kwenye ‘chamber’ wakati mahakama za wazi mahakamani hapo zilikuwa wazi.

Waandishi hao walieleza kuwa hatua hiyo ya Hakimu Lema, iliwapa wakati mgumu kusikiliza mwenendo wa shauri hilo.

Gile amefikishwa mahakamani ikiwa ni takriban mwaka mmoja sasa baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na mwenzake aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, walilazimika kujiuzulu nyadhifa zao kwa kashfa hiyo ya Kampuni ya Richmond.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 15 mwaka 2009


No comments:

Powered by Blogger.