Header Ads

SHAHIDI AMSHUSHIA MZIGO MAREHEMU BALLALI

*Adai alikuwa na utaratibu mbaya wa malipo ya EPA
*Adai alikuwa akitoa maagizo ya malipo kwa mdomo
*Ni Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Mkakati BoT
*Naibu Msajili BRELA naye atoa ushahidi mzito kortini

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa kwanza katika kesi ya wizi wa sh milioni 207 katika Akanuti ya Madeni ya Nje (EPA), mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daudi Ballali, alikuwa na utaratibu mbaya wa kulipa madeni ya fedha za EPA.

Shahidi huyo ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Mkakati wa BoT, Peter Noni, alieleza hayo jana mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi, Addy Lyamuya, wakati akijibu swali la wakili wa utetezi, Mabere Marando. Mawakili wengine wa upande wa utetezi ni Majura Magafu na Masaki Masatu.

Alidai utaratibu ambao haukuwa rasmi ambao walikuwa wakiutumia ni kwa wadeni kwenda kuona na Gavana wa BoT, Ballali, kisha gavana huyo kuyapeleka madai hayo kwa katibu wa benki kwa ajili ya kuhakikiwa na baadaye kupekekwa kwake (Noni) ambaye wakati huo alikuwa Mkurugenzi wa Uchumi na Sera na alikuwa akipendekeza madeni hayo yalipwe na kurudishwa tena kwa gavana kwa ajili ya kulipwa.

“Wakati mwingine madeni hayo yalikuwa yakilipwa kwa shinikizo la wanasheria wa wadai na Gavana (Ballali), alikuwa akitoa maagizo yasiyo ya kimaandishi kwa watendaji husika akidai walipwe haraka, ili benki isipate aibu ya kuburuzwa mahakamani na wadeni hao,” alidai Noni.

Hata hivyo, alidai wakati serikali inapata uwezo wa kulipa madeni hayo, BoT ilikuwa ikitumia programu nne tofauti za kulipa madeni, ambazo zilikuwa zikitumika miaka ya 1986 -2002 na baada ya kipindi hicho hapakuwepo programu rasmi ya kulipa madeni, ila madeni ya EPA yaliendelea kulipwa bila utaratibu rasmi.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya mawakili wa utetezi na shahidi Noni:

Wakili: Nitakuwa sahihi nikisema washtakiwa wa pili, wa tatu na wa nne walikuwa wakitekeleza maagizo ya Ballali kwa kulipa madeni hayo?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Kwa kuwa hakukuwa na taratibu rasmi, hivi mdai alikuwa anafikisha malalamiko yake wapi?
Shahidi: Kwa gavana ambaye kipindi hicho alikuwa ni Daudi Ballali, ambaye kwa sasa ni marehemu.
Wakili: Mbali ya Gavana, hakukuwa na ofisa aliyekuwa anamsaidia kazi hiyo gavana?
Shahidi: Alikuwa ni Naibu Gavana.
Wakili: Ni nyaraka zipi ambazo mdai alitakiwa kuziwasilisha kwa Gavana au Naibu wake?
Shahidi: Barua ya kuomba kulipwa na uthibitisho wa deni.
Wakili: Ni kitu gani kiliisaidia BoT kutambua mdai anayestahili kulipwa?
Shahidi: Tulitumia data base za NBC.
Wakili: Hizi data base zilikuwa chini ya nani?
Shahidi: Chini ya Kurugenzi ya Uchumi na Sera ya BoT ambayo mimi nilikuwa naingoza.
Wakili: Baada ya madeni, ombi la kulipwa deni kuhakikiwa na Idara ya Madeni, yalikuwa yanapelekwa wapi?
Shahidi: Kwanza yalikuwa yanapelekwa kwa Sekretari wa benki, kisha kwa gavana.
Wakili: Huyu sekretari ana kazi gani?
Shahidi: Ni mtaalamu wa sheria.
Wakili: Katika ushahidi wako uliotoa ulisema umekoma kuwa Mkurugenzi wa Uchumi na Sera Machi, mwaka 2005, nani alirithi nafasi yako?
Shahidi: Issac Kilato.
Wakili: Inawezekana mtu akaleta deni bila kupitia huo mlolongo?
Shahidi: Haikuwa kawaida.
Wakili: Hamkuona huo utaratibu usio rasmi wa kulipa madeni ungehatarisha Benki Kuu?
Shahidi: (kimya).
Wakili: Unaweza kukumbuka idadi ya watu waliolipwa?
Shahidi: Sina kumbukumbu.
Wakili: Mteja wangu, Anna Komu alinieleza kwamba hata wewe unafahamu kwamba yeye hakuwa na mamlaka ya moja kwa moja ya kuidhinishwa kulipwa kwa deni? Kweli?
Shahidi: Ni kweli.
Wakili: Pia Komu alinieleza kwamba mwaka 2004 wewe hukuridhika na utaratibu usio rasmi wa kulipa madeni ya EPA na ulimshauri gavana uundwe uratibu mpya ambao utatumika kulipa madeni, lakini gavana alikukatalia?
Shahidi: Eeh…ni kweli nilikuwa na nia hiyo, lakini nilimweleza gavana katika mazungumzo, lakini sikuwa nimeweka nia hiyo kwa maandishi.
Wakili: Una ushahidi wowote kwamba kuna wadeni waliwasilisha moja kwa moja maombi yao kwa mshitakiwa wa pili, wa tatu na wa nne, ili walipe deni?
Shahidi: Sina ushaidi huo.
Aidha, shahidi wa pili katika kesi hiyo, ambaye ni Naibu Msajili wa BRELA, Andrew Mkapa, alipanda kizimbani majira ya saa tisa alasiri akiongozwa na wakili kiongozi wa serikali, Stanslaus Boniface, kutoa ushaidi wake ambapo aliithibitishia mahakama hiyo kwamba Kampuni ya Rashhaz (T) Ltd ilisajiliwa kwenye ofisi anayoingoza.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili huyo na Mkapa:
Wakili: Nani wakurugenzi wa kampuni hiyo?
Shahidi: Wakati inasajiliwa Septemba 12 mwaka 2003, wakurugenzi walikuwa ni Rajabu Shaaban Maranda na Maranda Rajab Maranda, ambao pia ni wanahisa wa hiyo kampuni.
Wakili: Katika anwani yao ya makazi walisema wanaishi wapi?
Shahidi: Wakurugenzi wote wanaishi Mbezi Beach - Kitalu namba 24 W-Tangibovu.
Wakili: Walieleza BRELA ofisi yao ipo wapi?
Shahidi: Walieleza kwenye jalada la kusajili hiyo kampuni kwamba ofisi yao ipo Tangibovu, House of New BP.
Wakili: Alisema baadaye kampuni iliwasilisha fomu namba 14 ambayo inatolewa na ofisi yetu inayoonyesha mabadiliko ya wakurugenzi na kwamba Mkurugenzi mpya anaitwa Jaffer Hussein Jaffer na aliteuliwa kushika wadhifa huo Desemba 8 mwaka 2003 na walituambi Jaffer ni Mtanzania anaishi Mburahati kitalu 606, NHC, Dar es Salaam.
Wakili: Tangu kampuni hiyo isajiliwe ilishawahi kuwasilisha ripoti ya mahesabu ya mwaka ya kampuni?
Shahidi: Haijawahi kuwasilisha.
Wakili: Kisheria kama kampuni haiwasilishi ripoti hiyo ya mwaka, mnaichukuliaje?
Shahidi: Tunaichukulia kuwa ni dormant.
Wakili: Katika majukumu ya hiyo kampuni waliyoyainisha kuyafanya, kuna sehemu inaonyesha watakuwa na jukumu la kukusanya madeni?
Shahidi: Hapana.
Hakimu Lyamuya aliahirisha kesi hiyo hadi leo na kuutaka upande wa mashitaka kumleta shahidi wa tatu, ili shahidi wa pili atakapomaliza kuhojiwa na mawakili wa utetezi, shahidi wa tatu aweze kutoa ushahidi wake.
Kesi hiyo inamkabili Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma, Rajab Maranda na maofisa wa BoT, Iman Mwakosya, Anna Komu na Bosco Kimela, ambao wanadaiwa kuiibia benki hiyo jumla ya sh milioni 207.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Januari 23 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.