Header Ads

MRAMBA AANDALIWA MAPOKEZI MAZITO

*Mahakama yamruhusu kutembelea jimbo

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa ruhusa kwa Mbunge wa Rombo, anayekabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia taifa hasara ya mabilioni ya fedha, Basil Mramba, kutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa siku 29 kwenda kuwasalimia wananchi jimboni mwake.

Kutokana na ruhusa hiyo, Mramba sasa anatarajia kwenda jimboni kwake kesho ambako inaelezwa kwamba ameandaliwa mapokezi makubwa kutoka kwa wapiga kura wake kwa lengo la kumpa pole kwa matatizo yaliyomfika.

Diwani wa Kata ya Kelamfua Makola, Kata ya Mkuu Rombo, Festo Kilewe, aliiambia Tanzania Daima kuwa Mramba aliyekuwa rumande kwa kesi hiyo na baadaye kuachiwa kwa dhamana, ameandaliwa mapokezi makubwa na atafanya ziara katika kata za jimbo lake kuhamasisha shughuli za maendeleo.

Mipango hiyo imethibitishwa pia na msaidizi wa mbunge huyo, Roman Kilega, ambaye alisema Mramba atakuwa na ziara ya siku nne, ambapo ataanzia Kata ya Tarakea na Useri kuhamasisha ujenzi wa madarasa ya shule pamoja na kuangalia maendeleo ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Tarakea hadi Mkuu Rombo na kutoka Mkuu Rombo hadi Marangu.

“Kwa vile mahakama imetoa ruhusu hiyo leo (jana), tunatarajia atawasili hapa kati ya Ijumaa na Jumamosi na wapiga kura wake wamejiandaa kumpokea kwa kishindo ili kumpa pole,” alisema Kilega.

Uamuzi wa kumruhusu Mramba kwenda jimboni mwake, ulitolewa jana na mahakama hiyo kutokana na ombi la Mramba lenye kumbukumbu namba 10RCA/A1/64/2009, lililowasilishwa Ijumaa iliyopita na wakili wake, Hubert Nyange na Peter Swai, kutaka aruhusiwe kwenda jimboni kuwasalimia wapiga kura wake.

Akitoa uamuzi huo jana, Mwankenja alisema, amezingatia ibara ya 13(6)(B), inayotamka kwamba mtu asichukuliwe kuwa ana hatia hadi mahakama itakapomkuta na hatia na ibara ya 17 ya katiba ya nchi, inayosema kila mtu ana haki ya kutembea.

“Kwa kuzingatia ibara hizo za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, mahakama inakubaliana na ombi la Mramba kwa sababu bado hajakutwa na hatia, pia ana haki ya kutembea ili mradi asivunje sheria za nchi, na kwa sababu hiyo kuanzia sasa mshitakiwa anaruhusiwa kutoka nje ya mkoa huu.

“Pia niliipitia kwa kina sheria ya Bunge la Tanzania kabla ya kutoa uamuzi huu, kuona mbunge anayeshitakiwa mahakamani kwa kesi za jinai, anatakiwa atendeweje, nimebaini sheria hiyo haisemi chochote katika hilo, hivyo nimetoa uamuzi wangu kwa kutumia ibara hizo nilizozitaja ambazo zipo kwenye katiba ya nchi,” alisema Mwankenja.

Ijumaa iliyopita Mramba kupitia mawakili wake aliwasilisha ombi mahakamani hapo akitaka aruhusiwe kutoka nje ya Dar es Salaam kuanzia Januari 3 hadi Februari mosi mwaka huu.

Ruhusa hiyo itamwezesha pia mbunge huyo kuhudhuria mkutano wa Bunge unaotarajia kuanza Januari 27, lakini pia huenda akalazimika kuomba muda mwingine kwani kwa ruhusa ya sasa, ana uwezo wa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa siku sita kabla ya muda aliopewa wa Februari mosi kumalizika.

Mramba ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya jinai namba 1200 ya mwaka jana, ambapo anashitakiwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.

Mramba aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati wa utawala wa Awamu ya Nne pamoja na Yona na Mgonja, wanakabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

Ilidaiwa kuwa kwa makusudi au kwa kushindwa kuchukua tahadhari kwa mujibu wa taratibu za kazi, akiwa Katibu Mkuu Hazina na wakiwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu waliruhusu kutolewa kibali cha serikali kilichoisaidia Kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation kutolipa kodi, tofauti na mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA), uamuzi ambao uliisababishia serikali hasara ya sh 11,752,350,148.00.

Wakati huo huo, Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Addy Lyamuya, amesema Januari 16 mwaka huu, atatoa uamuzi wa kukubali au kutokubali mtuhumiwa wa 21 wa wizi wa Fedha katika Akauti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jonathan Munisi, aunganishwe kwenye kesi inayomkabili ya mfanyabiashara Japhet Lema.

Lyamuya aliyasema hayo jana baada ya kusikiliza hoja za upande wa wakili wa serikali Fredrick Manyanda na wakili wa utetezi Evarist Mbuya ambapo upande wa utetezi uliomba mteja wao, aunganishwe kwenye kesi inayomkabili Lema kwa sababu mashitaka yake, yanafanana na yanayomkabili mteja wao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Januari 8 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.