Header Ads

SHAHIDI: MSHITAKIWA AMEKUBUHU KUPORA WANAWAKE

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa pili katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia nguvu inayomkabili Ezekiel Matitu, maarufu ‘Madilu’, amedai kuwa mshitakiwa huyo amekubuhu kuwapora na kuwajeruhi wanawake wanaokodi teksi jijini Dar es Salaam.

Shahidi huyo, F 2486 D/C Pius, alidai mbele ya Hakimu Henzron Mwankenja wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mshitakiwa huyo ni mzoefu wa kufanya uhalifu huo kwa sababu anakabiliwa na kesi 11 za aina hiyo.

Akiongozwa na Mwendesha Mashtaka, Abubakar Mrisha, shahidi huyo alidai kuwa katika kufanya uhalifu huo, mshitakiwa huyo amekuwa akifanya uhalifu huo huwa na wenzake, ingawa Jeshi pa Polisi halijafanikiwa kuwakamata.

“Hakimu, huyu mshitakiwa ni hatari kwa jamii kwa sababu amekubuhu katika aina hii ya uhalifu na katika kuthibitisha hilo mshitakiwa huyu ana kesi 11 za aina hii mahakamani hapa na wanaolalamika ni wanawake.

“Kesi saba kati ya hizo zimeondolewa mahakamani kutokana na mshitakiwa na washirika wake kuwapigia simu za vitisho wanawake hao waliowatendea uhalifu kwamba wasifike mahakamani kutoa ushaidi na kwamba endapo watafika watafanyiwa unyama wa kutisha,” alidai mashahidi huyo.

Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Balili Kasongo, ambaye alipora vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh 1,140,000 alidai Januari mwaka jana, alipotoka Extelecom kuchukua dola 2,000 alizokuwa ametumiwa na ndugu yake alikodi teksi ambayo ilikuwa imeegeshwa jirani na kutaka impeleke Ubungo.

Alidai baada ya kufika Magomeni, dereva teksi alimweleza anaingia Sheli kuweka gari, lakini ghafra alimuona akipandisha vioo vya gari na kuwasiliana kwa simu na wenzake ambao baada ya muda mfupi walifika na kuwafungia milango. Shahidi huyo alidai miongoni mwa watu walioingia alikuwapo Madilu.

“Wakati dereva ananifanyia uhuni huo ndipo Madilu na mwenzake walianza kunipora cheni ya shingoni na mkononi, simu mbili za mkononi, pochi na dola 2000 huku Madilu akiendelea kunipiga vichwa kwenye paji la uso na kunichoma na bisibisi usoni,” alidai shahdi huyo.

Alidai licha ya mshitakiwa huyo kuwa rumande amekuwa akipokea simu za vitisho kutoka kwa mshitakiwa huyo akimtaka wakutane ampe fedha, ili asiende mahakamani kutoa usahidi.

Katika kesi hiyo, mshitakiwa huyo na wenzake wawili wanadaiwa kuwa Januari 29 mwaka jana, walimuibia Kasongo cheni za dhahabu za mkononi na shingo, simu mbili za mkononi vitu vyote vikiwa na jumla ya sh 1,140,000 na kabla ya kuiba alimtishia kwa silaha za jadi na kumjeruhi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Januari 9 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.