Header Ads

TUMELIZIKA AZIMIO LA ARUSHA,LA ZANZIBAR LINATUTAFUNA

Na Happiness Katabazi

TAIFA lisifike mahala likafikiri kwamba linaweza likavunja misingi iliyoliunda bila kuangamia.

Kama misingi aliyotuachia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, haitoshi ni vyema tuiboreshe. Lakini tukiing’oa misingi hiyo na kutupilia mbali, taifa litaangamia.

Kwa sasa hoja juu ya ufisadi kweli ni kubwa, lakini Mwalimu Nyerere alitaadharisha kwamba wale waliokwenda Zanzibar na kulitupa baharini Azimio la Arusha na miiko ya uongozi wanahujumu misingi isiyo na doa ya taifa letu.

Na kweli historia nzima ya ubinafsishaji imeonyesha jinsi tulivyoingia kwenye mfumo wa kibepari kwa pupa, huku ikiwa ni rahisi kujenga misingi ya ufisadi kwa kuruhusu viongozi kufanya biashara.

Leo hii kila uchwao, kashfa zinazoibuka ni zile zinazowahusu viongozi wetu wanaofanyabiashara wakati huo wanashikilia nafasi za uongozi.

Kwa kweli ni viongozi wachache mno ambao mali binafsi walizojichumia zinalingana na kipato halali.

Wengine wametajirika kwa kupora mali ya umma na wengi wanaendelea kutajirika kupitia Sheria ya Manunuzi ya Huduma za Umma kwa kuzipendelea kampuni zao au maswahiba zao wanaoshirikiana nao kibiashara.

Mwalimu Nyerere alitaadharisha pia ubinafsishaji uso na mpango wa mashirika ya umma. Kile alichokisema leo tunakiona, yeye alisema tutabinafsisha hadi Magereza, lakini leo ukweli tunaona tumebinafsisha kila kitu hata yale ambayo ni msingi wa uchumi na Usalama wa Taifa.

Mfano Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), hiki ni chombo ambacho kingetumiwa na serikali kuwawezesha wananchi lakini leo tumewauzia makaburu kwa bei chee.

Leo hii wananchi wamesawijika, wanahangaika na ili kukiwepa kikombe hiki cha aibu, viongozi hao hao wako mstari wa mbele kuwashawishi wananchi kuunda benki nyingine za wananchi na kuanzisha SACCOS wakati ambapo tulikuwa tayari tuna NBC ambayo ilikuwa na mtandao hadi vijijini .

Mfano wa pili,tumehujumu shirika la TTCL, Reli, TPDC haya yote ni mashirika nyeti leo hii wauzaji wa mafuta wakitaka wanaweza kukwamisha uchumi wa nchi yetu.

Leo hii makampuni binafsi ya mawasiliano yanaweza kufanya hujuma katika mawasiliano na serikali isiweze kuokoa jahazi kwani wameshikilia mpini, serikali makali. Tuko macho na hili?

Leo hii viongozi wakuu wa taifa kwa namna moja ama nyingine wameingizwa katika mitandao mipya ya kiuchumi inayoundwa kinyemela na serikali na kisha kuishia kuchafuliwa majina yao kwa vile serikali haina ubavu tena wakutangaza wazi kwamba inaanzisha mashirika ya umma.

Makampuni kama hayo ni Mwananchi Gold Company Ltd, Meremeta, Tangold n.k. Pia leo hii serikali imejikuta bubu kuelezea ubinafsishaji au ukodishaji wa miundombinu ya nchi kama reli kwa vile biashara hii kamwe haiwezi kuendeshwa na mtu binafsi.

Nafasi za watumishi wa serikali sasa inadaiwa kutolewa kwa kujuana, kulinda na kujenga mtandao wa ulaji lakini katika hayo yote kinachochefua ni pale viongozi wasafi (ambao ni wachache) wanapotuhumiwa kwa ufisadi ili tu kufurahisha wakubwa waliopo madarakani au kukomeshana kwa kuwachafuana ili kila mtu aonekane ni mchafu.

Tukubali rushwa inapokuwa ya kimfumo, kwa maana kwamba inafanywa kupitia vyombo vya dola wengi wataathirika lakini ifikie mahali tuache ushabiki wa vikundi kwa sababu tutaishia kuumizana, ikiwa kila tuhuma za uvunjaji wa sheria zitaunganishwa na ufisadi basi taifa linaweza likakosa mwelekeo.

Tunatambua ya kuwa kuna uvunjifu wa kawaida wa sheria, unaoweza kufanywa na viongozi hata mamlaka husika itawawia vigumu kuushughulikia uhalifu huo, ikiwa utetezi ni kwamba kiongozi amevunja sheria kwakua anapigwa vita na watu anaodai eti ni mafisadi.

Ni vyema tuwe waadilifu na wakweli kwa uvunjifu wa kawaida wa sheria, ushughulikiwe hata kama kiongozi anayehusika na uvunjifu huo atadai yeye ni mpiganaji dhidi ya ufisadi.

Tunachosema ni kwamba upiganaji dhidi ya ufisadi siyo kinga ya makosa ya jinai. Sasa hivi tusishangae kuona taifa lipo katika mkanganyiko, wale watu ambao wenye udhaifu mkubwa katika serikali hata sekta binafsi hawaonyeshi mwelekeo wa uzalendo na taifa usiojali kabila, jinsia, rangi, vikundi wala matabaka.

Matokeo ya hili taifa limeanza kumeguka kwenye makundi yanayotokana na kuporomoka kwa misingi ya taifa tuliloachiwa na Baba wa Taifa.

Kwa msingi huu, kila kundi linatetea maslahi yake na kutaka kulizidi makundi mengine. Katika kulitekeleza hilo, tunasahau kwamba sisi ni Watanzania na Tanzania ni yetu na kwamba pakiwa na amani na ustawi, kila mmoja ataweza kuishi kwa raha.

Kuwepo kwa makundi haya ndani ya jamii yetu yamejengeka maumbile mbalimbali likiwemo kubwa ambalo linachukua mrengo wa kisiasa. Sasa umejikita ndani ya chama kimoja, na uwepo wake unadhihirishwa na uwepo wa makundi mbalimbali tena yenye nia na madhumuni tofauti.

Lakini makundi hayo yanapotokea katika chama tawala (CCM) hatari ni kubwa zaidi sababu baadhi ya makundi yameshikilia vyombo vya dola na yana uwezo ya kuligawa taifa.

Sasa hilo likitokea si jema kwa amani na ustawi, wala si jema kwa vyama vya upinzani.

Cha msingi sasa wote tukubali kwamba Katiba ya nchi na sheria zetu havitoshi, tunaitaji Katiba bora zaidi, itakazoweza kukabiliana na changamoto mpya.

Tukikubali wote bila kufikiria makundi au vyama vyetu vitanufaika vipi, na maslahi mengine binafsi, basi tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuweza kuaandaa mazingira mwafaka ya siasa huru ndani ya nchi yetu, ambayo itaweza kutoa dira na mustakabili wa nchi hii kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Januari 21 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.