Header Ads

'MADILU' AMKATAA HAKIMU

Na Happiness Katabazi

MTUHUMIWA wa kesi ya unyang’anyi wa kutumia nguvu, Ezekiel Matitu, maarufu kwa jina la ‘Madilu’, ambaye anadaiwa kukubuhu kuwapora na kuwajeruhi wanawake, jana aliwasilisha ombi la kutaka Hakimu Henzron Mwankenja ambaye anasikiliza hiyo kujiondoa.

Madilu aliwasilisha ombi hilo mbele ya Mwankenja katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na kueleza amelazimika kuwasilisha ombi hilo kwa sababu hana imani naye hakimu.

Mwenedesha Mashtaka, Abubakar Mrisha jana alileta shahidi wa mwisho katika kesi hiyo namba 1023 ya mwaka jana, ili aweze kutoa ushahidi, lakini ilishindikana baada ya hakimu Mwankenja kueleza majalada yote ya kesi yanayomkabili mshtakiwa huyo yameitishwa kwa Hakimu Mkuu Mfawidhi Addy Lyamuya.

“Ombi lako nimelipokea ila siwezi kulitolea uamuzi, pia shahidi hataweza kutoa ushahidi wake leo hadi majalada yatakaporudishwa, hivyo naahirisha kesi hadi Jumanne ijayo,” alisema Mwankenja.

Mapema Januari mwaka huu, baadhi ya mashahidi katika kesi hiyo, walidai mshtakiwa huyo ni mzoefu wa kufanya uhalifu huo kwa sababu anakabiliwa na kesi 11 za aina hiyo.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa huyo na wenzake wawili wanadaiwa kuwa Januari 29 mwaka jana, walimuibia Kasongo cheni za dhahabu za mkononi na shingo, simu mbili za mkononi vitu vyote vikiwa na jumla ya sh 1,140,000 na kabla ya kuiba alimtishia kwa silaha za jadi na kumjeruhi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Januari 24 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.