MITONDOO MAHABUSU HADI LINI?
Na Happiness Katabazi
JESHI la Polisi chini ya uongozi wa Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, limepiga hatua kubwa kimaendeleo, jambo ambalo limetia moyo wananchi ambao walishaanza kuliona kama jeshi linaloshirikiana na wahalifu.
Kwa uchache, mafanikio ya Jeshi la Polisi yapo wazi. Tunawaona baadhi ya viongozi wa juu wa jeshi hilo wanavyoumiza vichwa kuwahimiza wananchi washiriki kikamilifu katika ulinzi wa polisi shiriki, ukarabati wa baadhi ya vituo vikubwa vya polisi, kuruhusu askari wengi kwenda vyuo vya elimu ya juu kuongeza elimu, pia kutoa semina na mafunzo mbalimbali kwa askari wa jeshi hilo.
Pia katika awamu hii ya uongozi wa Mwema, jeshi hilo kila wakati limekuwa likijitahidi kuelimisha wananchi watambue kuwa ni jeshi lao na wanalo jukumu la kushirikiana nalo kikamilifu katika mustakabali mzima wa kujenga taifa letu na wananchi kutambua haki zao pindi wanapokamatwa na polisi.
Binafsi ninalipongeza Jeshi la Polisi pamoja na viongozi wake wote kwa mafanikio hayo na ninalitaka lisibweteke na badala yake likaze buti sambamba na kuendelea kuwafunda askari wake ili waweze kufanya kazi yao kisayansi zaidi.
Turejee kwenye mada ya leo ambayo nitazungumzia matumizi ya mtondoo kwenye vituo vingi vya polisi nchini. Watanzania wengi tumezoea kusikia kwamba matumizi ya mtondoo kwa mahabusu na wafungwa, yapo kwenye magereza yetu hapa nchini.
Na wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakiipigia kelele hali hii na kwa kiasi fulani kilio hicho kimeweza kuzaa matunda, kwani inaelezwa kwamba baadhi ya magereza yetu yametengenezewa vyoo, hivyo mahabusu na wafungwa wanatumia vyoo badala ya mitondoo.
Kila kukicha mamlaka husika zimekuwa zikiifungia migahawa isiyo na vyoo kwa maelezo kuwa inaweza kusababisha kukatokea magonjwa ya milipuko.
Lakini hata siku moja hatujasikia mamlaka hizo hizo zinazosimamia sekta ya afya nchini zikithubutu kulinyoshea kidole Jeshi la Polisi au kuvifunga vituo vya polisi ambavyo mahabusu zake hazina vyoo. Huu ni unafki mkubwa!
Cha ajabu ni kwamba, askari polisi wanaowapokea watuhumiwa na kuwaweka mahabusu pia wanawaruhusu ndugu wa watuhumiwa hao kuwaletea chakula mahabusu hao.
Binadamu yeyote anapokula chakula na kunywa maji ni lazima atahitaji kwenda haja ndogo au kubwa.
Tuliulize Jeshi la Polisi, lengo lao ni nini hasa kuwachanganya binadamu pamoja na kinyesi chao?
Je, ni kutaka kuzalisha magonjwa ya milipuko katika mahabusu zetu au ndiyo wamekwisha kuwahukumu mahabusu hao kwamba hawana haki ya kupata huduma hiyo ya choo?
Mabwana na mabibi afya wakiifunga migawaha isiyo na huduma ya vyoo, wanasema kwamba huwezi kuwalisha watu halafu usiweke choo.
Sasa mbona askari wa vituo hivyo wanawaruhusu ndugu wa mahabusu hao kuwaletea chakula na vinywaji wakati mahabusu hazina vyoo?
Na mbona hatujasikia hao mabibi afya wakithubutu kuzifunga mahabusu hizo ambazo zinakusanya watu wa kariba mbalimbali huku wengine wakiwa na maradhi yao ambao mwisho wa siku wanajisaidia haja kubwa na ndogo kwenye ndoo?
Hakika huu ni unafiki mkubwa na haufai kuendelea kuvumiliwa.
Sote tunatambua kwamba hata watuhumiwa nao wana haki ya kupata huduma ya vyoo kama wananchi wengine wasio na hatia.
Tangu IGP Mwema aingie madarakani tunashuhudia vituo vikubwa vya polisi kama Oysterbay, Msimbazi, Kituo Kikuu cha Polisi, Buguruni na makao makuu ya jeshi hilo na vinginevyo vimefanyiwa ukarabati wa hali ya juu ambao umerejesha heshima za ofisi hizo, kwani ilikuwa imepotea kutokana na majengo hayo kuchakaa, lakini tunataka ukarabati huu usiishie kwenye vituo vikubwa, tunataka ushuke hata ngazi za chini, kwani huko ndiko kunakokuwa na mlundikano wa mahabusu wengi, wakiwemo wale wanaobambikiwa kesi na baadhi ya askari polisi ‘wachumia tumbo.’
Jeshi la Polisi linaweza kudai kwamba halina fedha za kutosha, sawa, tunaweza kulikubali hilo.
Kama ni hivyo. mimi nalishauri liendeleze ule utamaduni wake mpya wa kutembeza bakuli kwa wahisani, naamini litafanikiwa.
Kama wafanyabiashara wanalichangia mamilioni kwa ajili ya kununua magari na vikorokoro vingine vinavyolisaidia katika utekelezaji wa majukumu yake, naamini hawawezi kulichangia mabilioni kwa ajili ya kujenga vyoo kwa sababu wanajua fika kuwa ipo siku wao wenyewe au hata ndugu na jamaa zao wanaweza kuwekwa rumande na kukutana na hali ya sasa ya kunyea kwenye ndoo.
Lakini wakati Jeshi la Polisi likifanya hayo, ifike mahali wapanga bajeti wa serikali yetu waone haya na waongeza bajeti kwa Jeshi la Polisi ambalo ni taasisi nyeti inayoshughulika na raia moja kwa moja ili liweze kufanya kazi yake bila kutegemea misaada kutoka kwa wahisani.
Sote tunafahamu kwamba ‘huwezi kumfanyia madhila mfadhili wako’, hapa namaanisha kwamba endapo Jeshi letu la Polisi litageuka kuwa mnyonge wa kifedha na kusubiri kupokea ‘lawalawa’ kutoka kwa wafadhili, hivi kesho na kesho kutwa mfadhili huyo afanye uhalifu, uwe wa wazi au kwa siri, jeshi letu litakuwa na jeuri ya kumchukulia hatua?
Jeshi la Polisi ni la Watanzania wote, hivyo na sisi wananchi tunalojukumu la kuipigia kelele serikali ili iweze kuliongezea bajeti liweze kuachana na utegemezi wa wafadhili.
Kama tutafanikiwa katika hili, ninaamini tutakuwa na jeshi lenye meno ya kumng’ata mtu yeyote bila woga.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Januari 7 mwaka 2009

No comments:
Post a Comment