Header Ads

NJAMA ZA KUIBA MAFAILI KESI ZA EPA YAFICHUKA

Na Happiness Katabazi

JESHI la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limefanikiwa kuzima mpango wa baadhi ya makarani na wafanyakazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutaka kuiba majalada ya watuhumiwa wa kesi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), yaliyopo katika mahakama hiyo.

Vyanzo vyetu vya habari kutoka ndani ya mahakama hiyo, vilidai kuwa mkakati huo ulipangwa kufanyika juzi, majira ya saa 10:30 jioni, lakini ulizimwa na polisi.

Inadaiwa kuwa baada ya polisi kumi kutoka Kituo cha Polisi Kati, kufika katika mahakama hiyo, waliwatoa kwa nguvu makarani na wafanyakazi wa mahakama hiyo ambao walikuwa bado wamo ofisini wakati muda wao wa kazi ulishamalizika.

Kwa mujibu wa habari hizo, ujio wa polisi hao mahakamani hapo, ulitokana na mwito wa Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Addy Lyamuya, aliyetoa taarifa za kuwapo mpango huo kwani alishangazwa na hatua ya makalani hao kuendelea kubaki ofisini wakati muda wao wa kazi ulishamalizika.

“Juzi jioni waandishi wakati mmeondoka, kulikuwa na kasheshe, polisi waliitwa kimya kimya na Lyamuya na walipofika, waliingia maofisini na kuanza kuwatoa kwa amri baadhi ya makarani wakati muda wa kazi umepita na inadaiwa kulikuwa na taarifa za kuwepo njama za kuibwa kwa mafaili ya EPA,”

“Na kwambia walitolewa mbio ofisini na kuambiwa kuanzia jana (juzi) makarani ambao mahakimu wao hawatakuwa wakiendesha kesi zaidi ya saa 9.30, hawaruhusiwi kuendelea kuwepo eneo hilo, vinginevyo watachukuliwa hatua,” alisema mmoja wa maofisa wa mahakama hiyo.

Alipohojiwa na waandishi wa habari juu ya tukio hilo, Mkuu wa Waendesha Mashtaka, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Charles Kenyela, alikiri kuwapo kwa tukio hilo.

Alisema siku hiyo, alikuwa njiani kuelekea nyumbani kwake, alipigiwa simu na mkubwa wake wa kazi bila kumtaja jina, akimtaka arudi Kisutu haraka kwa madai kuwa kulikuwa na tatizo.

“Ni kweli askari waliletwa na kwa mujibu wa taarifa nilizopata ni kwamba kuna baadhi ya makarani walikuwa wakiandaa barua ya dhamana ya aliyekuwa Meneja Utumishi na Utawala wa BOT, Amatus Lyumba, ambaye yupo rumande kwa kushindwa kutimiza masharti, wakati muda wa kazi umekwisha….zaidi ya hapo sijui,” alisema Kenyela.

Alipomfuata Lyamuya ili aelezee tukio hilo, alikiri kuita askari hao lakini alisema aliwaita kwa ajili ya kuimarisha usalama katika eneo hilo la mahakama.

“Ni kweli niliomba niletewe askari polisi ili waje kuimarisha ulinzi, hayo maswali mengine siwezi kuyajibu, nendeni mkawaulize hao makarani watawaeleza kutoka midomoni mwao kwani nao wanahaki ya kuzungumza,” alisema Lyamuya.

Wakizungumzia hali hiyo ya kuwepo tuhumu za kutaka kuibwa kwa majarada ya kesi za EPA, baadhi ya mawakili wa serikali walisema hilo linaweza kufanyika lakini wao wapo makini katika utunzaji wa vielelezo vitakavyowasilishwa kwenye kesi hizo.

Taarifa za kuwepo wingu la ufisadi katika kesi za EPA kwa mara ya kwanza ziliandikwa na gazeti hili mapema Desemba mwaka jana kwamba kuna baadhi ya watendaji wa mahakama wamezigeuza kesi hizo kuwa mradi wa kujipatia fedha toka kwa washtakiwa, hali iliyosababisha baadhi ya watendaji hao kutoaminiana.

Hali hiyo ilimfanya Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Ferdnand Wambali kuwasili mahakamani hapo kuzungumza na mahakimu na makalani wao, akiwataka wawe makini na uendeshaji wa kezi za EPA.

Hadi sasa, jumla ya washtakiwa 21 wamefikishwa katika mahakama hiyo wakituhumiwa kwa wizi wa fedha za EPA zaidi ya sh bilioni 133, mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Januari 31 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.