Header Ads

MBATIA UPO SAHIHI,TUUNDE TUME

Na Happiness Katabazi

TAIFA linapoingia kwenye giza la ufisadi, inawezekana watu wakaamini kwamba kila mtu ndani ya taifa hilo ni fisadi.Kwa kufananisha na msemo ule ule kuwa “Samaki mmoja akioza basi wote wameoza ndani ya tenga”.

Ukitafakari kwa kina msemo huu utapingana nao kwani si rahisi samaki mmoja akioza ndani ya tenga basi wote wawe wameoza.

Nimelazimika kutumia msemo huu kwa kuwa ninataka kuangalia upande wa pili wa shilingi, hasa tunapoangalia mafisadi waliopo ndani ya nchi.

Nchi inapokuwa na mafisadi haimaanishi basi watu wote waliopo ndani ni mafisadi, kwani ufisadi ni uovu na ushetani.

Tunajua, raia wengi ni watu wema wanaoamka asubuhi kwenda kwenye shughuli zao halali bila kufanya ufisadi.

Lakini ufisadi unapofikia viwango vya kutumia vyombo vya dola na taasisi za umma, basi ufisadi huo ni mkubwa kupindukia na unaitwa ufisadi kabambe, kwa Kiingereza (grand corruption).

Sasa mbinu za kupambana na ufisadi wa aina hii huwa hazipo katika sheria za nchi, kwa kuwa baadhi ya sheria za nchi hutumika kuufanikisha ufisadi kabambe.

Mfano, ufisadi kabambe unaotumiwa na vyombo vya dola unaanzia kwenye sera ambazo zinaongoza serikali katika utendaji wake wa kila siku.

Sera ikishabuniwa, hata ikiwa potofu, ikatungiwa sheria na ikapitishwa na Bunge, ambalo ndilo chombo kilichopewa jukumu la kutunga na kusimamia sheria, huwa ni halali.

Kwa hiyo ukichukua sera ya kuuza nyumba za serikali kuwa ni wazo potofu lililoingia kwenye vichwa vya watawala wa nchi hii, basi wazo hilo lilipokubaliwa na dola, limefanikishwa kisheria na watendaji wa serikali wakauziwa nyumba za serikali.

Sera haijali nani amenunua nyumba hizo, lakini ukweli ni kwamba uuzaji wa nyumba za serikali ni ufisadi.

Ni kitendo cha kulinyang’anya taifa rasilimali yake iliyokusudiwa kuwahifadhi watendaji wa serikali wanapokuwa kwenye ajira za umma.

Matokeo yake ni kwamba nyumba hizo huuzwa kwa bei hafifu, japo zina thamani kubwa, jambo ambalo ni wizi kwa kila anayenunua nyumba hizo.

Lakini wafanyakazi wa serikali wenye stahili ya kupata nyumba kama vile majaji wanajikuta wanapanga kwenye hoteli za kitalii kwa gharama kubwa zinazolipwa na serikali.

Mzigo huo wa kulipa gharama za watendaji hao anatwishwa mlalahoi ambaye kila kukicha anakamuliwa kwa kodi mbalimbali.

Huu ni mfano wa wazi wa serikali ovu. Je, wale wote wanaoguswa na sera hii ama kwa kutunga ama kwa kunufaika nayo tuwaiteje? Mafisadi au manyang’au?
Hapo ndipo ninapounga mkono wazo la Chama cha NCCR-Mageuzi lililotolewa na Mwenyekiti wake, James Mbatia, katika tamko la chama hicho Januari 11 mwaka huu, kwamba yapo mambo ya kifisadi ambayo ufumbuzi wake unahitaji Tume ya Ukweli na Maridhiano ‘Truth Commission’.
Tume hiyo iwe na watu wachache, wasafi, wasio na masilahi katika ufisadi husika, watakaopewa mamlaka na sheria ya kuchunguza ufisadi wa aina hii ambao umeelekezwa kwa kutumia dola na sheria zake.

Tume kama hiyo itakuwa na mamlaka ya kuwaita watuhumiwa ili waeleze ukweli na pia wasio tuhumiwa kuja mbele ya tume hiyo kuthibitisha ukweli na kisha kuainisha uovu uliotendeka na kuupatia ufumbuzi.

Wengine japo ni watuhumiwa watahitajika kukubali uovu wao japo kama walipotenda ulikuwa halali kisheria, wakishakiri, sheria iwape fursa ya kuomba msamaha kurejesha mali ya umma na pengine kufidiwa kama itaonekana inafaa.

Tuone jinsi tutakavyowafidia watendaji wetu wawili walioguswa na sera za uuzaji wa nyumba.
Mtu wa kwanza ni ofisa wa serikali aliyeomba kununua nyumba ya serikali na ikathaminishwa kuwa ina thamani labda ya sh milioni 50, ofisa huyo akakubali na kuinunua nyumba hiyo.

Mtu huyu anastahili kuombwa radhi katika tume hiyo kwamba ameuziwa nyumba kwa sera mbovu ambayo ni kinyume cha masilahi ya nchi.

Kwa hiyo yeye akubali kurejesha nyumba ile na akubali kupokea sh milioni 50 na kifuta jasho.
Kwa lugha nyingine, huyu si fisadi, huyu ni mhanga ‘victim’ wa sera ya kifisadi.

Lakini mfano, mtendaji wa pili wa serikali hapa tumchukulie katibu mkuu wa wizara anayechukua fedha za serikali sh milioni 600 kukarabati nyumba ya serikali anayoishi na kisha kujiuzia nyumba hiyo kwa sh milioni 50.

Huyu ni fisadi, tena dawa yake Tume ya Ukweli na Maridhiano ikishagundua ukweli huo ni kupeleka ukweli kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ili aweze kumuandalia mashtaka na kumfikisha mahakamani ili ahumiwe kwa kosa la kuiba mali ya umma.

Na hilo ndilo pendekezo la Mbatia, licha ya baadhi ya watu kutokumuelewa vyema wakaishia kuibuka kwenye vyombo vya habari kumpinga.

Kwamba wapo watu itabidi wapelekwe mahakamani na sheria ya ufisadi itungwe kuhakikisha watu wa aina hii wanapata adhabu.

Sasa wanaompinga Mbatia ni kina nani? Na je, waliompinga walipata fursa ya kuisoma hotuba ya Mbatia kwa kina au waliamua kumkosoa bila kurejea hotuba yake aliyoitoa kwa maandishi?

Au waliamua kumkosoa baada ya baadhi ya magazeti kuripoti kwamba Mbatia anataka mafisadi wasamehewe?

Tujenge utamaduni wa kujenga hoja kwa vielelezo, hivyo mtu mwenye akili timamu anapotaka kumkosoa mtu kwanza ni lazima ajiridhishe na hoja anazotaka kuzitoa dhidi ya mtu huyo ili mwisho wa siku asionekane kichekesho mbele ya jamii.

Tanzania ni yetu sote na tuendelee na utamaduni wetu wa kukosoana kwa hoja na kupongezana panapostahili na si kukurupuka kama baadhi yetu wanavyofanya.

Tusipojirekebisha tutakuwa tukijenga taifa la wachochezi na majuha.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano la Januari 28 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.