Header Ads

UNAFIKI UNADHOOFISHA UPINZANI

Na Happiness Katabazi

MTAWALA wa zamani wa Taifa la Urusi, Nikita Sergeyevich Khrushchev, aliwahi kutamka kwamba - wanasiasa wanafanana kote duniani. Wote wana hulka ya kuahidi kujenga daraja pasipo na mto.

Leo katika makala hii nimelazimika kutumia nukuu hiyo ili iweze kuunga mkono mada yangu ambayo nitazungumizia ahadi iliyowahi kutolewa na vyama vinne vya upinzani hapa nchini lakini hadi sasa ahadi hiyo imegeuka kuwa hewa.

Kwa wale wenzangu na mimi tunaofuatilia kwa karibu siasa za taifa hili, tutakumbuka Mei 5 mwaka 2007, Chama cha NCCR-Mageuzi, TLP, CUF na Chadema vilifanya mkutano mkubwa wa hadhara mkoani Morogoro.

NCCR iliwakilishwa na Mwenyekiti wake, James Mbatia, TLP mwenyekiti wake Agustine Mrema, Chadema iliwakilishwa na John Mnyika na Erasto Tumbo na CUF iliwakishwa na Maharagande.

Ilielezwa kimsingi sababu za vyama hivyo kwenda Morogoro kuwa ni kuzungumza na wananchi kuhusu elimu na mpango wa vyama hivyo wa kukusudia kuungana.

Viongozi wa vyama hivyo katika hotuba zao, waligusia masuala ya elimu ya juu na gharama zake na walikosoa utaratibu wa utoaji mikopo inayotolewa kwa madaraja na kutofautina kwa viwango vya karo kutoka shahada moja hadi nyingine.

Shahada ya Uhandisi karo yake ni kubwa kuliko Shahada ya Sheria na shahada ya Sheria ni kubwa kuliko Shahada ya Elimu.

Waliukosoa waziwazi utaratibu huu kuwa unaweza kusababisha watu wenye uwezo pekee kusomesha watoto wao na pia unaweza kusababisha watu wakimbilie kusoma shahada ya bei nafuu.

Katika kuzungumzia hoja hizo pia waligusia mambo mbalimbali na walihitimisha kwa hoja ya nini kifanyike kufuatia kushindwa kwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulifanyia wema taifa letu.

Ndipo viongozi hao ambao walikuwa wakiwakilisha vyama vyao walipobainisha bayana mpango walionao wakuviunganisha vyama hivyo vinne ili kuwa na chama kimoja chenye nguvu kitakachoweza kuing'oa CCM madarakani.

Mashuhuda wa mkutano huo mara baada ya tamko hilo kutolewa, wananchi walishangilia sana kuliko walivyoshangilia hoja zote zilizotolewa kwenye mkutano huo siku hiyo. Na baadhi ya wanawake waliokuwa wamevalia sare za chama cha TLP walikuwa wakiimba wimbo huu, 'asiyependa muungano wetu atapata laana'na kuungwa mkono na wanachama waliokuwepo uwanjani pale kuviwakilisha vyama vyao.

Hiyo iliikuwa ni ishara ya si tu kwamba wananchi wanaunga mkono hatua hiyo, bali hicho ndicho walichokuwa wanakitarajia siku nyingi toka kwa vyama vya upinzani hapa nchini.Viongozi hao wa vyama waliwaeleza wakazi hao kwamba watatimiza hilo ndani ya wiki moja.

Lakini siku tano baadaye Mei 10 mwaka 2007,Wenyeviti wa vyama hivyo vinne wakafanya mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Makao Makuu ya Chama cha CUF,Buguruni Dar es Salaam,na siku hiyo badala ya kutamka kile ambacho kimekusudiwa na matarajio ya wanachama na wananchi kwa ujumla walitamka kwamba hoja waliyonayo ni kushirikiana tu na siyo kuungana. Hata baada ya kutamka kwamba vitashirikiana, hadi sasa hakuna ushirikiano wa kweli miongoni mwa vyama hivyo zaidi ya unafki.

Pamoja na Katibu Mkuu wa CCM,Yusuph Makamba kuwa ni mtu mwenye hulka ya kujenga hoja dhaifu katika hoja za msingi, aliwahi kuufananisha uamuzi huo wa ushirikiano wa vyama hivyo vinne kwamba ni sawa na 'Paka waliofungiwa mikia pamoja wakiona maziwa kila mmoja atavuta mkia upande wake'.

Hakuna ubishi kwamba usemi huu wa Makamba umetimia kwani tumeshuhudia vyama hivi vikishindwa kushirikiana na hiyo ilidhihirika ulipotekea uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime na sasa Mbeya Vijijini tena kwa sababu zisizo na msingi.

Viongozi hawa wanapaswa kulaumiwa kwa kuwaangusha Watanzania kwasababu wameshindwa kuishi kwa mujibu wa matamko waliyoyatamka ambayo waliyasaini wenyewe. Na kwa kulinyima taifa uwezekano wa kuwa na chama kimoja chenye nguvu kitakacholeta ushindani wa kweli na CCM.

Viongozi hawa wanathibitisha pasipo shaka kupitia suala hili kwamba, kwa ubinafsi walionao, uongo walionao, ulafi wa madaraka walionao, undumilakuwili, uzandiki na kwa unafiki walionao, hawafai kupewa dhamana ya kuliongoza taifa hili.

Laiti kama wanafikiri wanatafuta kupewa ridhaa ya wananchi kuliongoza taifa hili,toba yao iwe kulisafisha kosa walilolifanya la kuwadanganya wananchi kwamba wanaungana kumbe kanyaboya!

Katika kuendesha huu ushirikiano wa vyama hivyo vinne viliunda kitu kinaitwa Kamati ya Ufundi, ambayo awali ilikuwa ikifanya vikao vyake mara moja kwa mwezi lakini tangu vilipokorogana kwenye uchaguzi mdogo wa Tarime hadi sasa, kwa mujibu wa taarifa za ndani toka kwa vyama hivyo ,haijawahi kuketi tena. Na Kamati hii ilikuwa ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara,Wilfred Lwakatare.

Ni vyama hivi hivi kila kukicha vimekuwa vikiibeza serikali ya CCM tangu awamu iliyopita hadi sasa kwamba imeshindwa kazi na kutekeleza ahadi zake. Ni kweli kuna ahadi nyingi chama tawala kimeshindwa kuzitekeleza, lakini vyama hivyo vinne jambo hili moja lisilohitaji gharama bali utashi, limewashinda. Umefika wakati Watanzania wote kwa ujumla tujiulize hawa watawezaje kutekeleza mambo mazito ya kitaifa?

Katika hali ya namna hii viongozi wa vyama vya upinzani watakwepaje tuhuma za wao kuwa ni mapandikizi ya CCM na wapo kwa ajili ya kuvuruga upinzani au kuendeleza ile dhana kwamba Tanzania hakuna upinzani wa kweli ila ni usanii?.

Umefika wakati wa Watanzania kuanza kuwapima kwa kauli zao na matendo yao baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani. Je wana moyo wa dhati wakuleta mageuzi ya kweli katika taifa letu au wanaliletea unyang'au?

Ninamalizia kwa kusema kwamba naheshimu mchango mkubwa wa mapinduzi ya kifikra, uthubutu wa kuikemea na kuikosoa serikali na vyombo vyake ambao umetolewa na vyama vya upinzani hapa nchini sambamba na kuibua maovu, lakini hilo lisiwe kigezo kwa wananchi kushindwa kuvinyooshea vidole vyama vya upinzani vinapokosea au vinapotoa ahadi visitimize.

Hivyo hii ni changamoto kwa vyama vyote vya upinzani kwamba wakiacha unafiki na undumilakuwili,tamaa ya madaraka na fedha wanaweza kuleta mageuzi ya kweli.

Kwahiyo nukuu hiyo ya mtawala wa taifa la Urusi,katika makala hii imetufundisha kwamba kumbe hata wapinzani ni sawa na wanasiasa wa CCM ambao wamekuwa wakitoa ahadi lukuki mara kwa mara lakini mwisho wa siku hawazitekelezi,hivyo wananchi wenzangu nukuu hiyo inatufundisha kwamba tuwe makini na ahadi zinazotolewa na wasiasa wetu kwani uongo ndiyo hulka yao.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 14 mwaka 2009.

No comments:

Powered by Blogger.