Header Ads

KWA HILI NAPINGANA NA HAKIMU LYAMUYA

Na Happiness Katabazi

JUMANNE ya wiki hii nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari tuliokutana na fedheha ya kufungua mwaka ; fedheha ya kukataliwa kuripoti kesi hiyo eti kwa kuwa tulikuwa hatuna kibali!
Kadhia hiyo ilitukuta wakati tukifuatilia moja ya kesi ya wizi wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu (BoT) sh milioni 207 inayomkabili mweka hazina wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kigoma, Shaban Maranda, na wenzake watatu, ambayo ilikuwa inaanzaa kuunguruma kwa mara ya kwanza.

Fedheha hiyo ilitupata saa 8:42 mchana pale Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Addy Lyamuya, ambaye alikuwa ameketi katika kiti chake cha enzi.

Akisaidiana na hakimu mkuu mkazi ambaye ni Katibu wa Jaji Mkuu, Egnas Kitusi, na Hakimu Mkuu Mkazi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, John Utamwa, na kwa mara ya kwanza tangu mahakama hiyo ianze kusikiliza kesi za EPA, walikuwa wakisikiliza kesi hiyo kwa kutumia vipaza sauti na kompyuta za mkononi ‘Laptop’.

Mbali na Maranda, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Madeni ya Benki Kuu ya Tanzania, Iman Mwakosya, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo hicho, Anna Komu na mwanasheria wa benki hiyo, Bosco Kimela.

Kama ilivyo ada kwa sisi waandishi tunaoripoti habari za mahakamani tulifika mapema asubuhi, tayari kwa ajili ya kuanza kuwasikiliza mashahidi wa upande wa mashtaka, wakianzia na Peter Noni na kisha turejee maofisini kuipasha jamii habari zilizojiri katika kesi hiyo .

Ilipofika saa tano asubuhi wanahabari waliingia chumba namba mbili cha mahakama hiyo na kuanza kufuatilia shauri hilo ambalo liliahirishwa kwa mara mbili mfululizo na ilipotimu saa nane waandishi wote tulitakiwa kutii amri ya Lyamuya, ambayo awali ilitaka watu wote warejee kwenye chumba hicho tayari kwa kuipokea hati mpya ya mashtaka ambayo awali iliamriwa upande wa serikali ukaifanyie marekebisho.

Saa 8:11 tuliingia katika chumba hicho na wakili mwandamizi wa serikali Fredrick Manyanda ambaye aliwasomea mashtaka sita washtakiwa hao kwa mujibu wa hati ya mashtaka waliyoifanyia marekebisho.

“Jopo hili limekubaliana na hati mpya na kwa sababu hii, shahidi wa upande wa serikali apande kizimbani aanze kutoa ushahidi, ila wanahabari wekeni peni zenu chini, kwani hamna kibali cha mahakama cha kuripoti kesi hii…hivyo ni marufuku kuripoti kesi hii bila kuwa na kibali,” aliamuru Lyamuya.

Baada ya hakimu Lyamuya kutoa amri hiyo, shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo namba 1162 ya mwaka jana, Peter Noni , ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Mpango Mkakati wa BoT, alipanda kizimbani na kuapishwa na wakili wa serikali, Mganga Biswalo, kabla ya kuanza kutoa ushahidi wake.

Kutokana na hali hiyo, wanahabari tulitoka nje ya mahakama na kuelekea kwenye viwanja vya mahakama kwani uamuzi huo ulitukera kama si kutuchefua.

Kama kweli nchi yetu ina sheria inayopiga marufuku mwandishi kuandika wakati kesi inaendelea bila ya kuwa na kibali, basi mtakubaliana nami kwamba Lyamuya naye ameshiriki kikamilifu kuwasaidia waandishi wa habari kuivunja sheria hiyo.

Nasema ameshiriki kuivunja sheria hii kwa sababu siku hiyo aliwaona waandishi wakiandika mwenendo wa kesi hiyo tangu asubuhi na pia kuna kesi nyingine za EPA zinazowakabili washtakiwa wengi lakini siku zote amekuwa kimya.

Pia kuna kesi nyingine ambazo zipo mbele yake rekodi zake tunazo , waandishi tumekuwa tukirekodi mwenendo wa mashauri ya kesi hizo na alikuwa akituona lakini hakuwahi kutoa amri kama hiyo.

Kwa hiyo kama siku zote hizo alikuwa anatuona tulikuwa tukiivunja hiyo sheria ambayo hataki kuweka wazi ni sheria namba ngapi bali anaishia kusema hiyo ni sheria ya nchi, nadhani anastahili kuadhibiwa na mabosi wake kwa sababu miaka nenda rudi amekuwa kimya juu ya sheria hiyo.

Na kama sheria hiyo ipo basi kuanzia Jaji Mkuu Agustino Ramadhani, aliekuwa Jaji Kiongozi, Salum Masati, Jaji Laurian Kalegea, Jaji William Mandia, majaji na mahakimu wengine nao tunasema wameshiriki kikamilifu kutusaidia sisi wanahabari kuivunja sheria hiyo kwani tumekuwa tukiingia kwenye kesi wanazoziendesha na kurekodi mwenendo wa kesi hizo bila ya kupata kibali cha mahakama.

Tujiulize Jaji Mkuu na majaji wenzake ambao wanaruhusu wanahabari kuripoti mwenendo wa kesi bila ya kibali je ni wadhaifu wa kusimamia sheria za nchi kuliko hakimu Lyamuya?
Pia tujiulize hakimu Lyamuya ni makini? Kwani kama Lyamuya ni makini alipaswa kuwaondoa wanahabari kabla ya shauri hilo kuanza.

Au viongozi ambao wameapa kulinda Katiba na Sheria za nchi wanafaidika kwa namna moja au nyingine kwa ufunjifu wa sheria hiyo hadi wakati mwingine wanafumbia macho wanahabari wanaoivunja sheria hiyo?

Ni Lyamuya huyu huyu wiki iliyopita tulifika ofisini kwake tukamweleza kuwa tunataka kujua ombi la Katibu Mkuu Mstaafu, Gray Mgonja, la kutaka aruhusiwe kutoka nje ya Dar es Salaam limefikia wapi; alisema alikuwa anampatia jalada karani wake atupeleke kwa Hakimu Henzron Mwankenja ndiye angetupa taarifa na kusema tayari jalada hilo alikuwa amelishughulikia kiutawala.

Nimuulize Lyamuya wakati anatupa jibu hilo na kutukabidhi karani wake atupeleke kwa Mwankenja mbona hukutudai vitambulisho?

Ni huyu huyu Lyamuya, mara kadhaa sisi waandishi tunaoshinda mahakamani hapo kuripoti kesi mbalimbali, tumekuwa tukimfuata kupata ufafanuzi kuhusu baadhi ya kesi na amekuwa mgumu kutupa ushirikiano!

Akiamua kutoa ushirikiano anatoa huku akitoa sharti kwamba mwandishi mmoja ndiyo aingie kuzungumza naye kwa niaba ya waandishi wa vyombo vya habari. Siyo siri baadhi ya watendaji wa mahakama hiyo wamekuwa wakilalamikia utendaji wake.

Je haya siyo matumizi mabaya ya madaraka? Maana tusiishie kuwafikisha wakina Basil Mramba na Daniel Yona kwa shtaka la matumizi mabaya ya ofisi ya umma wakati kuna watumishi wa umma wanatumia madaraka yao vibaya kwa kukataa kutoa ushirikiano kwa wanahabari.

Ieleweke wazi waandishi wa habari katika hili hawataki kutunishiana misuli na Mahakama ya Tanzania.Tunaheshimu na kuipenda mahakama yetu.

Ila tunachotaka kuona uongozi wa Mahakama unatengeneza mara moja vitambulisho maalum kwa ajili ya waandishi wanaofika kila siku katika mahakama zetu zote na kuripoti kesi mbalimbali ambazo wananchi wana haki ya kikatiba kujua kinachoendelea katika mashauri hayo na si vinginevyo.

Siyo utaratibu usiotekelezeka ulitolewa juzi na Lyamuya wa kuwataka wanahabari eti kila watakapotaka kuingia kwenye kesi hata kama ni zaidi ya tatu waende kwa mahakimu husika na kujiorodhesha. Nasema utaratibu huu hautekelezeki katika zama hizi za utandawazi.

Hivi kitendo cha Lyamuya cha kuwatoa waandishi wa habari siku ile bila kuwaeleza utaratibu hata kama kilikuwa ndani ya sheria pia kilitudhalilisha waandishi wa habari mbele ya hadhara iliyokuwa imefurika katika mahakama hiyo, kwani tulionekana si chochote katika ujenzi wa taifa.
Lyamuya fahamu kuanzia sasa sisi wote tunajenga nyumba moja hivyo hatuna sababu ya kugombea fito.

Natoa changamoto kwa Lyamuya kufungua milango wazi kwa wanahabari na kutoa ushirikiano wa hali na mali pale unapohitajika kufanya hivyo.

Kwani pamoja na mashauri mengine kuwepo mahakamani hapo lakini kwa sasa Watanzania wengi macho na masikio yameelekezwa kwenye mahakama hiyo ya Kisutu anayoingoza kujua hatima za kesi hizo hivyo atakaposhindwa kutoa ushirikiani atakuwa anawapa wakati mgumu wanahabari.

Na endapo atafanya hivyo atakuwa amemaliza ile minong’ono ya chini chini inayotolewa na baadhi ya watendaji wa mahakama hiyo dhidi yake kwamba amekuwa ni kero katika utendaji wa mahakama hiyo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa 23 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.