Header Ads

HUKUMU KESI YA ZOMBE


WOSIA WA JAJI MKUU AGUSTINO RAMADHANI,UMETIMIA

Na Happiness Katabazi

“IBARA ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatamka wazi kuwa mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano ni Mahakama na ibara ya 107B inasema mahakama zote zitakuwa huru katika utendaji wake na kuongeza kuwa ibara hiyo ndiyo chimbuko la uhuru wa mahakama nchini.


"Inatakiwa iwe huru na mamlaka ya utendaji (executive). Uhuru huu wa mahakama kama papa baharini ndio unaovuma sana na pengine unakera pia. Ni vigumu kuelewa vipi rais amteue mtu kuwa jaji halafu asiweze kumdhibiti kama amdhibitivyo waziri, lakini Katiba imetamka hivyo.

“Si hivyo tu, lakini ili kutenda haki kikamilifu, uhuru wa mahakama ni muhimu uwepo. Mahakama inapaswa iwe huru na umma au sehemu za umma, huhitaji hilo nalo pia ni muhimu sana, wananchi wanaweza kuamini kuwa mshitakiwa ni mhalifu kumbe mahakama imemuona ana hatia.

“Sasa mahakama isishinikizwe kumtia hatiani mtu ambaye hana hatia, uhuru ni muhimu sana katika nyakati kama hizi za tuhuma zilizokithiri za ufisadi, ambapo baadhi ya wananchi tayari wamekwisha kuwatia hatiani baadhi ya watuhumiwa hata kabla ya kufikishwa mahakamani:

“Kuna uhuru wa kila jaji au hakimu binafsi, hupatikana kwa kumthibitishia uhakika wa ajira yake. Jaji au hakimu ambaye ana wasiwasi na ajira yake.

“Hivi sasa limezuka tishio dhidi ya uhuru wa mahakama kutoka mhimili wa nne wa dola (vyombo vya habari), alibainisha kuwa havitofautishi kati ya ukweli (facts) na maoni.

“Baadhi ya vyombo huandika maoni kana kwamba ndiyo ukweli wenyewe, hali hiyo hupotosha wananchi na athari iletwayo haitibiki hata kwa shubiri.

“Kwa mfano, mgomo wa walimu ulipigwa marufuku na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Uamuzi huo ulifikishwa Mahakama ya Rufaa ambayo iliona kuwa suala halikuwa limewasilishwa kihalali mbele ya Mahakama Kuu. Hivyo shughuli yote mbele ya Mahakama Kuu ilifutwa,” maneno hayo mazito yalitamkwa Februari 5, mwaka huu na Jaji Mkuu Agustino Ramadhan, Siku ya Sheria nchini, sherehe zilizofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu, Barabara ya Kivukoni Front, Dar es Salaam, sherehe hizo ziliashiria mwanzo rasmi wa kazi za mahakama kwa mwaka huu.Binafsi nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari siku hiyo tuliyohudhuria sherehe hizo na kumsikia Jaji Mkuu akitoa maneno hayo kupitia hotuba yake ambayo ilibeba ujumbe mzito uliogusa hisia za wengi, hivyo kusababisha kila mara waliohudhuria sherehe hizo kumshangilia kwa makofi.

Niliporudi kwenye chumba chetu cha habari, nilimtafuta bosi wangu na kumweleza kuwa Jaji Mkuu, ametoa maneno mazito na nikamweleza bayana kuwa maneno haya mazito leo hii (siku hizo) tunaweza tusijue maana yake, lakini siku za usoni, maana halisi ya maneno hayo itaonekana.

Kimsingi bosi wangu alikubaliana na mimi kwamba maneno yaliyotamkwa na Jaji Ramadhan ni mazito na nikamweleza wazi kuwa tafrisi ya maneno haya itaonekana kwenye maamuzi ya mahakimu na majaji katika kesi zinazohusisha vigogo au watu wenye nyadhifa katika jamii, ambazo kesi hizo zimefunguliwa kwa wingi tangu Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani.

Nalazimika kuamini kuwa maana halisi ya maneno hayo mazito ya Jaji Mkuu, yameanza kuonekana Agosti 17 mwaka huu, baada ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, aliyekuwa akisikiliza kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake wanane, kutoa hukumu ya kushtusha.

Jaji Massati ambaye ni miongoni mwa majaji wanaoheshimika nchini na aliyejizolea umaarufu, akitoa hukumu yake alisema:

“Baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapa, nilibaini kuwa serikali imeshindwa kuithibitishia mahakama kuwa ni kweli washitakiwa wote waliwaua marehemu na kwa sababu hiyo nawaachilia huru washitakiwa wote.

“Na kwa kuwa mahakama hii imewaona washitakiwa si wauaji, hivyo kuanzia sasa naliagiza Jeshi la Polisi liende kuwasaka wauaji wa marehemu wale, na Zombe na wenzake waachiliwe huru.”

Jaji Massati, alisema kamwe mahakama haiwezi kumhukumu mshitakiwa kwa ushahidi dhaifu na wa kusikia kama uliowasilishwa mahakamani hapo, kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi.

“Mahakama haipo kwa ajili ya kuonea mtu kwa kumhukumu kwa ushahidi wa kusikia, ambao haukubaliki kisheria,” alisema Jaji Massati huku akionekana kujiamini.

Lakini kabla ya jaji kutoa hukumu hiyo, ebu niwakumbushe wasomaji , Juni 25, mwaka huu, upande wa serikali katika kesi hiyo, ulijigamba kuwa umethibitisha kesi hiyo pasipo shaka, hivyo kuiomba mahakama kuwatia hatiani washitakiwa hao kwa makosa waliyoshitakiwa.

Naye Jaji Massati baada ya kusikiliza majumuisho hayo ya upande wa serikali, aliwaasa wazee wa baraza, kutoa maoni yao kuhusu kesi hiyo kwa kuzingatia ushahidi ulio bora, uliowasilishwa mahakamani hapo na kutozingatia yale yaliyoripotiwa na vyombo vya habari, kwani yameandikwa mengi kuhusu kesi hiyo na kuongeza wingi wa mashahidi.

Kauli hii ya Jaji Massati kwa watu makini ambao walikuwa wakifuatia kesi hii tuliijadili kwa kina na kuona kwamba huu ni mtego mwingine wa vyombo vya habari katika hukumu ya kesi hiyo.

Licha ya mimi kuwa shahidi katika tume ya Jaji Mussa Kipenka, SACP- Sidnye Mkumbi na niliweza kutimiza wajibu wangu kama mwananchi wa taifa.

Kabla na baada ya hukumu ya kesi ya Zombe kutolewa tayari wananchi mbalimbali wakiwamo wasomi (majina na waifadhi) walikuwa wakinitumia ujumbe mfupi wengine wakinipigia simu wakati jaji akiendelea kusoma hukumu wakisema:

“Mwandishi, Jaji Massati bado hajamtia kitanzi Zombe, ole wake jaji akiwaachia huru nikikutana na mshitakiwa mmoja (jina na liifadhi) nitamshughulikia, polisi wamezoe kuua nao leo wahukumiwe kunyongwa.”

Baada ya hukumu kutolewa nilianza kupokea simu na ujumbe mfupi na wengine wakatoa maoni yao kupitia mitandaoni, pia wananchi baadhi waliokuwa wamefika asubuhi katika viwanja vya Mahakama Kuu siku hiyo na pia baadhi ya waandishi walikuwa wakitamka maneno haya:

“Jaji Massati amehongwa ndiyo maana amewaachia huru washitakiwa, mahakama haitaaminiwa tena, tulitaka Zombe afungwe hata miezi miwili jela, tunaziheshimu mahakama lakini kwa uhuni uliofanywa na Jaji Massati unatulazimu sasa tuzivamie mahakama na kuzichoma moto, hukumu ni nzuri kwani imekata ngebe za wanahabari na wananchi waliokuwa wanashabikia ujinga, Jaji Massati ni shujaa.”

Watanzania wenzangu baadhi ya maoni yaliyokuwa yakitolewa na wananchi hao yalikuwa yanavunja ibara ya 107A ya Katiba ya nchi inatamka wazi kuwa mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano ni Mahakama na ibara ya 107B inasema mahakama zote zitakuwa huru katika utendaji wake na kuongeza kuwa ibara hiyo ndiyo chimbuko la uhuru wa Mahakama nchini.

Pia maoni hayo ya wananchi niliyoyaandika hapa juu, yamenifanya nikubaliane na kauli ya Jaji Mkuu Ramadhan, kwamba baadhi ya wananchi walikwisha kuwatia hatiani washitakiwa hata kabla ya hukumu kutolewa na mahakama.

Lakini sasa nakubaliana na maneno ya Jaji Mkuu ambaye ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwamba uhuru wa mahakama ni kama papa baharini, kwani ndio unaovuma sana na pengine unakera pia.

Pia hukumu ya kesi hii imenifundisha mambo mengi; mosi, imenifundisha kuwa wananchi wengi hawana taaaluma ya sheria.

Hukumu ya kesi hii imenifundisha kufahamu kwamba baadhi ya wananchi wamekuwa wakivunja Katiba ya nchi na sheria bila wao kutambua.

Jambo jingine nililojifunza katika kesi hii, bado tuna tatizo la kutoheshimu taaluma za wenzetu, mwananchi mwenye taaluma ya aina fulani anataka kumkosoa kitaaluma mtu mwenye taaluma nyingine ilhali taaluma hiyo haifahamu hata miiko yake.

Bado serikali yetu na taasisi zinazojihusisha bado zina jukumu la kuhamasisha wananchi wajifunze kusoma Katiba ya nchi na baadhi ya sheria ili kuondoa dhana ya mitazamo mibaya kama iliyojitokeza kwenye kesi hii.

Wakati nikitaja baadhi ya mambo ambayo nimejifunza kwenye kesi hiyo, naendelea kujiuliza, hivi ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) inayoongozwa na Johnson Mwanyika na ile ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) inayoongozwa na Eliezer Feleshi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai inaongozwa na Robert Manumba, kama kweli huwa zinajipanga kukabiliana na mashitaka kama haya?

Kilichosababisha Jaji Massati atoe hukumu ya kuwaachia huru washitakiwa wote ni matokeo ya udhaifu wa upande wa waendesha mashitaka na wapelelezi wetu ambao kwenye ofisi nilizozitaja hapo juu.

Udhaifu uliojitokeza katika kesi hiyo naweza kuulinganisha kwa kiasi fulani na ule uliotokea katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi wa na Utawala, Amatus Liyumba, na Meneja Mradi wa Benki Kuu, Deogratius Kweka, ambapo Mei 27, mwaka huu, Hakimu Mkazi Waliarwande Lema, aliamua kufutilia mbali mashitaka baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa na dosari za kisheria.

Kilichojionyesha katika kuachiliwa huru kwa Liyumba na kisha kukamatwa kwa muda mfupi na kufunguliwa kesi upya, ni udhaifu katika taaluma ya uendeshaji mashitaka kwa mujibu wa sheria za jinai.

Pamoja na kwamba mawakili wa serikali wanaoendesha kesi hizo waandamizi, inadhiirika kwamba taaluma yao kisheria haitoshi.

Je, hii si ishara mbaya katika kesi zote za matumuzi mabaya ya ofisi za umma na wizi wa EPA zilizopo mahakamani hivi sasa?

Je, hivi sasa si kweli kuwa mafisadi ambao hawajafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kashfa ya ununuzi wa rada, ndege ya rais, helikopta za JWTZ, Kagoda, Kiwira, Meremeta, Tangold, wanasherehekea na kugonganisha glasi zao za mvinyo?

Tayari upande wa serikali katika baadhi ya kesi zilizopo katika Mahakama ya Kisutu kwa sisi ambao siku tano za juma tunashinda hapo, tumeshuhudia wameonyesha kubabaika kwa kubadilishabadilisha hati za mashitaka kwa kupunguza mashitaka.

Je, itakapotokea watuhumiwa kuachiliwa huru, si kesi zitakuwa zimekwisha kwa kishindo kile kile kama zilivyofunguliwa kwa kishindo?

Tuseme nini sasa. Usanii mtupu au ufisadi mtupu unaofanywa na mawakili wetu wa serikali na vyombo vya upelelezi?

Kama mawakili wa serikali hawana taaluma ya kutosha kwanini wasiombe ushirikiano wa kitaaluma kutoka kwa mawakili wengine wenye ujuzi, ambapo mawakili wengine binafsi walikuwa walimu wenu vyuoni?

Kama ofisi ya DPP inaona vielelezo walivyoletewa na wapelelezi havitoshi ofisi yake kwenda kufungua kesi mahakamani dhidi ya mshitakiwa, ni kwanini ofisi ya DPP inafungua kesi mahakamani?

Ni rai yangu kwa Watanzania wenzangu sasa kuanza kuzinyoshea vidole bila woga ofisi ya DCI, TAKUKURU, DPP, kwani ofisi hizi zinashirikiana kiutendaji kabla na wakati wa kufunguliwa kesi za jinai mahakamani.

Naamaanisha wananchi wenzangu kufanya hivyo kwani uzembe huu wa wanataaluma kutoka katika vyombo hivyo, mwisho wa siku unalighalimu serikali kwa kulipa fidia kwa walioshinda kesi hizo.

Watanzania kuendelea kupinga hukumu ya Zombe bila kuona nakala ya hukumu na kupanga kuandamana, hakutasaidia chochote, badala yake kelele hizo zinatoa nafasi kwa watuhumiwa wa ufisadi wa Kagoda, Rada na Deep Green kuendelea kupumua.

Kelele hizi tunazoendelea kupiga tulipaswa kuzielekeza kwenye ofisi ya DPP na vyombo vya uchunguzi kuona vyombo hivyo vimefikia wapi kuhusu uchunguzi wa tuhuma hizo.

Nimalizie kwa kuwaasa wananchi wa kada mbalimbali, vyombo vya habari, waendesha mashitaka na wapelelezi wayasome na kuyaelewa maneno hayo ya Jaji Mkuu Ramadhani, kwani kwa watu wenye akili timamu watakubalina na mimi kiongozi huyo hakuwa mwendawazimu, kwa maneno kama hayo alisoma alama za nyakati na hasa alipoona kesi nyingi zinazohusu ufisadi, pembe za ndovu, matumizi mabaya ya ofisi za umma na mauaji, ambazo zinahusisha vigogo na watu wenye nyadhifa kwenye jamii zimefunguliwa katika mahakama anayoingoza.

Maneno hayo mazito ya kiongozi huyo wa juu wa mhimili wa Mahakama nchini, yana tafsiri pana ambayo kwa mujibu wa Katiba ya nchini, mahakama ni chombo huru kinachotakiwa kutenda haki kikamilifu, na kamwe isishinikizwe kumtia hatiani mtu ambaye hana hatia.

Hivyo maneno hayo yanadhiirisha wazi jinsi mahakama ilivyojipanga kusimamia kutokubali kunyang’anywa uhuru wake wa kutoa haki katika kesi za aina hiyo na nyingine.

Hivyo ni changamoto sasa kwa waendesha mashitaka wetu nao pia kutafakari maneno hayo kabla ya kufungua kesi, wasifungue kesi kwa lengo la kujionyesha kwa Rais Jakaya Kikwete na wananchi kwamba nao wanachapa kazi, bali wakumbuke kinachotakiwa mahakamani ni ushahidi ulio bora na si vinginevyo.

Pia nimalizie kwa kuwaombea dua mahakimu na majaji wetu wawe na moyo wa uadilifu, ujasiri na kusimamia taaluma na miiko yao ya kazi katika kusikiliza kesi hizo na mwisho wa siku watoe haki bila upendeleo, kwani tayari kuna minong’ono inaendelea kusambaa kwa kasi mithili ya moto wa gesi kwamba kuna baadhi ya waliokuwa vigogo serikalini na wananchi wa kawaida wamefunguliwa kesi kwa visasi.

Na mbaya zaidi, tuhuma hizi zinasambazwa na baadhi ya maofisa waofisa waliopo kwenye ofisi za umma na wengine wapo kwenye vyombo vinavyohusika na upelelezi na ufunguaji wa kesi hizo.
Inasikitisha sana na kuipaka matope Serikali ya Awamu ya nne ambayo inaongozwa na Rais Kikwete ambaye mara kadhaa amenukuriwa akisema anaheshimu utawala wa sheria na uhuru wa kutoa maoni, ambapo kwa miaka mitatu tangu aanze kuongoza tayari serikali yake imeandika historia ya kuwafikisha vigogo na watu maarufu mahakamani, ukilinganisha na awamu iliyopita.

Lakini historia hii ya kuwafikisha watu wa kada hiyo mahakamani, itakuwa imekamilika vyema pale tu serikali itakaposhinda kesi hizo, lakini kama serikali haitashinda, basi ni wazi Serikali ya Awamu ya Nne itaondoka madarakani ikiwa na sifa hii kwamba, iliwapeleka vigogo wengi mahakamani lakini ikashindwa kesi.

Sasa tuiulize Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Kikwete na watendaji wengine, ipo tayari kuondoka madarakani wakati wake ukifika na sifa hiyo ya kushindwa kesi?

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Agosti 23,2009

1 comment:

Mzee wa Changamoto said...

Dah! Ni kama umesema yote. NIMEJIFUNZA MENGI na naamini wengi wanastahili kujua haya.
Asante Da Happy

Powered by Blogger.