Header Ads

DITOPILE AAGA KEKO KWA VURUGU KORTINI

na Happiness Katabazi

MWANZO wa ngoma ni lele. Vurugu, kejeli na mbwembwe zisizo na msingi zilizoanza kufanywa na ndugu na jamaa wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri na kupigiwa chapuo na vituko vyake mwenyewe, jana vilitawala eneo la Mahakama Kuu, wakati shauri la mauaji ya bila kukusudia lilipofikishwa hapo kwa ajili ya kusikilizwa kwa ombi la dhamana.

Ndugu na jamaa hao wa Ditopile ambaye amekuwa katika mahabusu ya Keko tangu Novemba mwaka jana, wakisaidiwa na polisi waliokuwa katika sare na mavazi ya kiraia, walianzisha vurumai kubwa kuwazuia wanahabari kumkaribia au kumpiga picha mwanasiasa huyo ambaye alipewa dhamana.

Vurugu hizo ambazo zilisababisha waandishi kadhaa kujeruhiwa na wengine kuharibikiwa vitendea kazi vyao, zikiwamo kamera, ziliambatana na kurushiana makonde na maneno kati ya wanahabari hao kwa upande mmoja na jamaa na ndugu wa Ditopile, waliokuwa wakisaidiwa na polisi.

Matukio hayo yaliyokwenda sambamba na kuwamwagia maji wanahabari na kutoa maneno ya kuidhalilisha serikali na hata viongozi wake wakuu, yalifanywa na baadhi ya ndugu na jamaa hao wa Ditopile waliothibitisha pasipo shaka kuwa walikuwa ni watu wasio na staha, walioshindwa kujiheshimu, wapungufu wa hekima, waliokosa subira na walioamua kwa makusudi kuidharau mahakama na taaluma ya habari.

Vurugu hizo zilianzia ndani ya jengo la mahakama majira ya saa 8:59 na kumalizikia nje ya geti la mahakama hiyo saa 9:50 alasiri, wakati Ditopile aliyekuwa katika ulinzi mkali huku akiwa amevaa kofia yake ya ‘pama’ akitoka nje ya jengo la Mahakama Kuu.

Wanahabari wa Tanzania Daima waliokuwapo eneo la Mahakama Kuu katika Barabara ya Kivukoni walikuwa miongoni mwa watu waliokumbwa na zahama hiyo ambayo ilisababisha Joseph Zablon, ambaye ni mpiga picha kujeruhiwa sehemu za mdomoni.

Kikubwa kilichoonekana kuwakera polisi, ndugu na jamaa za Ditopile ni wajibu wa kikazi wa wanahabari hao kufanya juhudi za kumfikia mwanasiasa huyo aliyekuwa amezingirwa kwa lengo la kumficha, huku yeye mwenyewe akiwa amejiinamia.

“Tokeni zenu, sisi ndio wenye nchi…siku zote nazi haishindani na jiwe ni lazima itapasuka. …ni mtu wa karibu sana na Dito ambaye ni ndugu yetu, mnafikiri atakubali rafiki yake asote muda wote, haiwezekani na ndiyo kaishapata dhamana, yupo huru na nyie ‘wambea’ endeleeni kuandika weeee! Hadi kalamu zenu ziishe wino…ndiyo hivyo, kaisharejea uraiani.

“Au hamna habari kwamba Ditopile alikuwa Best Man wa …na hadi sasa ni marafiki, na nyie waandishi wa habari kwa akili zenu zilivyo ndogo mnafikiri anapenda anavyokaa jela…duniani hakuna haki, haki ipo mbinguni, utawala huu ni kujuana na wakubwa, mambo yatakunyookea,” ni maneno yaliyokuwa yakitoka kinywani mwa mmoja wa watu waliokuwa wamejumuika katika kundi la ndugu na jamaa wa Ditopile.

Alipotoka katika eneo hilo, Ditopile aliingizwa katika gari dogo aina ya Toyota Ballon, lenye namba za usajili T723ADF, la rangi ya fedha, lililokuwa likisindikizwa na Land Rover (Defender) ya Polisi yenye namba za usajili, T212AMV.

Muda mfupi baadaye, polisi waliokuwa katika eneo hilo, waliwaeleza waandishi wa habari kuwa, msafara huo kwanza ulielekea Keko kuchukua vitu mbalimbali vya mwanasiasa huyo, kabla ya kwenda nyumbani kwake.

Baada ya msafara huo kuondoka saa 9:30, ndugu wa Ditopile na askari kanzu waliobaki mahakamani hapo waliendelea kutupiana makonde na waandishi wa habari huku ndugu hao wakiendelea kutoa lugha ya matusi na kumwaga maji kwenye kamera za wapiga picha ili ziharibike.

Sekunde chache, hali ilibadilika baada ya mamia ya raia ambao waliungana na waandishi wa habari kuwafokea askari ambao awali walikuwa wakisaidia kumficha Ditopile asipigwe picha na kuwazuia waandishi wasimfikie.

“Polisi gani nyie, mnafanya kazi kwa kujipendekeza badala ya kulinda usalama wa raia na kutuliza ghasia lakini nyie ndio mmekuwa chanzo cha vurugu…na kwa taarifa yenu, kwa picha hii mliyoionyesha hapa tumeamini kabisa hapa hakuna kesi,” alisikika akisema mwananchi mmoja aliyekuwa mahakamani hapo na akajitambulisha kwa jina la Dk. Hassan Zubeir.

Miongoni mwa wanahabari waliopata athari kutokana na vurugu hizo ni mpiga picha wa magazeti ya Majira, Business Times na Spoti Starehe, Patrick Spear, ambaye mbali ya kamera yake kuharibiwa alichaniwa vifungo vya shati lake.

“Vurugu hizi zinazofanywa na ndugu wa mtuhumiwa kila kukicha, tena mahakamani, zinaipaka matope serikali na Jeshi la Polisi, na serikali ikae ikijua tayari wananchi wengi wana wasiwasi wa haki kutendeka…haiwezekani hawa ndugu kila kukicha wanafanya vurugu mahakamani na hawachukuliwi hatua,” alisema Mpiga Picha Mkuu wa gazeti la TheCitizen, Mpoki Bukuku.

Awali kabla ya vurugu hizo, Ditopile alipandishwa kizimbani saa 5:20 asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali, huku mahakama ikiwa imefurika mamia ya wananchi waliokuwa na shauku ya kujua kulikoni.

Mmoja wa mawakili wa Ditopile, Profesa Jwani Mwaikusa, aliiomba mahakama impatie dhamana mteja wake kwa kuwa shitaka linalomkabili linadhaminika na kwamba mteja wake ni mtu anayejiheshimu na kuaminika mbele ya jamii, hivyo hawezi kuruka dhamana.

Upande wa Mwanasheria wa Serikali, ulidai mahakamani hapo kuwa haukuwa na pingamizi kuhusu ombi hilo, kwa kuwa dhamana ni haki ya kila mtu.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kuzichambua, Jaji Augustine Mwarija, alitoa dhamana kwa masharti ya bondi ya sh milioni 60. Mshitakiwa alitakiwa kutoa bondi ya sh milioni 20 na wadhamini wawili ambao kila mmoja wao alitakiwa kutoa bondi ya sh milioni 20 kila mmoja.

Mtuhumiwa alitakiwa kukabidhi hati yake ya kusafiria polisi na akatakiwa kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ruhusa ya polisi, na akatakiwa pia awe akiripoti kwa Kamanda wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Ditopile aliletwa mahakamani hapo saa 2:54 asubuhi na msafara wa polisi na akapitishwa kwenye mlango unaotumiwa na majaji.

Muda mfupi baada ya majaji na viongozi wa mahakama hiyo kubaini mchezo huo, waliwafokea polisi hadharani na kusema kitendo hicho kimefanywa kinyume cha taratibu za mahakama.

Naye Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Philophr Lyimo, alikiri kutokea kwa tukio hilo na akasema mahakama hiyo imekerwa na tabia ya polisi hao na kuongeza kuwa, tayari ameshawasiliana na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, ili aweze kuwachukulia hatua askari wake.

“Ule mlango unatumiwa na majaji, hata sisi tumeshindwa kuelewa ni kwa nini wamempitisha katika mlango ule na huku Ditopile ni mtuhumiwa kama mtuhumiwa mwingine….siyo siri tumekerwa na tumeshawaambia kabla ya saa sita leo mchana (jana) wajieleze.

“Hii ni mahakama na watu wanakuja kutafuta haki hapa. Sasa polisi wanapofanya mambo kama haya ambayo nasema yana lengo la kuichafua mahakama yetu, hatuwezi kuyavumilia. Ni lazima wachukuliwe hatua,” alisema Lyimo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Ijumaa Septemba 2 mwaka 2007
;::Sitaisahau vurugu hizi kwani zimeweka historia mbaya katika mahakama ya Tanzania

No comments:

Powered by Blogger.